Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru, sambamba na hilo nimshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehma na Utukufu kwa kutujaalia uzima na uhai. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mwezi Mtukufu wa Ramadhan niwapongeze Watanzania na Waislam wote ulimwenguni kwa kukaribia kumaliza mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan. Tunawatakia kila la kheri na mafanikio makubwa kuelekea kwenye Eid El-fitri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeza wizara kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaifanya katika kuboresha suala zima la elimu yetu ya Tanzania. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kila bajeti lazima watenge mafungu kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu pamoja na kutoa nafasi za ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba miundombinu imeboreshwa lakini kuna changamoto nyingi katika miundombinu hii ikiwepo suala zima la maabara, madarasa, vyoo vya walimu, vyoo vya wanafunzi na miundombinu mingine mbalimbali na hasa nyumba za walimu. Changamoto hizi haina maana kwamba hakuna kilichofanyika kuna mambo mengi na makubwa yamefanyika lakini hakuna mambo utakayoweza kuyamaliza kwa wakati mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, elimu ni msingi wa kila kitu katika maisha ya mwanadamu. Mwanadamu asipokuwa na elimu kwa kweli anakuwa yupo nyuma. Nikirejea kwa Nabii wetu Muhammad (S.A.W) alipopewa Utume, alisema mimi siwezi kusoma. Mwenyezi Mungu akamwambia usiwe na wasiwasi kwa sababu alipewa ule Utume ili awaongoze Waislam au wafuasi wake. Mwenyezi Mungu akamteremshia Sura inaitwa Iqra bismi rab bikal lazee khalaq kwamba nenda kasome na alipomwambia asome hakumwambia asome kitu kimoja, alimwambia soma mpaka China. Leo China ni nchi inayoongoza kwa sayansi na teknolojia katika ulimwengu huu wa leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nini mantiki ya kuyasema haya. Tunaboresha elimu yetu kama Nabii Muhammad asingekuwa na walimu wa kumfundisha asingeweza kupata mafanikio makubwa. Sasa kwa mukhtadha huu nataka nichangie kuhusu udhibiti wa elimu na upungufu wa walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukianzia kwenye suala la walimu. Tunampongeza Mheshimiwa Waziri wetu Profesa Ndalichako pamoja na timu yake ya wataalam na wametuambia kwamba kuna mkakati madhubuti wa kuongeza walimu katika nchi yetu ya Tanzania yaani kutoa vibali kwa ajili ya ajira na vibali 6,000 vitatolewa. Sasa vibali 6,000 vikitolewa maana yake ni nini? Tuna walimu 6,000, tuna halmashauri 185, kwa uwiano ina maana kila halmashauri itapata walimu 32.43. Walimu hawa kwa kweli ni wachache sana ukilinganisha na uhaba wa walimu tuliokuwa nao. Ushauri wangu hapa ni nini? Ni lazima tuongeze walimu wengi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada kuyasema hayo, nikubaliane na Kamati yangu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusiana na changamoto zilizopo. Niongelee Udhibiti wa Ubora. Hiki chombo ni muhimu sana tena sana ni sawasawa na Taasisi ya CAG. CAG bila kuwepo ina maana kwamba upungufu mwingi uliojitokeza katika maeneo mbalimbali usingeweza kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwalimu kazi yake ni kuandaa somo na kulifundisha. Lazima awe na Scheme of Work na Lesson Plan. Akishafundisha atajitathmini yeye mwenyewe. Sasa pamoja na kujitathmini yeye mwenyewe, hatutaweza kuboresha elimu kama hakutakuwa na wadhibiti ubora ambao watakuwa wanapita shule nyingi mbalimbali hapa nchini kuona je, alichokiandika huyu mwalimu na jioni akakitathmini ni sahihi? Maana huwezi kuandika kitabu ukakihariri wewe mwenyewe na ukahariri mara ya kwanza, ya pili na ya tatu. Kwa hiyo, mwalimu huyu anatakiwa awe na hiki chombo ili ajione kile alichokifanya ni sahihi au siyo sahihi? Kiko sawa au hakiko sawa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mdhibiti ubora ili aweze kufanya kazi yake vizuri zaidi ni lazima awe na vitendea kazi. Awe na bajeti inayojitosheleza. Akiwa na bajeti hiyo, ina maana kwamba atafanya kazi yake kwa umakini zaidi na kuhakikisha kwamba shughuli inakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye uhaba wa walimu, kwa mfano, ukienda kwenye jimbo langu la Mchinga peke yake, tuna uhaba wa walimu chungu nzima. Ninachoshauri, walimu hawa wanapopangwa vile vile tuwapange walimu wa kike. Kwa mfano, shule yangu ya Nangaru haina mwalimu wa kike hata mmoja. Binti akiingia kwenye ule mfumo wake wa kwenda kule angani, au ndiyo imeingia sasa hivi, anaongea na nani? Kwa hiyo, tunapopanga tuhakikishe kwamba walimu wa kike wanapewa nafasi kwenye shule zetu nyingi zilizopo hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenda angani, maana yake kuwa katika kipindi cha hedhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)