Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Jumanne Kibera Kishimba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Elimu ya juu, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Waziri wa TAMISEMI kwa zoezi waliloanza sasa hivi la kupeleka wanafunzi kwenye vyuo vya VETA kwa muda wa miezi sita ninampongeza sana. Ninaona suala langu kidogo umelianza lakini lipo eneo lile lile, juzi hapa kulikuwa na mjadala kati ya Mheshimiwa Nyongo na Mheshimiwa Waziri, kuhusu suala la watu stress sijui presha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Waziri miongoni mwa asilimia 50 ya presha ambayo wazee na watu wanayo sasa hivi ni suala la elimu, na suala hili la elimu sio kwenye elimu yenyewe kama ulivyosema. Leo bahati nzuri ulivyosema nimekuja na sample hapa nina sample ya daftari ambazo zinasomea shule za private, shule ya private inasomea daftari la shilingi 200 ambapo kwa mwanafunzi kwa madaftari 11 itakuwa shilingi 2,200 lakini shule ya Serikali inasomea counter book. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, counter book 11 ni sawa sawa na shilingi 55,000 kwa kijijini ambao ni sawa sawa na gunia zima la mpunga au mahindi. Sasa inawezekanaje matajiri wakasomea daftari la shilingi 200 maskini wakasomea daftari la shilingi 5,500? Na mnasema kwamba watu wana stress ni kweli watu hawana raha na shule, hawana raha wananchi na shule nina-sample ya uniform hapa. (Kicheko/Makofi)

(Hapa Mhe. Jumanne K. Kishimba alionesha mfano wa uniform)

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Spika, uniform za private ni rangi hizi (blue bahari) uniform za shule za Serikali ni rangi nyeupe ni vipi mzazi ataweza kufua kila siku, haiwezekani Mheshimiwa Waziri wa Elimu na TAMISEMI wote ni Wabunge wa kuchaguliwa ni kweli ni sahihi? Kwanini private wasomee za rangi wanafunzi wa shule za Serikali wasomee nyeupe. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo kutwa nzima wazazi wanaendelea kushinda wananunua sabuni na kufua, tunaongeza umaskini badala ya kuongeza elimu. Ni kweli Mheshimiwa Waziri ni lazima kabisa alifikirie upya wananchi wamechoka hawataki kabisa shule, kwasababu sasa hivi kijijini ukifika unakuta mahali unauliza ng’ombe za hapa mlizipeleka wapi? wanasema ng’ombe amemaliza ndugu yako shuleni, hakuzimaliza kwa ajili ya kulipia shule alimaliza kwa ajili ya kulipia vifaa vya shule ambavyo havihusiani na elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, matokeo yake mtu anaona bora kuzaa watoto wajinga huwezi kufilisika kuzaa kuliko kuzaa watoto wenye akili. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunamuomba sana Mheshimiwa Waziri na Waziri wa TAMISEMI walifikirie sana. Nakuona kila siku unalalamika kwamba timu zetu za Taifa watu hawana nguvu lakini watoto wanatoka asubuhi wamebeba huo mzigo uliousema sasa hivi wa hizi counter book 11 wana miaka minane mpaka saa tisa jioni wamekataliwa kubeba chakula kwamba kinaitwa kiporo. Kilibatizwa kitaitwa kiporo wanakwenda bila kula, lakini je wakirudi kutoka shuleni kuna mzazi atapika chakua fresh kwa yule mtoto, si atampa kiporo, sasa ulimkataliaje kubeba kiporo asubuhi kwenda nacho shule. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, matokeo yake sasa hivi unaweza ukaongea lugha nyingine ambayo sio nzuri, lakini watoto hawana afya, hawali chakula. Sisi Waislamu tumefunga lakini tunakula daku saa kumi lakini saa saba ukikutana na Muislamu mkali kama pilipili na ni saa saba mchana. Vipi huyu mtoto wa shule ambaye alitoka saa 12 hajala kitu chochote kule kwetu vijijini hakuna chai wewe mwenyewe unatoka huko. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, hakuna chai anakwenda mpaka kule anarudi saa tisa, saa tisa kama walikuja wageni walipewa kile chakula wakakila anaambiwa subiri usiku atakuwa na afya huyo mtoto? Na hizo mimba mnazosema za shuleni zitakosekana kama mtu ameshinda bila kula ataacha kutongozwa kweli? Ni kweli twendeni kwenye mambo ambayo yapo straight kabisa. Wenzetu Wizara ya Elimu lazima wafikirie haiwezekani leo hii kwenye shule za University wame-introduce tena wanataka simu ya WhatsApp wanataka na laptop.

Mheshimiwa Spika, ukiongea laptop kwa mtu wa kijijini au mama ntilie na simu ya WhatsApp ni shilingi Milioni 1,000,000 tayari kuna miji haijawahi kuishika laki 500,000 kwa miaka 30 anaweza akafanyaje huyo mtu? Lakini je kweli toka mme -introduce hizi laptop na hizi elimu imepanda? Na je, watu wamekuwa efficient? Kwa kuwa leo mmeweka laptop mbona ndio mdololo umeongezeka zaidi. Haiwezekani lazima wenzetu wafikirie upya, wanawabebesha mizigo mizito mno wazazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tunalazimishwa vitatu unaambiwa kiatu cheusi kweli inawapa wazazi wakati mgumu mno kila unapofika kijijini ukiwaita watu kwenye mkutano kuwaambia habari ya shule baada ya dakika 10 unabaki una watu sita tu. Maana yake wanaona umewaletea lile zimwi ambalo linakula haliishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naungana sana na Mheshimiwa Mpima maneno aliongea mengi kule kuhusu suala zima la elimu ni kweli kabisa kunahitaji mabadiliko makubwa. Lakini kabla ya mabadiliko Mheshimiwa Waziri atupe waraka unaoonesha kwamba wanafunzi wanatakiwa wasomee nini.

