Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hotuba hii ya Wizara ya Maji. Kwanza, nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri kijana na machachari ambaye amedhihirisha umwamba wake katika Wizara hii ya Maji. Nadhani ukiona mpaka Mheshimiwa Rais ananukuu yale unayoyafanya maana yake unahakikisha unayasimamia kwelikweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimkushukuru kwa miradi ambayo imeainishwa kwa ajili ya wakazi wa Biharamulo. Nikushukuru kwa mradi ule wa Maziwa Mkuu, nimeona Biharamulo imetwaja; ni mradi wa shilingi bilioni karibu 750 ambayo itahudumia miji inayozunguka Ziwa Victoria na Biharamulo ipo na vijiji vyake, kwahiyo nakushukuru kwa ajili ya hilo. Pia ukurasa wa 149 nimeona miradi ambayo nimetengewa kwa ajili ya Wilaya ya Biharamulo nishukuru, itatutoa hapa tulipo na kutusogeza mbele zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nizidi kukumbushia tu nadhani nilim-consult kwa ajili ya ahadi ya Rais; mradi mkubwa wa kuleta maji katika Mji wa Biharamulo kutoka Ziwa Victoria. Naomba azidi kuukumbuka hata kama bajeti imebana ili shida ile ambayo imekuwepo kwa muda mrefu iweze kumalizika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze kwa nia thabiti ya kutusaidia kwa sababu nilishamuona ameniahidi baada ya bajeti mimi kama Mhandisi na yeye kama mzoefu twende pale tuangalie chanzo ambacho kinatuhudumia sasa hivi ili tuweze kuanza mwanzo mwisho ikiwezekana tupate treatment plant ya kuanzi sasa hivi kipindi ananiandalia mradi mkubwa. Nazidi kukushukuru kwa ajili ya hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa shukrani niweze kuongea mambo machache mengine yatakuwa yangu ya ufuatiliaji kwa ajili ya eneo langu ila kwa sababu ninao uzoefu mkubwa katika sekta hii kwa hiyo napenda kuongea juu ya yale ambayo nayajua na yale ambayo nadhani tukishauri Serikali ikayabeba na wakayafanyia kazi yataweza kweli kutusaidia. Cha kwanza, niipongeze Serikali kwa uanzishaji wa RUWASA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ile ambayo Mheshimiwa Waziri amekuwa akiita ni kichefuchefu; mpaka anawaambiwa watu wachezee vitambi lakini sio miradi, nakumbuka iliyo mingi ni ya BRN (Big Results Now), ndiyo ilifeli wakati ule tukitumia wakandarasi na Halmashauri mkaona solution ni kuja na RUWASA. Kweli RUWASA imetusaidia kwa sababu wakati ule nakumbuka unakuta mkandarasi hajui chochote, mwingine ana stationary na kadhalika na miradi mingi ilikuwa ni ya viongozi hao hao waliokuwa kwenye halmalshauri zile; mainjinia na watu wengine ndio maana ilifeli. Kwa hiyo, tuhuma zile za nyuma tuziache tuku-support tuanzie hapa na RUWASA ili twende mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimejaribu kufuatilia utendaji wa RUWASA, wanafanya kazi vizuri, wote tunajua. Development partners wanatoa pesa kusaidia miradi ya maji vijijini, lakini based on performance. Nimefuatilia nimeona DFID, sasa hivi imetoka shilingi bilioni 23 imeenda mpaka shilingi bilioni 79. Maana yake RUWASA wamefanya vizuri, wame-qualify kwenye vigezo na fedha imeongezeka. Nimeona hata ya World Bank ilikuwa shilingi bilioni 118 nadhani safari hii inaenda mpaka shilingi bilioni 186, hii ni good performance kwa sababu wanafanya wanavyofanya, mkienda kuchujwa kwenye viegezo, inaonekana mme- qualify mmeenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, baada ya kuyaona haya yote na kwamba RUWASA inaaminiwa, ili lisiwe bomu baadaye, maana mwanzo wakandarasi waliharibu. Maana unapoongelea miradi ya maji is purely engineering practice. Huwezi kufanya engineering project bila kuwa na ma-consultant, na watu ambao wanahausika. Hata ukijenga nyumba yako wewe mwenyewe unaita fundi. Wewe sio mjenzi, lakini kuna kipindi unapitia nyumba unamwambia fundi hapa ulivyopiga ripu siyo. Wewe sio engineer wala nini, lakini unaona.