Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nfasi hii nami niweze kuchangia Wizara hii ya Mambo ya Ndani ambayo ni muhimu sana.

SPIKA: Atafuatiwa na Mheshimiwa Condester.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nitachangia mambo machache kwa sababu ya dakika tano. Nisipotambua mchango wa Askari wetu nitakuwa naidanganya nafsi yangu. Tunatambua mchango wa Askari wetu hasa kwa kujitolea kwenye nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kuna changamoto kadhaa ambazo zinawakumba Askari wanaojitolea hasa wa chini kabisa. Nitatolea mfano tu kwenye uchaguzi uliopita. Mheshimiwa Naibu Waziri nimezungumza nawe sana na jambo hili liko Wizarani. Siku ya uchaguzi siyo Jimboni kwangu, labda wanaweza wakafikiri nazungumza kwa sababu ni Jimboni kwangu. Askari amevunjika mguu siku ya uchaguzi akiwa kazini, mpaka leo nazungumza hakuna mchango wa Wizara hata kidogo. Askari wenzake wale wa chini ndio wanaojichangisha na mimi Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo kwa sababu, Wizara haijachangia, isipokuwa inaleta picha mbaya kwa Askari wengine siku nyingine kujitolea. Inaleta picha mbaya sana na watarudi nyuma, kwa sababu wataamini kwamba nikiumia, itakuwa ni mzigo wangu mimi na familia yangu. Jambo hili haliko sawa, tuwatie moyo Askari wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wakuu wa Vituo kwa maana ya Ma-OCD, wale ni viongozi. (Makofi)

SPIKA: Unaweza ukamtaja jina la huyo Askari ili…

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, Naibu Waziri nafikiri anajua, kwa sababu anajua jina na ameshafanya naye mawasiliano, anajua vizuri.

SPIKA: Lakini Hansard haijui.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nikikumbuka nitalitaja, lakini hapa sina kumbukumbu nzuri.

SPIKA: Haya ahsante.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, ahsante

SPIKA: Wakati mwingine ni vizuri kutaja maana tutakapofuatilia baadaye…sana.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, ahsante

SPIKA: Ahsante, haya.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba Askari hao wachache ndio wanaopata mateso makubwa; lakini Ma-OCD, wale ni maaskari ambao wana vyeo hivyo. Ukiangalia ofisi zao, wale sio wafungwa, wanastahili kupewa hizo nafasi na angalau mazingira yao yafanane. Kwa hiyo, tunapozungumzia kuboresha makazi ya askari, hata ofisi zao zifanane, angalau nao wakiwa mle ndani wajue wako ofisini, angalau watimize majukumu yao. Siyo wanapita huku kuna kunguni, kuna panya na nini. Yaani ifikie mahali kwa kweli tuwatie moyo askari wetu. Pamoja na kwamba kuna shida ya maslahi na nini, basi angalau mazingira yafanane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya dakika tano, nitakwenda kuzungumzia pia habari ya vitambulisho vya Taifa. Alipokuwa anazungumza Mbunge wa Kigoma, yawezekana alisomeka kwamba ni Kigoma. Mikoa yote ya pembezoni tuna changamoto hiyo. Mimi natokea Wilaya ya Nkansi, sisi tunapanda boti tu kwenda Kongo pale. Ikifika wakati wa uchaguzi, wale wote wanaoonekana wana mtazamo tofauti na CCM, wanaambiwa wewe sio raia. Hili jambo siyo zuri, linaleta unyanyasaji. Siyo jambo jema kabisa. Pamoja na kwamba bado tuna changamoto ya utekelezaji wa vitambulisho, basi mikoa ile ya pembezoni ipewe kipaumbele ili kumaliza hizi changamoto ambazo zinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna watu ambao walipewa namba toka mwaka 2020, sasa kama namba wameshapata, vile vitambulisho vinachukua muda gani? Hili jambo ni lazima tulitazame. Kwanza tunawakwamisha kwenye mambo mengi. Leo unapokwenda kwenye sijui usajili wa line na vitu gani, kote unahitaji kitambulisho cha Taifa. Kwa hiyo, tunawakwamisha sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo napenda kuishauri Serikali yangu ya Tanzania, sisi wote ni Watanzania. Leo hawa watu ambao wanaitwa wahamiaji au wageni ambao wamekuja kufanya shughuli mbalimbali Tanzania, tunatambua kwamba ipo sheria ya wageni wanapotaka kufanya kazi. Kipindi cha nyuma ilikuwa ni shilingi milioni sita kwa miaka miwili. Leo watu wengi hawana hivyo vibali vya kufanya kazi, wakiwemo watu wachache tu ambao wanafanya kazi saluni, hizi shughuli ndogo ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka kuishauri Serikali kwenye jambo hili, imekuwa ni kama upenyo wa baadhi ya watu wa uhamiaji, wanakwenda kufika kule wanawaambia nipe shilingi 500,000/= ili nikuachie, kwa sababu sasa hawana vibali. Kwa hiyo, naishauri Serikali, ni vizuri mkawatambua wale wanaofanya kazi nchini ambao ni wageni, wako wangapi? Je, wana vibali vya kufanya kazi hizo? Yawezekana hata idadi yao hatuijui. Kwa hiyo, Serikali inakosa mapato, ila watumishi wachache wanakwenda kwa kukosa uaminifu, anaomba shilingi milioni moja, wanamalizana; naomba shilingi laki mbili, wanamalizana.

Mheshimiwa Spika, sasa hawa watu, kama kweli kuna vibali, tuangalie aidha kuna shida kwenye sheria yenyewe, tuifanyie maboresho. Ila kabla ya kufanya maboresho, tuwatambue wako wangapi? Je, kweli hizo kazi wanazofanya wanafanya kwa mujibu wa sheria? Yawezekana tukiwatambua itasaidia sasa hata kile kiasi ambacho tunakitaka kama ni kikubwa kipunguzwe. Lengo ni kwamba kifike Serikalini, kisipotee huko mtaani kama kinavyopotea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)

SPIKA: Ahsante. Kwa hiyo, pia kwako kuna shida ya uhamiaji?

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, eeh, wapo wengi tu.