Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza kabisa nimpongeze Waziri wa Elimu, Profesa Ndalichako kwa hotuba yake, lakini pia na Kamati nzima kwa hotuba ambayo wameitoa.

Mheshimiwa Spika, najikita kwenye mambo matatu ya haraka. Jambo langu la kwanza, ukifuatilia kwenye hotuba ya Rais wetu ukurasa namba 28 anazungumzia suala la elimu akiwa anazungumzia kwenye kujikita kuimarisha miundombinu mashuleni, mimi nitazungumzia suala la madawati. Suala la madawati ni bado changamoto kwenye nchi yetu licha ya kwamba TAMISEMI wanakuja na mpango wa mkakati wa dawati za milioni saba kwa mwaka unaofuata, lakini nina mapendekezo kwenye Serikali na hasa Wizara ya Elimu kwamba tunahitaji kuongeza kiwango cha madawati kwa kuwa na mkakati wa pamoja.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali sisi Makete, Njombe na Iringa ndio wazalishaji wakubwa wa malighafi za mbao. Ubao wa mbao unaouzwa Mwanza shilingi elfu saba elfu nane, Makete unauzwa shilingi elfu mbili ubao ambao unauzwa Dodoma shilingi elfu saba Makete unauzwa shilingi elfu moja. Je, hatuoni kama kuna haja sasa kwa Serikali kujenga kiwanda cha kimakakati na sekta binafsi, ikaingia mkakati binafsi na private sector ikajenga kiwanda katika Mkoa wa Njombe pale Makete au ikageuza VETA ya Makete kuwa sehemu ya uzalishaji wa madawati tu, mwaka mzima, miaka mitatu, miaka mitano wanazalisha madawati tu kwa ajili ya Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, tuna JKT, tuna Magereza lakini tuna vijana wa VETA wengi tu ambao wanamaliza ufundi seremala, tungeweza kuwapa hizo ajira wakatengeneza madawati na tukaanza kusambaza kwenye Taifa hili kwa sababu magari ya jeshi yako mengi ya kuweza kusambaza mashuleni kwetu na changamoto ya madawati ingekuwa imemalizika kwenye Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, sisi Makete tuna eneo, tuna mbao, tuna malighafi za katosha, tunaomba Wizara ya Elimu waone kama hii ni haja ya Serikali kuliko kumwachia Waziri Mkuu, ikifika siku ya enrolment mwezi Januari aanze kusema watumishi wa Serikali msiondoke maofisini hadi madawati yapatikane. Sasa twende na mpango mkakati wa kuwa na kiwanda maalum cha kuzalisha madawati na fanicha za nchi hii.

Mheshimiwa Spika, jambo langu la pili…

T A A R I F A

SPIKA: Haya mwenye taarifa nampa ruhusa, Mheshimiwa Tabasamu.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, kusafirisha dawati kutoka Makete mpaka Sengerema au mpaka Bukoka ni gharama kubwa kuliko kusafirisha mbao.

Mheshimiwa Spika, naomba kama mbao zipo aishauri Serikali sisi tuweze kuletewa mbao tutengeneze dawati kutokea kwake sio kubeba dawati kulipeleka Sengerema na sisi tuna vijana wa kufanya kazi.

SPIKA: Unapokea hiyo taarifa, Mheshimiwa Festo Sanga?

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimwa spika sijaipokea kwa sababu, sisi tuna uwezo wa kulisafirisha dawati kama dawati tunafanya assembling Sengerema ili tuwe na madawati mengi yanayosafirishwa kwa wakati mmoja kwenye magari ammbayo tunaona yanafaa kama magari ya jeshi. Sasa niseme jambo moja magari ya jeshi yapo na kazi maalum ipo, nchi hii haina vita na wanaomba bajeti za mafuta kila mwaka, tungetumia magari ya jeshi kwa ajili ya kwenda kusafirisha mizigo kama hiyo kuliko kufanya hiki ambacho Mheshimiwa Mbunge anakishauri.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo nataka kushauri ni kwenye sekta ya michezo, Mheshimiwa Ndalichako, mawakala na Wabunge wengi asilimia 90 waliopo humu ndani wanaahadi nyingi mashuleni kwenye suala la kugawa vifaa vya michezo. Tunaomba Wizara ya Elimu, Wizara ya Habari na Wizara ya TAMISEMI waone haja ya kutengeneza agency, wakala wa vifaa vya michezo mashuleni wa Serikali ili waweze kutoa ruzuku au kupunguza kodi, vifaa vya michezo mashuleni viweze kupatikana kwa wingi, kuliko kuendelea kusubiria kila Mbunge hapa aagize vifaa China, aweze kusambaza mashuleni, wakati tuna uwezo wa kutengeneza wakala wa vifaa vya michezo na tukasambaza nchi nzima na vijana wetu wakapata.

Mheshimiwa Spika, ile hoja ya Wizara ya Michezo na Wizara ya Elimu kuona UMITASHUMTA na UMISETA vinakuwa kwenye hii nchi ingekuwa kama tungekuwa na hili jambo. Naomba Wizara iifikirie na hili kwa kweli nimwambie Mheshimiwa Waziri kabisa nitashika shilingi kama watakuwa hawana majibu ya kujibu.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, lilikuwa kwenye taulo za kike. Kwanza I call for the ladies of this country even the girls’ student wa nchi hii. Hili taifa kwa sasa ndio kwa wakati mmoja limeanza kupata viongozi sita wanawake watupu. Naanza wa kwanza mtu wa kwanza ni Raisi wetu mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni mwanamama; mtu wa pili ni Mheshimiwa Ndalichako Professor Waziri wa Elimu ni mwanamama; mtu wa tatu ni Waziri wa Afya, Mheshimiwa Dorothy Ngwajima ni mwanamama; mtu wa nne ni MheshimiwaJenista Mhagama ni mwanamama; mtu wa tano ni Naibu Spika, Mheshimiwa Tulia ni mwanamama na akina mama wengine wote na Mheshimiwa Ummy Mwalimu Waziri wa TAMISEMI ni mwanamama.

Mheshimiwa Spika, watoto wa na nchi hii watawalilia kama suala la taulo za kike hawataweza kuli-solve, wanategemea halmashauri zitenge bajeti kwa ajili ya taulo za kike, ni jambo ambalo sikubaliani nalo. Nawaomba na nawashauri kwamba Tanzania tuingie ubia na viwanda, tuweze kutengeneza taulo za kike zenye ubora ambao watoto wanaweza wakazitumia, kwa sababu watoto wengi wa kike wanakosa masomo…

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge wanawake kweli mmejaa humu mnategemea Festo Sanga ndio awaongelee hili jambo. Mheshimwa Festo nakuunga mkono malizia hoja yako.

MBUNGE FULANI: Taarifa.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, kwa ripoti ya UNESCO inaonyesha kati ya watoto kumi wa kike kwa siku watoto wawili au watatu wanakosa kuingia darasani kwa sababu ya hedhi isiyo salama. Nataka ninukuu wanasema menstruation is not a problem but hygiene is a problem.

MBUGE FULANI: Taarifa.

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge wanaume mpigieni makofi Mheshimiwa Festo Sanga (Kicheko)

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, naomba wasimalize dakika zangu naomba nizungumze.

SPIKA: Ahsante sana, wananyanyuka wenyewe Bunge nitalishindwa dakika za mwisho, wenyewe wanataka kuja moto, hapa Waheshimiwa mnasaidiwa kazi hapa. (Kicheko)

Kwa hiyo Wabunge wanaume kumbe tuna faida na sisi. Ahsante sana umetubeba Mheshimiwa Festo Sanga.