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba turudishe practice ile ya ma-engineer. Nimefuatilia nikaona kwamba mpango wa kuchuja wakandarasi unaendelea na ni hatua nzuri sana ambayo inafanywa na RUWASA, kufanya shortlisting ya wakandarasi mkajua kama wana vigezo then twende hatua ya pili ya kuwaamini wakandarasi hawa tuwarudishe kwenye miradi watusaidie.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii miradi ni mingi, hatuwezi kuifanya kwa kutumia force account tu. Ni lazima tu-employ wakandarasi. Kwanza watatengeneza ajira kwa vijana wa Kitanzania na miradi itafanyika haraka kwa sababu wananchi hawa wanachohitaji ni maji. Tukienda kwenye process hii ya muda mrefu, kesho na kesho kutwa tutakwama tena. Maana ni bajeti hii, mwakani utakuja na bajeti nyingine na bajeti nyingine. RUWASA ni mtoto mdogo ambaye mmemzaa hata miaka miwili hajafikisha, kaanza 2019. Mwezi wa Saba ndiyo anaenda mwaka wa pili. Tumwezeshe pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu utakuwa enginee; wote jiografia ya mazingira yetu tunaijua. Hata magari, kuna baadhi ya sehemu hawana magari bado. Kuna baadhi ya sehemu bado hawajaruhusiwa kuajiri. Ni wafanyakazi wale wale waliotoka nao Halmashauri, leo ndiyo wale wale ambao tunawategemea wafanye miradi hii. Sasa tuhakikishe kwamba kwenye bajeti hii tunawasaidia mtafute magari, vijana hawa wakafanye kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepiga kelele sana ya TARURA hapa, lakini miradi haifanyiki mjini. Ni bora sasa hata TARURA tunawafuata wananchi kwenye sehemu ambazo wamelima wenyewe. Wote tunajua, vyanzo vya maji viko maporini, tunatoa maji kwenye mapori tunayatiririsha yanakuja kwenye vijiji au miji. Sasa kama hawana vitendeakazi hawa watu watakwama sehemu. Baadaye tutarudi hapa kuwahukumu, tutaona RUWASA haina maana, tutaazimia kuivunja. Sasa tuwawezeshe. Tukishawawezesha nia hii waliyonayo ni nzuri itaweza kutusaidia.

Mheshimwia Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri with due respect, mimi nimekuwa na uzoefu na nimejaribu kufuatilia hususan kwenye suala la maji. Yapo makampuni ambayo yapo tayari kutusaidia kuhakikisha kwamba tunapata vifaa. Kwa sababu almost asilimia 60 ya miradi ya maji iko kwenye mabomba na viungio, lakini viwanda viwanda vya Kitanzania viko hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumesema tu-engage private companies. Private companies twende tukaongee nao wakubali kutoa mabomba kwa wakandarasi ambao leo tutawaleta hapa. Wakishakubali kutoa mabomba kwa wakandarasi, wakandarasi wafanye miradi ili nyie sasa mtakapoipata fedha mlipe kwenye viwanda moja kwa moja kwa niaba ya wakandarasi. Viwanda vitatoa mabomba hapa na miradi itakimbia. Maana na best practice najua, nawe mwenyewe unajua nimekuwa nafuatilia hayo kwako.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiweza kufanya hivi, kelele kubwa ni vifaa. Mabomba yakishafika site, hamna shida tena. Shida imekuwa kubwa kwa sababu kazi ya kuchimba mitaro na kufukia siyo issue. Mkandarasi anaweza akawa na fedha, lakini kazi ya kununua mabomba pale; unaenda kwenye kiwanda mtu anaambiwa shilingi bilioni 700 au shilingibilioni 800. Wakandarasi wa Kitanzania tunajua, walio wengi wamekuwa wanaandika paper works tu. Ukienda kwenye reality vile vitu havipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuwanyanyue tuwarudishe kwenye mstari wale waliokuwa wameanguka, tukubali kufanya commitment ya Serikali kwamba viwanda vikubali kutoa mabomba, Wizara na RUWASA wasimamie. Mabomba yale yakishaletwa, kateni pesa za viwanda muwalipe waweze kukopesha wengine i-rotate kule miradi hii itakimbia. Hakuna Mbunge hapa atakayekuja kulalamika kwa sababu kila mahali mlipopeleka mkandarasi, ataanza kufanya kazi kwa sababu mabomba yatakuwepo, viungio vitakuwepo, kazi yake ni kuchimba mitaro na kulaza mabomba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, kuna jambo lingine ambalo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Ni kengele ya kwanza eh!

