Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Jacquline Andrew Kainja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii niweze kuchangia katika Wizara ya maji, awali ya yote nipende kuishukuru Wizara na kumshukuru Waziri wa Maji kwa kazi nzuri wanayoifanya kuhakikisha kwamba wananchi tunapata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kijikite moja kwa moja kwenye suala zima la kupata maji kwa njia ya uvunaji wa maji ya mvua kutengeneza mabwawa. Nasema hivyo kwa maana ya kwamba katika hotuba ya Mheshimiwa Rais Mama yetu Samia Suluhu Hassan ukurasa wa 29 aliweza kuongelea kuweza kulinda miundombinu ya maji na vyanzo vya maji. Lakini vile vile hakuacha mbali suala zima la kuhakikisha tutatengeneza mabwawa ya kuvunia maji hasa kwa sehemu ambazo hazina vyanzo vya maji vya kutosha zenye ukame. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninatoka Mkoa wa Tabora Mkoa wetu hauna vyanzo vya maji vya kutosha na sehemu ambazo ziko pembezoni akinamama wanateseka sana kupata maji ya kutumia. Lakini niipongeze Wizara kwa Mradi wa Maji wa ziwa Victoria ambao mpaka hivi sasa umefika Tabora Mjini na katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ameeleza kwamba wana mpango wa kupeleka maji katika Wilaya ya Urambo, Kaliua Sikonge. Kwa hiyo, nilikuwa ninaiomba Wizara katika huu mradi wa maji wa Ziwa Victoria mradi ambao umetengewa fedha shilingi bilioni 11 kutoka maji Tabora Mjini mpaka kwenda Jimbo la Igalula Kata ya Kigwa nilikuwa ninaomba Wizara iweze kuangalia hii National Water Fund iweze kuwa inaongeza fedha mradi ni bilioni 11 lakini katika mradi huo wa bilioni 11 mpaka sasa hivi imetoa bilioni mbili kasoro. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unajaribu kuangalia kama kilometa 30 kutoka Tabora kwenda Kigwa na Mradi ni gharama kubwa za bilioni 11 unaanza kuona je, kama hawatoweza kuongeza fedha hawa National Water Fund je, huu mradi unaweza ukaisha kwa muda gani? Lakini vile vile niiombe Wizara iangalie kwamba kwa namna nzuri tukiweza kuwekeza kwenye uvunaji wa maji ya mvua maeneo ya pembezoni inamaana hata gharama ya kutandika mabomba ya maji ya ziwa Victoria kwenda maeneo kama Tarafa ya Kiwele, Wilaya ya Sikonge ambapo kutoka Sikonge kwenda hadi Kiwele ni kilometa 200.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna maeneo ya pembezoni kutoka labda Bukene Mambali kupeleka maji yale kule kama vile maeneo ya pembezoni tukiwawekea mabwawa wananchi wakaweza kuvuna maji ya mvua yale wakatoa maeneo itakuwa imewasaidia akinamama kuhakikisha kwamba tunakwenda na Sera ya kumtua mwanamke ndoo kichwani kwenye uhalisia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile niweze kuipongeza sekta ya maji ya Mkoa wa Tabora ambayo inafanya kazi vizuri kupitia RUWASA kwa jinsi ambavyo kuna mradi ambao ni wa Benki ya Dunia payment for results ambao mara ya kwanza walipewa bilioni 8.5 wakaifanyika kazi vizuri wakachimba visima vya maji lakini hivi sasa tunaona tunaletewa fedha bilioni 21 hii ni kazi nzuri sana inayofanya na sekta ya maji katika Mkoa wa Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuangalie tunapokwenda kwenye Mkoa watu wa Tabora fedha zile tunazopeleka kwenye visima ardhi yetu ni kavu mkandarasi anakwenda pale anachimba kisima kwa gharama kisima kimoja ni milioni 25 lakini akifika chini maji hakuna. Kwa hiyo, tukiangalia namna gani nzuri katika aina mbili ya mradi huu wa Maji wa Ziwa Victoria lakini vile vile tuwekeze kwenye uvunaji wa maji ya mvua ili tuhakikishe mwanamke wa Mkoa wa Tabora tunamtua ndoo kichwani inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaendelea kuishukuru Serikali iweze kuangalia Wizara kuhakikisha mradi ambao umeshatengea fedha wa Bukene maji kwenda ya bilioni sita na mradi wa Nsimbo wa bilioni nne tuhakikishe basi hizi fedha zinakwenda kwa wakati, ili akina mama hao wa Nsimbo kwa Jimbo la Manonga na akinamama hawa wa Jimbo la Bukene na kata zote za mbali Kamangaranga na kwingine kote huko waweze kupata nafuu ya upatikanaji wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo naomba niunge mkono hoja. (Makofi)