Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi asubuhi ya leo niweze kuchangia.

Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema. Nianze kuchangia kwenye issue ya kubadilisha mtaala. Kwangu nafikiri Serikali inatakiwa ifanye hili jambo kwa utulivu kwa kusikiliza wadau, ninachoona elimu yetu ya Tanzania wakati mwingine inaathiriwa sana na matamko ya kisiasa. Mwanasiasa mwenye madaraka akiamka asubuhi analolifikiria yeye bila kufuata ushauri wa kitaalam kwasababu, kwenye elimu kuna mambo mengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia kubadili mtaala sio jambo la siku moja. Tunatakiwa tufanye need analysis kwa nini huu uliopo haufai na kama haufai tunaongeza nini au tunapunguza kitu gani? Sio suala la kuamka siku moja ukasema watoto wasijifunze hiki wajifunze hiki na kunatakiwa kuwe na taratibu lakini kuwe na maandalizi. Kwa sababu, unapobadilisha mtaala ukumbuke unatakiwa walimu nao uwafundishe waweze kwenda kuutekeleza ule mtaala ambao wewe unautaka. Lakini unakwenda kubadilisha mtaala elimu za msingi, walimu ngazi ya cheti wanafundishwa yale yale ya zamani, hiko ndio kilichopo sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fuatilia mtaala wa ngazi ya cheti unaofundishwa, halafu fuatilia mambo tunayoyataka watoto wetu wa shule za msingi wayasome. Kwa hiyo, ninachoomba tufanye mambo kwa utulivu tuangalie, tumetoka wapi? Tuko wapi? Na tunataka kwenda wapi? Tuache mihemko tuna wataalam wazuri kweli kweli tuepuke mambo ya kisiasa.. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda kuzungumzia Idara ya Udhibiti Ubora, kwangu natambua sana umuhimu wa Idara ya Udhibiti Ubora, lakini kila tukisimama humu ndani hata ukisoma hotuba ya kamati imeeleza wana changamoto kubwa ya fedha. Tunaweza leo tukaona udhibiti ubora hawafanyi kazi zao sawasawa pamoja na mambo mengine, lakini wanakosa bajeti ya kutosha. Ili mtu aweze kukagua ni lazima afike, anafikaje kama hana gari, hana mafuta, hana vitendea kazi ama watumishi wachache? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anajua namna Idara hii ilivyo na changamoto ingawa kuna baadhi ameanza kuzitatua. Nikiri kwasababu, nafuatilia najua kuna baadhi zimeanza kutatuliwa lakini nguvu zaidi inahitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kitu kingine ninachotaka kusema, kila mtu anahitaji watoto wasome, yaani mimi Tunza ukiniuliza ninahitaji wamakonde wenzangu kule kwetu wasome. Lakini, issue inakuja mdhibiti ubora yeye ana checklist ili asajili shule kuna vigezo ambavyo vimewekwa. Shule iwe na choo, iwe na madarasa mangapi, iwe na ofisi, iwe na madawati, kuwe na vitabu, kuwe na walimu kuwe na nini, anaweza kuisajili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sio kwamba akikuta tu wanafunzi wamekaa wanasoma anaweza kusajili. Sasa pendekezo langu kwa Wizara, tunataka wasome lakini pia tunataka wasome katika mazingira bora. Kwasababu, tendo la kujifunza linahitaji mazingira bora tusichukulie tu kwamba, watu tunataka wasome no! Tunataka wasome katika mazingira bora. Labda, kwasababu, population inaongezeka mahitaji ya watoto kusoma ni makubwa. Labda tuangalie mrudi kwenye zile checklist ikiwezekana basi hizi shule zipangwe kwa madaraja. Kwamba, hii imesajiliwa imekidhi vigezo vyote, hii tumeisajili tunaipa uangalizi miaka mitatu, hii tunaisajili tunaipa uangalizi mwaka mmoja urekebishe hiki na hiki na hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, labda twende kwa mtindo huo tunaweza tukafanikiwa, lakini tukiacha tu kwamba kila shule mtu akitaka isajiliwe basi isajiliwe, hata kama haijatimiza vigezo maana yake ni nini? Tunaweza kwenda kusajili shule lakini zikatoa elimu ambayo sisi hatukuitarajia. Matokeo yake tukija humu ndani tena tutakuja kulalamika kwamba, watoto wetu wanajifunza lakini hawaelewi hawawezi kuajirika kumbe tumeharibu msingi tangu kule wakati tunasajili zile shule zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hilo suala kwasababu, tunataka watoto wetu wasome ni suala la kukaa wakaguzi waangalie namna gani wanakwenda kuweka vigezo mbalimbali na shule zingine ziwe kwenye uangalizi ili kusudi watoto wasikose kusoma lakini pia wasome katika mazingira ambayo yataweza kuwafanya wao wajifunze vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda kumalizia kwenye hoja ya vyuo vya ualimu. Natambua kwamba, Serikali kuna baadhi ya jitihada imefanya ikiwemo kuboresha majengo ya vyuo vya ualimu. Kwa mfano, Chuo cha Ualimu Mtwara kawaida kweli majengo yameboreshwa, lakini uboreshaji ule wa majengo yale uende sambamba na uboreshaji wa maslahi ya wafanyakazi. Unaweza ukawa na majengo mazuri lakini wafanyakazi waliopo pale kama huwatekelezei matakwa yao kwa mujibu wa sheria, wafanyakazi wa vyuo vya ualimu hata annual increment ya mishahara yao ni shida. Hata kupata pesa za likizo, kupata nauli, kupandishwa madaraja, kulipwa kwa wakati kwao ni shida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wale wafanyakazi wa vyuo vya ualimu wakufunzi ni watu wa kuwaangalia kwa jicho la pekee. Kwasababu, elimu yote tunayozungumza shule za msingi ndio wao wanakwenda kutengeneza walimu. Lakini pia, Mheshimiwa Waziri namuomba akaangalie namna mtaala wa grade A ule wa cheti, unavyoendana na mabadiliko yanayofundishwa shule za msingi. Kama kuna gap tunaomba hilo gap walitoe kwasababu, nimekuwa nikifuatilia sana wakufunzi wanalalamika kwamba, kile kitu ambacho kiko huku kwenye ngazi ya cheti, ni cha zamani ukilinganisha na kitu ambacho kinafundishwa shule za msingi sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini zile TRCs, Teachers Resource Centers naomba zitumike kwasababu, niliongea hapa hata kisu kinatakiwa ukikinunua unakitumia baadaye unakinoa kuongeza makali yake. Kwa hiyo, zile TRCs zilikuwa zinasaidia walimu kufanya mafunzo kazini, wanakwenda pale wanaongezewa maarifa kwa hiyo, mambo yanakwenda vizuri. Naomba uangalie sana Idara ya Ukaguzi kwa jicho la pekee kwasababu, Idara ya Ukaguzi ndio CAG wa elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo machache nakushukuru sana. (Makofi)