Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Fakharia Shomar Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na pia kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia na kuipongeza Wizara; Waziri, Naibu Waziri na watendaji wao wote waliokuwepo Bara na Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia magari ya doria ya Polisi pamoja na Magereza na magari yanayochukua mahabusu. Magari ya doria ya Polisi ndiyo kiini kikuu kwa Polisi kuweza kuwakamata au kufuatilia majambazi na aina zote za tatizo litakalotokea katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati Viongozi Wakuu wanapokwenda ziara, magari ya doria ndiyo yanayoshughulikia, lakini Mheshimiwa Waziri alipokuja kuzungumzia hapa ukurasa wake wa 37, kasema anatoa magari tisa na hayo anawapa Magereza kwa ajili ya utawala. Hiyo kweli sikatai, lakini kwanza tutizame katika utendaji. Kamati yetu ilikwenda ziara, tukapewa gari ya doria, kila mkoa tulikuwa tunabadilishiwa na ndiyo utaratibu. Ilikuwa likifika kwenye kilima, gari inatoa moshi utafikiri chetezo. Haliwezi kwenda, halina nguvu. Sasa ina maana hizi gari ni mbovu na haziwezi kukidhi mahitaji. Unamfukuza jambazi kwa gari kama hiyo utampata? Humpati. Sasa kwa vyovyote mjitahidi baada ya gari kutumia ninyi utawala au viongozi, mtafute gari za doria kwa ajili ya maskari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukichukua Magereza wakati mahabusu wako Magereza, tatizo linakuwepo hapo, hawapelekwi Mahakamani kwa wakati, maana hakuna gari na Magereza yapo mbali na Mahakama. Ina maana tunawapa tatizo wafungwa wale walioko ndani au mahabusu kuweza kufika kwa wakati Mahakamani. Namwomba Mheshimiwa Waziri aangalie, magari ndiyo uti wa mgongo katika kazi zao, maana bila hayo magari hao Polisi hawataweza kufanya kazi zao kwa ufasaha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikija na ajenda ya pili, nataka kuzungumzia kwa upande wa Zanzibar kidogo. Zanzibar kuna kituo kinaitwa Ng’ambo Police Station. Nakumbuka wakati mimi mdogo ndiyo kwanza nazaliwa, bibi yangu nilimsikia anakiita kibiriti ngoma, ambalo ndilo jina la awali, baadaye likabadilishwa, likawa Ng’ambo. Kituo kile kiko katikati ya mji pale Mkoa wa Mjini Wilaya ya Mjini, ambapo kipo katika katika Jimbo la Mheshimiwa Abdulwakil. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la kushangaza, kituo kile hakina uzio na kituo cha mwanzo kikubwa kile; hicho Madema kimefuatia baadaye, lakini kituo kile ndiyo kilikuwa kituo mama na kimezungukwa na barabara. Unaweza kupita ukakuta ndani kuna kuku anaranda, mara ndani kaingia mbuzi anaranda. Sasa Polisi na hivyo vitu vinaendaje? Unaweza ukapita ukaona kinachofanyika ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pale pale pana kituo kingine tu cha Serikali wamejengea uzio wa matofali. Sasa na nyie naomba kile kituo kwa sehemu kilipokuwepo kipate uzio wa matofali ili kiweze kujisitiri, baadaye na kile kituo mtaweza kukikarabati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiendelea, kuna tatizo hili la Magereza. Magereza wanapokea mahabusu, lakini mahabusu wanaopokea wengine na kwa wale wakimbizi ambao wamechukuliwa kama 100 au 50. Sasa baada ya kupelekwa Mahakamani inabidi warejeshwe mahabusu. Wanaporudi mahabusu kwa kweli tunawaonea wale Jeshi la Magereza. Mnawapeleka, wale hawako kwenye bajeti, hawana chakula na wale wako wengi, mnategemea kule Magereza watakula nini? Ina maana sasa wajibane.

Mheshimiwa Spika, Magereza itafute mbinu wewe Polisi umekamata, kazi yako imekwisha; Mahakama kuhukumu, kazi yake imekwisha; lakini wakati mwingine hukumu inatoka inabidi watolewe wale na wakitolewa inatoka faini ili watoke, lakini ile faini haiendi Magereza, inakwenda Serikalini. Sasa yeye ile bajeti yake ya chakula aliyoitumia akiwalisha wale itakuwaje? Mngefanya basi wakati wao wanapita njia za panya nanyi mkawakamata, basi wajilishe, japo ni mahabusu wajilishe wenyewe, lakini uzito huo msiwape Jeshi la Magereza ambao wanapata usumbufu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukija kwenye zimamoto, nawapongeza. Wana club ambayo wanafundisha katika katika school za sekondari jinsi ya kuzima moto ili ukitokea moto waweze kujihami wenyewe, lakini wanakwenda kidogo kidogo. Maana toka wameanza, ndiyo kwanza sekondari 10. Nawaomba wajitahidi wafanye kila mkoa angalau sekondari tatu, nne na siku hizi majanga ya moto kwa mashule yako mengi, halafu tena kama wao watakuwa hawafanyi hii club, siyo vibaya kuwa na club, lakini wafanye haraka ili zisambae kwa Tanzania nzima, vijana wetu wawe na weledi wa kuweza kuhami moto kabla haujawaathiri.

Mheshimiwa Spika, nikija kwa Polisi wastaafu, hawa kila siku wanaongeza ingawa suala hili mama kaligusia jana, lakini kwa nini hawafanyi wakati mtu unamjua tarehe fulani anastaafu. Kwa nini hawamfanyii ili akiondoka pale, aende na cheque yake, unajua umemtumia toka kijana, ujana wake kamalizia pale mpaka anakuwa mtu mzima, leo unamtoa haki yake humpi na nina hakika kwa viongozi wa juu, wakiondoka wanaondoka na cheque zao au wanaondoka pesa imeshaingia kwenye akaunti, lakini hawa wanyonge ndio wanaowahangaisha.

Mheshimiwa Spika, sasa hawa wanyonge wajaribu kuwapa, ikiwa wanatoa cheki au cash, tena wanawapingia tunajua tarehe fulani mwaka fulani, fulani atastaafu, anajijua mimi naondoka pale naagwa na changu tayari, la sivyo tutakuta wanapata malazi ya pressure, wanakufa mapema, ameshazoea kutumia, ana familia wanawaangaliaje, ina maana kila siku wawafuate, bora wampe chake. Nalishukuru Bunge, unaondoka, unaondoka na chako, tena mwenyewe utajijua. Kwa hilo Bunge halina mjadala. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Fakharia.

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Spika, Ahsante naunga mkono hoja.