Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Jeremiah Mrimi Amsabi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Serengeti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ya kuchangia Wizara ya Elimu. Nazidi kushauri na kupendekeza Wizara hii kupewa fedha zilizoombwa na kuona uwezekano wa kuiongezea fedha nyingi Zaidi. Hii ni kwa sababu Wizara ya Elimu ni moja ya Wizara pekee zinazoweza kuzifikisha nchi yetu mahali tunapopata. Nasema haya kwa sababu ukiangalia hata katika Dira ya Maendeleo ya Taifa letu ya 2020 – 2025, katika yale malengo makubwa matano tuliyokuwa nayo, malengo yote matatu yanategemea sana elimu ili tuweze kufikia huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi imeonyesha tunahitaji kutoa zaidi ya ajira milioni nane na hizi ajira kwa hakika zitatokana na uboreshaji mkubwa wa elimu. Pia ni dhahiri kuwa, tafiti nyingi zimefanywa, kwa mfano utafiti mmoja wa ending poverty in India uliofanywa na Profesa Ramanuja umeonesha hakuna nchi yoyote inaweza ikaendelea zaidi ya maendeleo yake katika elimu. Kwa hiyo niombe tutenge fedha nyingi ili kuona tunaweka vizuri katika elimu

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Waziri kwa kazi kubwa ambayo wameifanya kwa miaka mitano iliyopita pamoja na Wizara yote kwa ujumla, lakini niombe kuchangia mambo machache kwa ajili ya kuboresha zaidi na kufikia matarajio ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Wizara ikawekeze zaidi katika bajeti hii kuona tunapata Walimu wa kutosha. Shule zetu nyingi hazina Walimu wa kutosha, katika jimbo langu la Serengeti ukienda shule nyingi Nagusi, Serengeti, Machochwe na zingine nyingi hazina Walimu wa kutosha. Walimu wengi imeonekana wanaoletwa katika Jimbo la Serengeti, wanahama, wanaobaki ni wachache.

Sasa wakati tunajipanga kujenga nyumba za kuishi pamoja na mazingira kuboreshwa Zaidi, niombe Wizara ishirikiane na Wizara nyingine kuhakikisha kuwa Walimu wanaojitolea ambao wanatoka mazingira yale, tuweze kuwapatia kipaumbele katika ajira na mie niko tayari kutoa ushirikiano mkubwa kwa Waziri ili kuona kuwa tunawaajiri vijana wale.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri pia tuwekeze zaidi katika maabara, vitabu na mabweni. Shule yoyote ya sekondari isiyokuwa na vitabu vya kutosha na maabara ni sawa na kujenga bwawa la kuogelea lisilokuwa na maji. Na shule zetu bila kuwa na maabara, bila kuwa na vitabu watoto hawa tusitarajie kuwa na elimu tunayoitaka. Kwa hiyo, niombe fedha nyingi iende kuwekezwa huku.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tuangalie kwasababu ya changamoto ya fedha kutotosheleza, katika jimbo langu na majimbo mengine ambayo wamejenga maboma ya maabara, maktaba pamoja na mabweni ziende kupewa fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunakamilisha mabweni, maabara pamoja na maktaba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jimbo langu shule za Sekondari za Serengeti na Dagusi, Shule ya Msingi Mugumu, Kitunguruma, Machochwe, Kisaka, Ngoremi wameshajenga maboma pamoja na shule nyingine nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende pia kushauri kwamba ili tufikie ajira milioni nane, sasa Wizara iende kuweka kipaumbele kikubwa katika ujenzi wa vyuo vya VETA, VETA zinahitajika sana ili tufikie lengo hili la ajira milioni nane. Kwa hiyo, niwaombe Wizara twende kufanya kazi kubwa. Katika jimbo langu tayari tumetenga maeneo yapo ya kutosha na tupo tayari kutoa ushirikiano unaohitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri kuhusu mitaala, tumelalamika sana, tumezungumza kuhusu elimu na Watanzania wengi wanaona kuna shida. Sasa wakati mwingine sit u kwamba kutoa degrees nyingi ni shida, lakini shida kubwa naiona katika suala la mitaala, mitaala yetu mingi ambayo tunaitumia, hasa ile ya knowledge-based education and training haiwezi kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mitaala ya competence- based education (CBET) pamoja na outcome-based inaweza ikatusaidia. Mitaala hasa inayosimamiwa na NACTE inaweza kufanya vizuri sana. Kwa hiyo niiombe sana Wizara iangalie namna ya kuipa nguvu NACTE kuweza kusimamia mitaala hii. Na process ya utengenezaji wa mitaala, hasa katika situation analysis tuweze kwenda kuwekeza vizuri sana katika eneo hili. (Makofi)

Niishauri pia Serikali kuangalia vizuri suala la uongozi au management ya elimu. Leo ukiona katika shule nyingi walimu wakuu ndio hao sasa wamekuwa manesi, wahasibu, wamekuwa pia kama matron. Sasa kazi hii inawafanya ile core business yao iweze kuwa shifted. Tuombe sasa katika hizi shule tupeleke wahasibu, manesi na watu wa kusaidia shughuli nyingine, wakuu wa shule washughulike na kazi yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia shule zetu nyingi sasa na Wizara yetu tunaangalia sana suala la matokeo ya mitihani zaidi ya process ya ufundishaji. Naomba management ya elimu sasa i-focus kwenye process ya ufundishaji.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niombe sana Wizara iweze kuhakikisha wanazipatia TCU na NACTE nguvu zaidi zitusaidie katika ubora wa elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)