Mheshimiwa Spika, wa tajiri aje la laptop wa maskini atengenezewe hata internet cafe pale shuleni ili walipe shilingi 500 waangalie hizo laptop mnazotaka wa download watoke lakini sio kuwabebesha laptop.

Mheshimiwa Spika, leo hii wote humu ndani ni wazazi kila asubuhi unagongewa hodi na mtoto na ndio wanamwambia mgongee wewe hawezi kukasirika, ukiamka asubuhi unawakuta wanne wanataka hela ya kwendea shule wakanunue chakula kweli itawezekana na kila siku utalala na chenji? Je hatuoni kama watoto tunawafundisha wizi maana yake kila wakirudi ukiwauliza chenji wanasema tulinunua hiki, tulinunua hiki wana ku- blackmail je, huyu mtu baada ya miaka 10 hatakuwa mwizi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, si atakuwa mwizi sasa mnakataaje watoto wasipike chakula wao wenyewe asubuhi waondoke nacho waendenacho shule, na vile vile kama tunawakatalia wakale maandazi na mikate! Je, maandazi na mikate yenyewe sio kiporo, si mkate una-expire baada ya siku 14 sasa haujawa kiporo na una amira. Kwa hiyo, tunamuomba Waziri wa Elimu wafikirie kama tunawatumikia wananchi wa Tanzania ambao ni maskini, hapa hatuna mpango wa kumjadili tajiri, tajiri atapeleka private atapeleka kila mahali private lakini sisi tunayemjadili ni mtu maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni suala hili ya University ni kweli ukiongea wakati mwingine unaweza kuwa kama unaongea kichwa kama hakipo. Lakini makampuni yote duniani sasa hivi yanafanya biashara yanakwenda yanatafuta wateja yanatafuta hiki, lakini sijaona University wakiwatembelea watu waajiri haijatokea kwa wale watu wa University ni kwasababu wao wanasukumiwa wateja kwa hofu ya dunia kwamba usiposoma shauri yako. Kwa nini na wao wasiwe wanaenda wanatatufa kazi kwenye makampuni ndiyo wanatangaza kwamba bwana sasa hivi tumepata kazi NBC mshahara shilingi 800,000, tumepata NSSF na Bakhresa, kwa hiyo, tayari tunazo nafasi za kazi 4,000, kama unataka kusajili lete shilingi 10,000,000 baada ya kupata degree na kazi hii hapa.

Mheshimiwa Spika, nalisema kwa mara ya kwanza duniani linaonekana kama ni neno la kipuuzi, lakini inaweza ikasaidia sana kwa sababu inawezekana hata ile elimu wanayotoa wao, wale watu wa ajira hawaihitaji. Kama watakuwa wameongea na mwajiri atakuja sasa kuuliza nataka niwaone vijana wangu kama wameelewa. Inawezekana muda wa kusoma badala ya miaka mitatu ya degree ya biashara ikatosha miezi minane huyu benki akasema mimi wananitosha nipe nikaanze nao. Kuliko sasa hivi mimi nikishasema ni Profesa nina degree kazi yangu inakuwa ni kuchukua milioni 10 za watu na kuwa-dump, haiwezekani ni lazima na vyuo navyo viwe committed pia, vikatafute na vyenyewe ajira ndiyo visajili. Vyuo vikaongee na waajiri ili hata hiyo mitaala vitaibadilisha sasa kulingana na soko lenyewe watakalokutana nalo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala hili la elimu kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameliongea vizuri tuanze kulijadili kwa mapana. Mheshimiwa Mpina na Mheshimiwa Sima wameliongea lakini kwa nini elimu tunaiongea Kizungu peke yake, kuna ubaya gani watu wakafundishwa kuchunga ng’ombe za kienyeji shuleni ni kosa? Mwalimu mle ndani akawemo Mmasai, Msukuma au Mtaturu akawa anawaambia ili ufuge ng’ombe wa kienyeji unatakiwa uwatoe asubuhi kwa mwelekeo huu, uwapeleke maji kwa mwelekeo huu, je, itakuwa ni kosa? Ni lazima mtu afundishwe Kizungu? (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, maana karibu wanafunzi wote wanarudi kijiji sasa hatuna mwalimu, kama alivyosema Mheshimiwa Mpina elimu ya biashara inafundishwa na Profesa wa biashara lakini hajawahi kufanya biashara. Kwa nini hatuna kitabu cha Bakhresa au Mohamed Enterprise ili tukitumia kwenye masomo tukafanye biashara? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kama tumesema elimu iwe wazi tusiifichefiche kama uchawi tuendee nayo tu moja kwa moja. Madaktari wanasomea hospitali ndiyo maana hatuna mgogoro na daktari lakini huku kwingine unasomea manunuzi, mnaita procurement kweli manunuzi ni miaka mitatu, unajifunza kununua nini miaka mitatu. Haiwezekani manunuzi miaka mitatu kweli inawezekana? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, wale wazazi kule mtoto hawamuoni, unamrudisha kule ni miaka 25 ukimuuliza umesomea nini, anasema nimesomea manunuzi. Sasa haya maduka yote nani atakuajiri maana watu wote wananunua bidhaa zao wao wenyewe. Haiwezekani! Tuongee moja kwa moja ili wananchi waanze kuona kweli tunaongea kitu ambacho wanakielewa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, baada ya mchango huo kwa kumalizia tu, nimuombea Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI watupe regulation ya mahitaji ya shule ili na sisi iwe rahisi kuwajibu kule majimboni kwetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hivyo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)