Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa. Kwanza kabisa nianze kwa kusema kwa kuwa muda ni mfupi namwomba baba yangu Mheshimiwa Waziri Simbachawene pamoja na Naibu Waziri, wapate nafasi ya kutembelea Jimbo la Momba ili kwa haya ambayo nitayaainisha kutokana na muda mfupi, sitaweza kupata nafasi ya kuelezea kwa kina, watakuja kujionea kwa uhalisia wenyewe nitakachokiongea hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto ya kwanza ambayo nataka kueleza hapa ambayo inawapata Jeshi la Polisi na wanashindwa kutekeleza majukumu yao vizuri kwa wananchi wa Jimbo la Momba, jambo la kwanza ni usafiri. Jimbo la Momba ni Jimbo ambalo ni pana sana, lina square meter za mraba 5,856; vijiji 72 na vitongoji 302. Unaweza kuona ni kwa kiasi gani Askari hawa wanawezaje kufanya kazi; kutoka kijiji kimoja kwenda kingine wakati mwingine ni zaidi ya kilomita 100. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, uhalifu unapotokea mfano labda Kijiji cha Itumba, Kata ya Nzoka mpaka Askari huyu afike eneo la tukio kwenda kuwasaidia wananchi hawa, nasi tuko kwenye Jimbo la mpakani, unakuta wahalifu hawa wameshakimbia, wameondoka, wametokomea Zambia. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali na Wizara hii itutazame, tupatiwe gari ili Askari hawa waweze kufanya kazi yao vizuri. Wakati mwingine hata lambalamba tu wanatusumbua sana. Hatuwezi hata ku-deal na lambalamba.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Taarifa Mheshimiwa.

SPIKA: Endelea wa taarifa. Mheshimiwa Condester, kuna taarifa unapewa. Upande gani?

T A A R I F A

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba hali iliyoko kule Momba ni sawa sawa na Nyang’hwale, tuna magari mawili Landcruiser lakini hayana matairi. (Kicheko)

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hiyo, lakini sisi hatuna kabisa hiyo gari.

SPIKA: Pokea taarifa hiyo Mheshimiwa.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, hatuna kabisa hilo gari, hata pikipiki hakuna; hata baiskeli hakuna.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, Jimbo la Momba, yaani Halmashauri ya Wilaya ya Momba ndiyo Jimbo ambalo linabeba Makao Makuu ya Wilaya ya Momba, Majimbo mawili ya uchaguzi…

SPIKA: Kwa hiyo, Mheshimiwa Amar Hussein afadhali wewe una magari hayana matairi, mwenzako hata baiskeli hana. Sijui yupi zaidi sasa hapo. Endelea Mheshimiwa. (Kicheko)

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, jambo la pili, ni kuhusiana na kwamba Jimbo la Momba yaani Halmashauri ya Momba ndio jimbo ambalo Makao yake Makuu inabeba Wilaya ya Momba, lakini hatuna kituo cha polisi ambacho kinafanana na hadhi ya wilaya. Tuna outpost mbili tu ambayo ni kituo kidogo cha Kamsamba ambacho kina askari nane, kituo kidogo ambacho kipo Chitete ambako ndio makao makuu, kina askari wanne, yaani hata ukipata ya Uchaguzi jamani askari huyu hana baiskeli, hana pikipiki anakwenda kumkamata nani.

Mimi kuna wakati nimefanya kampeni na lambalamba, maana yake nimekuta lambalamba anafanya mkutano wake na hawezi kuja kunisikiliza, wananchi wanafanya pale, kwa hiyo ikabidi tuwaombe kwa sababu hatuwezi kuwapigia Jeshi la Polisi watakuja na nini, watembee kilomita 50.

SPIKA: Mheshimiwa Condester, lambalamba ndio nini?

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, lambalamba ni mkusanyiko. Ulinde dakika zangu Mheshimiwa Spika tafadhali, nitakapotoa ufafanuzi wa lambalamba.

Mheshimiwa Spika, lambalamba ni hawa wanajiita, sijui tusemeje! Sijui waganga wa kienyeji, kwa hiyo wakifika kwenye Kijiji wanahamasisha kwamba tumtafute mchawi na kitu kama hicho. Sasa vile vinaleta mgongano kwenye jamii, kwa hiyo utakuta wakati mwingine wananchi wanataka hata wakaague shule. Nimefika mahali nimewaambia Serikali haitambui uchawi, wananchi wanasema hapana si tunataka Mbunge ambaye anayetutetea, tunaumwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaomba sana, naamini kungekuwa na gari na kungekuwa na Kituo cha Polisi kizuri, kina Afisa mwenye nyota tatu, akapewa askari wa kutosha wangeweza kufanya patrol na kuzunguka, wananchi katika hali ya kawaida tunaogopa sana askari. Kwa hiyo kuona askari wanapitapita, wanalinda wanaona kwamba kuna usalama wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine hatuna askari wa kike, nafikiri kwa sababu hatuna kituo ambacho kina hadhi ya wilaya ili Afisa mwenye nyota tatu akikaa pale kuna mwongozo wa Jeshi la Polisi ambao wanabidi awe na askari wa idadi fulani. Sasa tunajiuliuza sisi wananchi wa Jimbo la Momba sisi wote ni wanaume? Hapana, sasa tunakaguliwa na nani kama askari wote hawa ni wanaume? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, hakuna nyumba za maaskari na wakati mwingine hata Kituo cha Polisi chenyewe huwezi ku-identify kama ni Kituo cha Polisi. Askari hawa wanalala wapi, wanajichanganya huko, wanapanga huko mitaani. Sasa kama ilivyo kuna imani za kishirikina, wakati mwingine wanaweza kuamini hata askari mwenyewe ni mchawi. Kwa hiyo akachomewa nyumba, kwa sababu kule watu wanakatana mapanga kwa hizi imani za kishirikina.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo namwomba baba yangu Mheshimiwa Simbachawene afike kule tu, kwa sababu muda hautoshi nisije nikasitishwa hapa, ili akajionee, tukatembee nimfikishe kule Katumba, nimpeleke kule Chole, Siliwiti na kule Kichangani Kamsamba. Akishaenda kuona tu, baada ya mwezi mmoja ataniletea askari hata 40 na atanipa gari.

Mheshimiwa Spika, ahsante san ana naunga mkono hoja. (Makofi)