Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehma anayenijalia uzima mpaka siku ya leo nimesimama katika Bunge lako Tukufu. Niwashukuru sana wana Nkansi Kaskazini kwa kuendelea kuniamini na kunipa ushirikiano katika kipindi kigumu nachokipitia hivi sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na suala la Mradi wa Ziwa Tanganyika. Mheshimiwa Waziri kabla sijazungumza jambo hilo na mimi nikupongeze kwa kwa uthubutu na namna ambavyo unawajibika kwenye Wizara yako, pamoja na Naibu wako, mnafanya kazi nzuri. Hata hivyo, kazi nzuri zitaonekana kwa vitendo, tunatamani kuona maji siyo maneno.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua mchango wa Serikali kwenye Jimbo langu la Nkasi Kaskazini katika suala zima la kupeleka maji lakini pamoja na jitihada hizo za Serikali bado kuna changamoto kubwa. Tunapozungumzia upatikanaji wa maji vijijini, Nkasi Kaskazini ni miongoni mwa majimbo ambayo yapo pembezoni na maeneo hayo Kata zote zinatoka vijijini. Serikali imetuletea kiasi cha fedha; Kata ya Kabwe kuna mradi wa maji wa bilioni 1.4, Kata ya Kilando bilioni 1.3, Kata ya Namanyere bilioni 1.7, lakini ukiangalia miradi yote hii, haiwezi kutatua changamoto ya maji hata robo ya Jimbo la Nkasi Kaskazini. Ndiyo maana tunasema kwa kuwa Mungu ametujalia kuwa na mito, maziwa na bahari kwa nini tusitumie vyanzo hivyo ambavyo ni vyanzo vya uhakika? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna jambo linaniumiza naamini na wewe Mheshimiwa Waziri linakuumiza, wakati huu ndani ya Bunge tunazungumzia mafuriko na shida ya maji, kuna shida gani? Mungu ametujaliwa mvua za kutosha, lakini wakati huo ambao tunazungumzia mvua za kutosha zina athari zake lakini tunatumiaje sisi hiyo neema ambayo Mungu ametupa ya mvua nyingi kuweza kuvuna maji tukaepukana na hizi athari ambazo zipo leo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutoka Kilando ambako ndiko chanzo cha Ziwa Tanganyika kwenye Wilaya yangu ya Nkasi ni kilometa 64 kufika Namanyere, leo tunazungumza habari ya maji miaka nenda rudi. Kuna vitu ambavyo hatuhitaji kutumia nguvu zaidi, nimezungumzia kata tatu tu juu ya miradi inayoendelea hivi sasa ambayo haiwezi kumaliza changamoto hata robo kwa nini tutumie hiyo miradi midogo midogo ambayo haiwezi kumaliza changamoto badala ya kuja na fedha ambazo tunaamini kwamba tukitumia chanzo cha Ziwa Tanganyika hatutazungumzia wanufaika Nkasi peke yake, tutazungumzia Sumbawanga DC, Sumbawanga Mjini, Kalambo, mkoa mzima wa Katavi lakini itaunganisha na Mkoa wa Songwe. Kwa hiyo, tunazungumzia mradi wa uhakika ambao Serikali mkikaa utatusaidia. Pamoja na kwamba utatumia gharama kubwa lakini ni mradi ambao utakwenda kuwanufaika wananchi wengi na habari ya maji itakuwa historia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto hiyo lakini hata hivi fedha chache tunazopeleka usimamizi wake ukoje? Pamoja na kwamba kuna mambo ya ajabu yanayofanyika kwenye miradi ya maji, lakini bado kuna changamoto ya watumishi, yawezekana hata waliopo uwezo wao ni mdogo; hao waliopo ni wachache hawawezi kutatua hizo changamoto za maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali, pamoja na kwamba uhaba upo wa kutosha Serikali ni moja, Wizara ya Utumishi kama kweli maji ni kipaumbele lazima itoe vibali vya kuajiri watu hawa na watu hawa wapo shida ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitapenda kumshauri tena Mheshimiwa Waziri hata wale watumishi wachache waliopo Wizara ya Maji wanatakiwa kupewa training. Yawezekana kuna maeneo ambayo sisi labda tuna bahati mbaya, tunapotumia wale local fundi wanafanya kazi nzuri lakini wale pia wanahitaji angalau wapewe elimu ya kila wakati waweze kutusaidia. Hata hivyo, kwa nini tutumie wale kama wapo waliomaliza wapo mitaani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie miradi hiyo ya maji, pamoja na kupeleka fedha ni vizuri tukawa na utaratibu wa umaliziaji wa miradi hiyo tunayoianzisha. Tunaanzisha miradi mbalimbali tunaiacha. Tunapopeleka fedha tunataka ku-achieve nini? Tunataka kumaliza changamoto ya maji. Kama hilo ndio lengo kwa nini hatufiki mwisho kwenye hiyo miradi ambayo tunaianzisha? Tusifikirie kuanzisha miradi mipya wakati hii tuliyonayo bado hatujaweza kufikia hitimisho na kufikia lengo ambalo tulikusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia kwa mfano ule Mradi wa Namanyere, toka mwaka jana wananchi hawapati maji. Tunaambiwa habari za pump, pump ni shilingi ngapi Mheshimiwa Waziri? Mnapokuwa mnafanya upembuzi si mnajua kwamba hapa kunahitajika pump? Inakuwaje mnafika mwisho mmefanya kazi mpaka asilimia 70 watu wanakaa miezi saba, miezi nane, mwaka mzima hawajapata maji kwa sababu ya pump, nini tunafanya? Natambua namna ambavyo unawajibika, lakini kuwajibika kama watendaji wako hawawajibiki kama wewe tutabaki kupiga story tu ambapo hazitatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Nkasi Kaskazini tuna kata 17; hakuna kata hata moja yenye uhakika ambayo unaweza kusema tunapata maji. Mimi leo nitakupongeza kwa sababu ya uthubutu lakini tunapata shida sana kwenye Wizara yako ya Maji na inashangaza ni kama kilometa 64 kutoa maji Ziwa Tanganyika lakini mpaka leo tunalia juu ya maji, nafikiri hili haliko sawasawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika ugawaji angalieni utaratibu ni vigezo gani mnavitumia kwenye kugawa miradi ya maji. Kuna maeneo mengine tunapata changamoto na tunaanza kujifikiria shida itakuwa ni nini. Naomba nizungumzie katika hizohizo kata ambao zina miradi; Vijiji vya Itindi, Masolo, Lyele, Kanazi, Misunkumilo, Kolongwe, Kalila, Matine, Mkombe, Mpenge hayo maeneo yote hayana maji kabisa. Nakuomba utapokuwa unahitimisha hapa natamani na wewe ukaone yale maji yenye rangi ya njano ambayo wanakunywa wananchi wangu, uone kama kweli tunawatendea haki wananchi hawa. Ni Watanzania kama wengine na wanastahili kupata haki na ni wajibu wa Serikali kuwapelekea huduma ya maji ambayo ni safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)