MBUNGE FULANI: Ndiyo.

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, kuna jambo lingine ambalo nimekuwa nalo kwa experience yangu. Nilichokuwa naomba, tujaribu pia kuangalia uendeshaji wa hizi taasisi tulizonazo. Nilikuwa natamani RUWASA iendeshwe kama inavyoendeshwa TANROADS. Ikiwezekana muwape target. Yaani I believe in targets kwa sababu private companies kwa sehemu kubwa tunafanya kazi kwa target. Nimekuwa Nairobi National Water, nimekuwa Uganda National Water nimeona, yaani Mamlaka ya Maji iko responsible kwa Bodi na wana target. Kwa sababu nimekuwa kwenye hii biashara kwa muda, kwa hiyo, nilikuwa nafuatilia sehemu zote. Nimekuwa Uganda na Nairobi, nimeona wanavyoendesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, tujaribu kuwapa target, they have to perform based on targets kwa sababu mtu anapokuwa anafanya kazi na hana target, ndiyo kesho na keshokutwa unakuja kukuta uzembe mdogo mdogo wa mtu mmoja unakuletea kashfa wewe Waziri ambaye unapigana, unamletea kashfa Mkurugenzi Mkuu, lakini kwa sababu tu ya watu wachache ambao wako huko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, muundo huu wa kuunda hii taasisi ni mzuri, lakini twende mbele na turudi nyuma, ni lazima iwe performance based. Tuifanye kama Taasisi separate, tusiifanye kama sehemu ya Wizara, iwe performance based, Bodi ipo, iwajibishe watu wanaoleta uzembe. Kabla ya Rais kukuwajibisha wewe, hebu wewe uanze kuwawajibisha hao watu. Maana nimeona hapa ukurasa wa 29 wa hotuba ya Rais, mambo aliyoyataja kwenye upande wa maji. Usimamizi ametaja mara mbili. Nilikuwa nafuatilia hapa ukurasa wa 79. Usimamizi mbaya na huku kaja tena kwamba, ili kuimarisha usimamizi, atafanya mabadiliko moja mbili, tatu, nne kama alivyotaja hapa. Kwa hiyo, sehemu kubwa ambayo inatukwamisha, ni usimamizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninachoomba ili msimamizi asitafute sababu yoyote ya kukwepa, hebu tuwawezeshe. Tuwape magari na vifaa. Baada ya hapa, usimamizi ule sasa ambao unautaka wewe kupitia RUWASA kwenye Bodi, kupitia RUWASA kwenye Management uende ukatekelezeke huku mtu akiwa hana sababu yoyote ile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine cha kumalizia, wako watu ambao wakati wa nyuma walipata shida kidogo kwenye miradi hii ya maji. Maana wakati ule miradi mingi sana ilikuwa imekwama kama ulivyosema. Miradi karibu 177 mmekuta ikiwa imekwama kabisa kabisa, lakini leo mmetekeleza almost miradi 85 inatoa maji. Sasa unavyoona kazi hiyo kubwa imefanyika kwa muda mfupi na miradi iliyokuwa kichefu chefu, sina budi kukupongeza. Maana nisipokupongeza wewe Mheshimiwa Waziri na RUWASA nitakuwa siwatendei haki. Hotuba nimeipitia, kazi mliyofanya ni kubwa. Tunaojua maji, tunajua miradi ilivyokuwa imekwama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake; nampongeza Naibu Waziri maana amekuwa kila anapoitwa anakubali kufika, kwangu ameshatembelea. Nampongeza pia Katibu Mkuu kwa sababu amekuwa msikivu, unapoenda kumwona yupo tayari kusaidia na Naibu Katibu Mkuu. Kwa hiyo, ni Wizara ambayo kwetu ambao tunajaribu kufanya ufuatiliaji, mmekuwa tayari kutusikiliza na kutuhudumia. Kwa hiyo, haya ambayo yanafanyika hapa na especially kazi ngumu ya kukwamua miradi iliyokuwa imekwama, mnastahili sifa ya pekee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Bunge tuwaunge mkono kwenye bajeti hii tuweze kuipitisha sasa ili yale ambayo wananchi wanayategemea hasa kwenye maji, maana kilio cha Watanzania ni maji; maji ni uhai na bila maji, uhai wetu hautastawi; na tusipopata maji huko tunakoelekea majimboni mnajua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)