Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa kuchangia katika Wizara hii ya Maji na nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji ndugu yangu Mheshimiwa Aweso, pamoja na Naibu Waziri, Engineer Maryprisca. Lakini pia nimpongeze Mkurugenzi Mkuu wa DAWASA kwa namna ambavyo anatuhudumia Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa shukrani, naishukuru Wizara ya Maji pamoja na Serikali kwa kukamilisha mradi wa maji wa Kisarawe, kwa kukamilisha mradi wa maji Mkuranga, lakini kwa ahadi yake ya kuanza upembuzi yakinifu ya kutoa maji ya Mto Rufiji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni imani yangu wanawake wa Mkoa wa Pwani wa Wilaya hizo, watapata tija kubwa na tunaweza kuwatua ndoo kichwani. Sambamba na hilo niishukuru Wizara pamoja na DAWASA na pia kumshukuru sana Rais aliyepita Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa maelekezo ya mradi mpya wa kutoa maji Ruvu, Chalinze - Mboga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika mradi huu kazi inaendelea, lakini wana Chalinze pamoja na mchango mzuri wa Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo wameniomba pia niombe kasi ya mradi huu iongezeke. Usambazaji wa maji katika maeneo ya Bwilingu, Chalinze Mjini, Pera, Nero na uunganishaji wa wateja wanaomba kama ambavyo Mkurugenzi Engineer Luhemeja ametuambia inawezekana mpaka tarehe 30 Mei, 2021 mradi huu ukikamilika basi ukamilike kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine ni wa kawaida maombi ya wanawake, pamoja na miradi mingi ya maji lakini gharama za kuunganisha maji ni kubwa sana laki tatu. Wanawake wengi wa vijijini hawawezi kumudu kuitoa kwa wakati mmoja, wanaomba pengine ilipwe kwa installment. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, wanawake wameniomba niombe Wizara ya Maji pamoja na Taasisi zake, itoe elimu kwa namna ambavyo wanasema umetumia unit ngapi, mahusiano yake na ujazo wa maji. Kwasababu, yapo malalamiko ya bili kuwa kubwa na Mheshimiwa Waziri amekuwa akilisemea mara kwa mara, kupitia elimu hiyo wanaweza wanawake na watumiaji wa bili wakawa na uhakika na bili zinazowasilishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la tatu, wanawake pia wameniomba, utaratibu pengine wa Wizara ya Maji na Taasisi zake, zianze kutumia prepaid meter kwa ajili ya uhakika wa kile kitu ambacho unatumia maji hayo. Lakini sambamba na hilo, wanawake wameniomba pia na wananchi wa kawaida kwamba, inapotokea na hili hata Katibu Mkuu mama Queen Mlozi ndio amenitumia hapa. Inapotokea umehamia nyumba ambayo mtumiaji alikuwa halipi bili, bili hiyo inapewa kwa mtu aliyehamia kwa hiyo, Wizara na Taasisi zake ziweke mkazo katika kuhakikisha wanakusanya bili kwa mhusika. Lakini kumpa deni ambaye hahusiki na usipolipa maji yanakatwa hilo limelalamikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la nne pia, wananchi wa Kata ya Mpangani, Kibaha Mjini tuna mradi mkubwa wa machinjio na DAWASA walituahidi mradi mkubwa pale, ni miaka mitatu sasa mradi haujajengwa. Na machinjio yale halmashauri inatumia pesa nyingi zaidi ya milioni 40 kwa maji ya ma-bulldozer haya ukizingatia na mapato tu ya milioni 60 kwa hiyo, tunaomba hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa, pamoja na hotuba ya Waziri kuainisha changamoto mbalimbali, lakini ipo changamoto ambayo hata Mheshimiwa Rais aliisisitiza, matumizi mabaya ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya upatikanaji wa maji safi na salama. Nikuombe Mheshimiwa Aweso, unawazingua wanaokuzingua, lakini kwenye hili la matumizi mabaya naomba endelea na kasi ya kuwazingua. Katika mapitio machache tu ya taarifa ya CAG naomba ukawazingue watu wafuatao: - (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri kwanza, katika ripoti ya CAG licha ya kwamba tutapata fursa ya kuijadili, lakini kwa kuwa imeainisha matumizi mabaya usichelewe hapa:-

(i) Kuna fedha zaidi za bilioni mbili na milioni 200 zimetumika kwa matumizi mengineyo, ukurasa wa 64 wa taarifa ya CAG ya ukaguzi maalum na amesema mchukue hatua za kisheria;

(ii) Kuna miradi ya thamani ya bilioni nne na milioni 700 haifanyi kazi, haitoi huduma, CAG ameomba mkachukue maamuzi;

(iii) Kuna miradi ya bilioni moja ambapo malipo yamefanyika kwa kazi ambazo hazikufanyika ni ufisadi, kawazingue Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

(iv) Kuna miradi ambayo wakandarasi wameisababishia hasara Serikali na mapungufu ya zaidi ya bilioni 10, nakuomba Mheshimiwa Waziri kashughulikie, kawazingue. Kwasababu, tunazungumza hapa namna tutakavyoongeza mfuko wa Taifa wa maji vijijini lakini tusipofanya jitihada za kutosha kwa hiki kidogo kinachotengwa, zaidi ya bilioni 680 unaziomba leo za maendeleo kwa ajili ya miradi ya maji. Tusiposhughulika na mchwa hawa kwa wakati ni wazi tunaweza tukaona kila siku hela nyingi zinatumika lakini miradi haitoi tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Aweso kasi yako nzuri, Naibu Waziri Engineer anafanya kazi vizuri. Lakini na sio wahandisi pekeyake shirikiana na Wizara ya TAMISEMI wameanza kazi vizuri na wao, hatua zinachukuliwa na mamlaka zingine. Pia, nimemuona Waziri wa Utumishi naye akiagiza TAKUKURU ipitie miradi mbalimbali. Kwa kweli, kama tusipopata muarubaini wa kupambana na pesa zinazotumika vibaya kwenye miradi, tutaona kwamba hela nyingi zinatumika na miradi haifanikiwi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, Mradi wa WAMI Awamu ya Tatu Chalinze tunapongeza hatua ya Serikali ya kusitisha mkataba na kumpa mkandarasi mpya kazi inaendelea. Lakini kuna maeneo kwa mfano, vitongoji vya Ludiga, Kwaruhombo, Kata ya Kibindu nao tunataka wapate maji ya bomba, maeneo ya Ubena aliyosema Mheshimiwa Mbunge na nakazia hapo hapo naomba mradi huu kama ulivyokusudiwa kwamba utakamilika mwaka huu mwishoni basi ukamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno haya nakushukuru sana kunipa nafasi naipongeza Wizara hii, nampongeza mama yetu mama Samia, nina uhakika atawatua wanawake ndoo kichwani. Na ninamtakia kila la kheri ahsante sana. (Makofi)