Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Leo nifuate mwongozo wako au ushauri wako kwamba uongee jambo moja linaloeleweka. Leo nataka kuongelea sekta ya ulinzi binafsi. Sekta ya ulinzi binafsi hapa imeanza mwaka 1980 na kampuni mbili na ilianzishwa na Mheshimiwa Rais aliyekuwepo madarakani kwa kumwita IGP kwamba sasa tunarudisha makampuni yote na mali zote za wenyewe hatuwezi kuendelea kuzilinda na mgambo, Jeshi la Polisi. Kwa hiyo yakaanzishwa makampuni mawili Group Four na bahati nzuri sana IGP aliyekuwepo akaomba share kwenye Group Four lakini pia Ultimate Security nayo pia Kamishna wa Polisi Rashid akaomba nae awe kwenye group hilo.

Mheshimiwa Spika, leo tuna makampuni 3,500 yameajiri askari walinzi laki tano, Jeshi la Polisi hawazidi elfu 60. Kwa hiyo sehemu kubwa ya ulinzi nchi hii inafanyika na sekta ya ulinzi binafsi. Hata hivyo, hakuna GN wala sheria wala mwongozo wowote ulioanzisha sekta hii nchi. Sekta hii imeendelea kukua, matokeo yake mambo mabaya sana yanafanywa kwenye sekta hii, lakini pia Serikali inakosa kodi, haina idadi kamili ya makampuni kwa sababu hakuna mwongozo wowote.

Mheshimiwa Spika, duniani, mimi nina sheria tatu hapa za sekta ya ulinzi binafsi, tulikoiga sisi; Private Security Services Act, lakini tuna Sheria ya Common Wealth, hii ni ya Jumuiya ya Madola, Sheria ya Sekta ya Ulinzi Binafsi, lakini kuna sheria nyingine muhimu sana inaitwa Data Protection Act ya sekta ya ulinzi binafsi, lakini pia kuna sheria nyingine Regulatory of Investigatory Power Act. Zote sheria tatu zinadhibiti makampuni ya ulinzi kwa sababu yanalinda raia na mali zao lakini wana silaha.

Mheshimiwa Spika, sekta ya ulinzi binafsi hapa nchini imesaidia kueneza silaha nchi nzima shotgun na udhibiti hakuna kwa sababu makampuni haya yalipoanzishwa mwaka 1980 na Jeshi la Polisi, viongozi wote wa Polisi wana makampuni ya ulinzi. Asilimia 75 makampuni ya ulinzi nchi yanaongozwa au yanadhibitiwa na polisi. Matokeo yake Polisi hawa viongozi waliokuwa na uwezo mwaka 1980, miaka 40 baadaye wamezeeka au wamefariki.

Mheshimiwa Spika, sasa makampuni haya yanaendeshwa na watu ambao hawana uwezo wowote, yamerithiwa kama mali ya mtu binafsi, watoto wamerithi, wake zao wamerithi na ndugu zao wamerithi. Mabunduki yako uvunguni, hivi karibuni naomba nitaje maslahi yangu, nilikuwa Mwenyekiti wa Sekta ya Ulinzi Binafsi, tulianzisha chama ili kuweza kuji-control sisi wenyewe. Nikamsaidia Mheshimiwa IGP Mwema kuanzisha at least kanuni ndogondogo ambazo sio sheria wala haziko kwenye sheria yoyote.

Mheshimiwa Spika, leo hii makamppuni yana hasara huku na huku. Kwanza makampuni yenyewe haya baada ya miaka 40 na kurithiwa na watu ambao hawana taaluma, yanaendeshwa yanapata mambo yafuatayo kama changamoto:-

Mheshimiwa Spika, Askari wanaiba mali za watu ambao wanawalinda, mnakumbuka kesi ya Kasusura aliyetumwa kwenda kuchukua milioni mbili dola akatoweka nazo; Wizi wa mishahara ya benki ya NMB, walitumwa wagawe hela, walinzi wakavua nguo pale Kawe wakachukua hela, wakaacha silaha na kila kitu; Wizi wa CRDB Azikiwe mabilioni; Wizi wa kule Moshi mabilioni pia; na Walinzi wanakufa na hakuna uhakika na hawapati haki zao.

Mheshimiwa Spika, Temeke NMB ilivamiwa, kulikuwa na Polisi na kampuni za ulinzi binafsi, walinzi wote wakafa, huyu Polisi wa cheo cha chini akazikwa na bendera ya Taifa na huyu mlinzi aliyekuwa Sergent wakati anastaafu akazikwa kawaida kabisa, hii sio haki. Vilevile walinzi wote waliopiga risasi majambazi wameshtakiwa kwa mauaji. Pale Tabora majambazi yanataka yambake mtoto, samahani lugha chafu, wanataka kumbaka mtoto wa kike, yule mlinzi amekamata silaha wanamsukuma mwisho akafyatua risasi, baadae amekamatwa kwa mauaji. Naye yupo kazini, hii ni kwa sababu hakuna sheria.

Mheshimiwa Spika, haya naweza kuyasema kwa uchungu sana. Mimi nilipoingia madarakani nilitoka sekta ya ulinzi binafsi, nimeleta mfano wa sheria, Serikali ikasema itaileta. Leo hii hakuna chochote kilichokuja humu Bungeni. Sheria itaanzisha mamlaka inaitwa Public Security Authority kama EWURA, TCRA, TRA na kadhalika, ndivyo ilivyotoka duniani kule, hiyo mamlaka itakuwa chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani sio Jeshi la Polisi, lakini polisi hawa wanashindwa kuleta sheria hiyo kwa sababu sasa wenyewe ni wenyewe, wanajisimamia wenyewe.

Mheshimiwa Spika, limezuka jambo lingine ambalo linasikitisha sana, kutokuwa na mamlaka yoyote tunakosa local content kwenye migodi au kwenye mashirika makubwa ya kidunia, kwa sababu hatuna viwango. Makampuni ya Tanzania hayana viwango, hayana cheti wala hayajapangiwa kiwango gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuchukulie zabuni itangazwe ya kujenga barabara, si lazima mtu wa civil ndio afanye quotation kule na ufundi umeme naye ana-quote kwenye barabara; tunatangaza zabuni ya ulinzi wana-quote makampuni yote, kumbe kwenye sekta hii kuna man guarding, kuna mitambo, lakini kuna upelelezi na vilevile kuna wanaosindikiza mali wanajiita CIT. Sasa inatangazwa zabuni vurugu tupu, ni ya nani hiyo zabuni. Kungekuwa na mamlaka itapanga kwanza kazi hii daraja la ngapi.

Mheshimiwa Spika, tunapotangaza kazi ya ujenzi wa jengo hili tunasema mkandarasi daraja kadhaa, makampuni hayo huko yalikotokea yana madaraja la kwanza mpaka la saba, lakini pia yana taaluma hapa tunaenda fujo tu. Hivi karibuni kumekuwa na usemi wa Auxiliary Police wanasema haya makampuni yote ni Auxiliary Police, sio kweli, Auxiliary Police ni watu wengine na sekta ya ulinzi…..loh!

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti naunga mkono hoja hii nitaandika (Makofi)