Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon Haji Makame Mlenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chwaka

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. HAJI MAKAME MLENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nikiwa mmoja wa mchangiaji katika Wizara hii ya Mambo ya Ndani. Kwanza, nianze na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika hapa tukiwa katika hali ya afya na uzima. Namwomba Mwenyezi Mungu kwa wale ambao wana afya mgogoro, basi awaponyeshe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende katika mchango wangu katika Wizara hii. Nianze tu na Polisi. Niseme tu kwamba, Polisi ndio ambao wanatufanya tuendelee na vikao vyetu tukiwa huru na salama kutokana na kazi zao. Nawashukuru kwa hilo kwa sababu tumeondoka mitaani kwetu lakini bado hatujapata migogoro kutokana na kazi zao nzuri, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme kutokana na umuhimu wao wa kazi, japokuwa na wenzangu wamesema sana suala la ajira, lakini naomba, ili waweze kufanya kazi vizuri, basi suala la ajira lisiachwe nyuma, liangaliwe kwa umakini na umahiri mkubwa. Kwa sababu ndilo ambalo litasababisha kuweza kufanya kazi zao vizuri. Sitakaa sana hapa kwa sababu watu wengi wamezungumza.

Mheshimiwa Spika, nije kwenye suala la usafiri. Suala la usafiri ni changamoto kubwa katika Jeshi la Polisi, pia tukizingatia kwamba hawa ndio ambao wanatufanya tuweze kukaa kufanya kazi kwa amani na usalama, lakini wanaposhindwa kupata usafiri wa kutosheleza, maana yake huenda tukaja tukawalaumu siku moja lakini watakuwa hawana tatizo la kulaumiwa.

Mheshimiwa Spika, nitoe mfano, ndani ya Jimbo langu nina vituo viwili vya Polisi; nina Kituo cha Chwaka lakini pia nina Kituo cha Jozani. Vituo hivi viwili vyote vinafanya kazi, lakini vikiwa havina usafiri wa aina yoyote. Sijui wanapangaje kazi zao mpaka waweze kufanya kazi vizuri. Kituo cha Chwaka, eneo lake hili lina mahoteli yasiyopungua 18 kwa wale wa Shirika la Umeme, wanaita mahoteli makubwa ambapo wameweka katika ngazi ya kushughulikia maalum, lakini hawana usafiri. Sasa sijui, kazi hizo zinaweza zikafanywa vipi iwapo wataendelea kukosa usafiri? Ikiwa Serikali wanaelekeza sana nguvu zao na tunapiga kampeni kila siku kuona utalii unaongezeka, lakini hatuwapatii usafiri katika maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, la kushangaza zaidi; na nimsemee ndugu yangu Naibu Waziri, kwa sababu hana nafasi nzuri ya kusema maana yeye ni mtetezi wa Serikali ndani ya Jimbo lake. Kile kituo hakina usafiri na kinapokea kesi nyingi sana. Kwa hiyo, suala la usafiri ni jambo muhimu sana ili waweze kufanya kazi zao vizuri.

Mheshimiwa Spika, niongelee kidogo suala la maslahi. Suala la maslahi nalo lina changamoto. Niiguse suala la maslahi ya wastaafu, kwa sababu wenzangu wamesema, sitaki niende sana hapa ili muda wangu usije ukamalizika, lakini nazungumza zaidi kuhusiana na utaratibu mzuri wa Askari Polisi pale ambapo linatokezea tatizo la kufiwa na mfanyakazi, wanakuwa na utaratibu mzuri sana. Pengine unapotaka kuchukua maiti unaweza kuwajulisha wakakwambia hata, usimguse maiti, tunakuja wenyewe kumchukua na kumpeleka katika sehemu husika.

Mheshimiwa Spika, hiyo ilinitokea mimi mwenyewe, pale marehemu ndugu yangu alipofariki. Wakati nawajulisha na nilikuwa nimeshatafuta usafiri, nikaambiwa kwamba wanakuja kumchukua wenyewe na ikabidi usafiri ule niutumie kwa mambo mengine na nisiutumie kwa kumpeleka marehemu. La kushangaza ni kwamba, anapofariki mtu, basi wanachukulia kwa umuhimu, wanamshughulikia, lakini kwanini wasishughulikie maslahi yao?

Mheshimiwa Spika, naomba sana kwa jeshi la Polisi waone kwamba huyu Askari wanapokuwa naye ni mtamu na anapokufa wana hamu sana ya kwenda kumzika. Pia, wawe na hamu ya kuona mafao yao yanapatikana kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafikiri katika tarehe 19 nilikuwa na swali la msingi la kuhoji kutokana na Askari ambaye amefariki toka mwaka 2003 hadi leo warithi hawajapata mafao; mpaka na wao wafe! Kwa hiyo, siyo jambo zuri. Kama uliweza kwenda kumchukuwa wakati amefariki na ulikuwa unamtumia, basi ni vizuri na kuona maslahi yao yanapatikana kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali yangu hapa, tuone kwamba watu wote siyo sawa, kwa hiyo Askari Polisi wawe wanachukua jukumu la kuwashauri wale wafiwa. Wengine hawana uwezo wa kufika. Sisi tulipata maslahi yetu kwa kupitia wakubwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. HAJI MAKAME MLENGE: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, siyo utaratibu mzuri.

Mheshimiwa Spika, ahsante. Naunga mkono hoja.
(Makofi)