Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Mambo ya Ndani. Kwanza nianze kumpongeza sana Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri na IGP Sirro pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanazozifanya za kutulinda sisi pamoja na mali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina mambo kama mawili na la kwanza vitambulisho hivi vya NIDA ni tatizo kubwa sana katika maeneo mbalimbali hususan katika Jimbo langu la Makambako. Watu wameandikisha, wengine wamepata namba lakini vitambulisho vyenyewe hawajapata, kila wanapofuatilia havipatikani. Wengine wanakaa mbali vijijini kwenda wilayani kule nenda rudi nenda rudi, jambo hili limekuwa lina usumbufu mkubwa, nina imani na majimbo mengine katika nchi hii tatizo hili ni kubwa. Kwa hiyo, tunaomba sana katika bajeti hii Waziri aone namna ya kuhakikisha anaondoa usumbufu kwa wananchi juu ya kupata haki zao za vitambulisho vya NIDA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, pamoja na kwamba nimewapongeza kwa kazi nzuri ya ulinzi wanayofanya katika nchi hii, wanafanya kazi nzuri sana lakini hivi sasa vibaka wameanza kunyemelea kurudi taratibu na majambazi wameanza kuteka magari. Nikuombe Waziri na timu yako na IGP Sirro, kama mlivyosimamia jambo hili awali msimamie na sasa ili likome kabisa wananchi waishi kwa amani katika nchi yao na mali zao kwa sababu sasa vibaka wameanza kujitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine liko kwenye Jimbo langu na ni tatizo la muda mrefu. Kituo cha Polisi cha Mji wa Makambako kuna wananchi takriban sita wako ndani ya eneo la polisi; hawaruhusiwi kufanya kitu chochote hata choo kikibomoka hawaruhusiwi kutengeneza. Siku ukipita pale tu hata wewe mwenyewe utawaonea huruma; choo zimebomoka na nyumba zao ziko katika hali mbaya. Niombe fidia ambayo walikuwa wanaidai walipwe ili waweze kuondoka. Nimwombe sana Waziri na IGP Sirro waone namna ya kulipa wananchi hawa sita na tathmini ilishafanywa ili waweze kwenda kutafuta mahala pengine na wao waishi kwa amani katika nchi yao. Chonde chonde sana naomba jambo hili walichukulie kwa umuhimu wake.

Mheshimiwa Spika, Makambako ni center na ni lango kuu la kwenda Songea au Mbeya na sehemu nyingine hata baadhi ya matukio ni watu waliotoka sehemu mbalimbali kuja pale. Kuhusiana na vitendea kazi naomba atenge gari maalum kuja katika kituo cha Makambako ili askari wangu pale waweze kufanya kazi kwa uhakika kulinda wananchi na mali zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine tunashukuru kwa kujengewa nyumba za polisi katika eneo letu la Kituo cha Makambako. Haijawahi kutokea kuwa na nyumba pale sasa hivi wametujengea nyumba kwa kweli lazima tushukuru wamefanya vizuri na wananchi ndiyo maana waliunga mkono kujenga nyumba zile za polisi ili walinde mali zao vizuri na mimi Mbunge wao niliunga mkono kuhakikisha nyumba zile zinajengwa.

Mheshimiwa Spika, ombi langu tuendelee kuwajengea nyumba zingine katika bajeti hii ambayo wameitenga ili askari wetu pale waweze kupata nyumba nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo sikuwa na mambo mengi ya kuchangia katika Wizara hii kwa sababu inafanya vizuri ni changamoto ndogo ndogo hizi tulizozizungumzia. La mwisho Mungu aniongoze kwa busara kuna jambo umelisema sasa na mimi kulisema tena siyo vizuri.

WABUNGE FULANI: Sema.

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi/Kicheko)