Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze tu kwa kusema ukisikiliza toka asubuhi mijadala ya Bunge letu hili Tukufu, Bunge la Kumi na Mbili, lakini pia ukisikiliza wadau wanavyozungumzia hasa kwenye wizara na sekta nzima ya elimu; utagundua wote tunajikita kwenye sera ya elimu yetu ilivyo kwa maana sera ya mwaka 2014.

Mheshimiwa Spika, pia tunazungumzia mfumo wa utoaji wa elimu nchini namna ulivyokaa. Ukisikiliza hotuba ya Mheshimiwa Rais, alivyozungumza juzi kipindi anahutubia Bunge, amezungumzia namna Serikali ilivyojikita kwenda kupitia Sera ya Elimu Nchini. Hata hivyo, sote hapa ni mashahidi huko tunapotoka kwenye majimbo, kwenye maeneo yote ya mijini, namna ambavyo wananchi na wadau mbalimbali wamekuwa wakizungumzia muundo na Sera ya Elimu ilivyokaa na namna gani ambavyo wameshauri jinsi ya kutoka hapa.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaenda kwenye kuchangia. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kwenye majumuisho yake, kwa sababu leo tunajikita kwenye bajeti, basi kama haitatupendeza, Bunge hili la Kumi na Mbili kwa mikutano inayofuata Mheshimiwa Waziri waende kama Serikali, waende wakaanze mchakato wa kukaa na wadau, kuona namna gani ya kuifumua Sera ya Elimu na mfumo mzima wa elimu namna ulivyokaa ili Bunge linalofuata kwa maana kikao kinachofuata iwe kama section, iwe ni sehemu maalum ya kujadili namna ya mfumo na Sera ya Elimu jinsi ilivyokaa, kwa sababu pale tutakuwa na uwanja mpana wa kujadili elimu yenyewe kama ilivyokaa Nchini Tanzania.

Mheshimiwa Spika, pili, tutakuwa tunazungumzia yale ambayo wao wamekaa na wadau angalau wamepata mawazo yote kwa ujumla ili Bunge lako Tukufu, hili Bunge la Kumi na Mbili, tutoke na maazimio namna gani tunakwenda kufumua mfumo mzima wa elimu ili tutakapokuwa tunazungumza kama Wabunge tuwe angalau tumeshiriki kwenye hili ambalo kimsingi ukitazama kila mtu anayezungumza, anazungumzia namna ya mfumo na sera jinsi ilivyokaa ya utoaji elimu nchini.

Mheshimiwa Spika, naomba sana Waziri atakapokuja angalau atuahidi hiyo, kwamba angalau baada ya Bunge hili watakapokwenda waweze kuangalia namna gani tunaweza tukarudi mara ya pili kwenye vikao vinavyofuata ili tuweze kulijadili hili kwa upana wake na kwa ujumla ili tutoke na kitu kimoja kama Taifa ambacho kitakuwa na mustakabali mzuri wa kutuongoza kwenye sekta ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maoni hayo, nirudi tu kuzungumzia masuala baadhi ndani ya jimbo langu. Nilikuwa natamani sana Wizara ya Elimu na Wizara ya TAMISEMI wafanye kazi kwa ukaribu sana kwa kushirikiana. Leo ulikuwa unazungumza hapa asubuhi, kuna mahali ukienda ndani ya jimbo langu mathalan, mimi nina shule mbili ambazo moja imejengwa tangu 2005, wamejenga wananchi kuanzia msingi. Wamejichangisha wenyewe wamejenga msingi, wamejenga maboma zaidi ya matano kule, lakini namna ya kupewa idhini sasa ya kufunguliwa iwe shule, kwa maana ya kufanya usajili mpaka leo ninavyoungumza hawajapewa usajili. Kila wakienda kwa hawa mabwana ambao wanajiita watu wa ukaguzi wanawaambia bado ongezeni majengo mawili. Unaweza ukatazama maboma matano na choo na ofisi za Walimu wamejenga wananchi, hapa Wabunge wengi wanatoka maeneo ya vijijini wanajua namna inavyokuwa kwa wananchi wakati mwingine kwenye kuchangishana ili kujenga haya maboma.

Mheshimiwa Spika, wakati mwingine mtu ana-sacrifice, alikuwa ana shilingi elfu moja, anaacha kwenda kununua mboga yake, kununua mahitaji yake ya ndani anachanga ili aweze kujenga ile shule. Badala yake wanapomaliza bado hatuwezi kuwapa usajili kwenye shule hii. Nini maana yake? Unakuta shule nyingine ambayo mwanafunzi anatakiwa kwenda ipo zaidi ya kilomita tano kutoka maeneo wananchi wanapoishi na wakati mwingine katikati ya maeneo hayo kati ya shule na wananchi wanapoishi kuna majaruba ya maji. Ili mwanafunzi huyu wa miaka saba au nane aweze kufika kule wakati mwingine wakati wa mvua inamlazimu kupita kwenye yale majaruba. Wananchi kwa kutambua umuhimu huo wakaamua kujenga shule yao. Leo ukiwaambia huwezi kuwasajilia na wakati ni suala la kuzungumza kati ya Wizara ya Elimu na TAMISEMI tukaona namna gani tunawasaidia, tunakuwa hatuwatendei haki wananchi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri, atakapokuwa ku-wind up anisaidie kwenye shule zangu hizi mbili hizi; kuna Shule ya Tacho ipo Kata ya Kirogo na Shule ya Kuruya ipo Kata ya Komuge. Hizi ni shule ambazo zimejengwa na wananchi; hivi ninavyozungumza maana yake Shule ya Kuruya hata wanafunzi hawajakwenda mwaka huu, wameambiwa hatuwezi kuwapa wanafunzi kwa sababu haijasajiliwa, lakini wamejenga wananchi kwa kuepuka huo umbali wa kusafiri muda mrefu. Niombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anafanya majumuisho angalau wananchi nao wapate ahueni kutokana na nguvu zao ili mwisho wa siku wasije kuona nguvu zao zimetumika bila ya kuwa na maana yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili, naomba sana, Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anafanya majumuisho angalau apitie yale madai mbalimbali ya Walimu. Walimu wamekuwa na manung’uniko mengi sana na naamini kabisa hili lipo ndani ya uwezo wa Waziri. Manung’uniko haya anaweza akayatatua kwa muda mfupi sana. Wananchi wengi, Walimu wengi wamekuwa wakilalamikia miundombinu yao; maeneo wanayofundishia siyo rafiki kwao, lakini wengi wamekuwa wakilalamikia madeni ya likizo na madeni mbalimbali ya malimbikizo ambayo yamelimbikizwa huku nyuma. Naamini kupitia Mheshimiwa Waziri kwa sababu tayari nimeambiwa alikuwa ni Mwalimu na alikuwa Mwalimu mzuri ataweza kuwasaidia katika hili.

Mheshimiwa Spika, pia wana madai ya likizo ambazo walikuwa nazo. Ni imani yangu Mheshimiwa Waziri atawasaidia hili. Pili, tunapofanya mabadiliko ya mtaala, tunapowapelekea Walimu niombe sana tutengeneze fedha angalau za kuwatengezea capacity building, tuwajenge ili waendane na ule mtaala mpya tunaowapelekea. Kwa sababu unapobadilisha mtaala Mwalimu bado alikuwa anajua skills za nyuma zilizopita, ukimbadilishia anapata wakati mgumu sana kuendeana na ule mtaala mpya ambao umeupeleka kipindi hicho. Tuweze kuwapa mafunzo ili waendane na mtaala mpya ambao tumewapelekea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho kabisa, ningependa sana kuzungumzia kuhusiana na ujenzi wa Vyuo vya VETA. Mimi Rorya nimepaka na Tarime, population ya haya majimbo mawili au hizi halmashauri ni zaidi ya watu 600,000. Hata kama bado Serikali inajipanga namna gani ya kupeleka Chuo cha VETA kila halmashauri, tuwekeeni chuo kimoja hata ukiweka pale VETA katikati ya Tarime na Rorya angalau tuweze kuwasaidia wanafunzi wote wanaotoka ndani ya halmashauri zote mbili…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Chege.

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)