Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kupata nafasi ya kuchangia katika bajeti ya Wizara hii ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Spika, bajeti ya mwaka 2020/2021 Mheshimiwa Waziri alieleza mafanikio makubwa sana juu ya bajeti hasa kwenye kipengele cha NIDA kwa asilimia 86. Kumekuwa na shida kubwa sana ya Vitambulisho vya Taifa hususan watu wa vijijini. NIDA walisema wana mpango wa kusajili watu takriban 25,000 leo hii Waziri anasema wamesogea wamefika watu 23,000 lakini waliopata Vitambulisho vya Taifa hawazidi milioni saba.

Mheshimiwa Spika, kuna watu walipata namba wakati ule akizungumzia bajeti hii walikuwa watu milioni 17 leo wameongeza wamekuwa 18. Deadline ya kupata Vitambulisho vya Taifa kwa mwaka huu ni tarehe 8 Juni, 2021 lakini kuna watu wanakaa zaidi ya mwaka mmoja hawajapata hivyo vitambulisho ijapokuwa wana hizo namba ambazo wamepewa hivyo kuwapa ugumu kuendelea kufanya shughuli za kitaifa kwa sababu wanavitegemea vitambulisho hivyo.

Waziri alisema kuna mashine mpya mbili wamenunua ambazo zina uwezo wa kutoa vitambulisho takriban 144,000. Naomba kupata maelekezo yake kama kweli mashine hizo zipo na vitambulisho vinapatikana. Leo Waziri ameeleza vizuri kwamba amejitahidi kutafuta taasisi zaidi ya 39 za umma na binafsi ili ziweze kujiunga na vitambulisho hivi vya taifa kama chanzo cha mapato ili watu waweze kutumia vitambulisho hivyo. Umuhimu wa vitambulisho ni mkubwa tunaomba Waziri atuambie mwisho wa changamoto hii ya upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa utakuwa lini.

Mheshimiwa Spika, nikija eneo la polisi, bajeti iliyopita walikuwa wajengewe nyumba 431 lakini leo hii tuna polisi wanakaa mitaani. Kamati imeshauri vizuri unapokuwa na polisi mtaani na yeye kazi yake anayoifanya wakati mwingine ni ya kugombana na hao raia kwa maana inategemea ni maeneo gani wanafanyakazi ni hatari sana kwa askari huyu. Polisi hawa wanakaa uraiani maana nyumba ni chache. Tunaomba bajeti hii waweze kuongezewa ili polisi wajengewe nyumba.

Mheshimiwa Spika, Rais amezungumzia suala la upandishwaji madaraja, naomba sana wakati huu madaraja hasa kwa askari wadogo utiliwe maanani. Hata hizo nyumba tulizozisema tuachane na viongozi wenye vyeo vikubwa kwani wanaopata shida ni maaskari wadogo ambao na wao wanahitaji kukaa kwenye makazi bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mafunzo ya kipolisi, nilishawahi kufika Chuo cha cha Polisi Kidatu, mazingira wanayosomea siyo rafiki kabisa. Majengo yale yalijengwa siku nyingi na ni chakavu, kwa hiyo, watu wale wanasoma katika mazingira magumu sana. Hivyo basi naomba Wizara hii safari hii isimamie na kuwatizama.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie makampuni binafsi ya ulinzi ambayo naamini yanasimamiwa na Wizara hii. Nataka kujua ni namna gani Wizara inasimamia hasa silaha za moto kwa makampuni haya binafsi. Wanawasimamiaje kuhakikisha wanatunza na kuwa waaminifu katika matumizi ya silaha hizi za moto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo hivyo tu, makampuni mengi binafsi yanaajiri wafanyakazi toka nje ya nchi. Ukienda kwenye hoteli nyingi za Five Stars, Three Stars utakuta walinzi wale wengi wanatokea Kenya wakilinda kwenye makampuni haya. Mimi nafikiri ni wakati sasa kuhakikisha SUMA JKT wanapewa kazi ya kulinda mahoteli hayo badala ya kutumia makampuni binafsi kwa sababu vijana wetu wengi hawana ajira, tunafikiri wao wanaweza wakatusaidia kupunguza ajira kwa kutumia makampuni ya nyumbani na si vinginevyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie masuala ya Zimamoto. Mara nyingi huwa nasema hapa Zimamoto ni jeshi la mwisho. Nikisema la mwisho nina maana hii, ni kweli kabisa ukiangalia uniform, dawa na nyumba za Zimamoto ni jeshi ambalo limekuwa likipata bajeti ndogo kulinganisha na majeshi haya mengine. Kama Kamati ilivyosema tunahitaji kuwekeza kwenye Jeshi hili. Si hivyo tu wamezungumzia Jengo la Mchicha shilingi bilioni 2 ziliwekezwa pale, ile ni pesa iliyolala mahali pale, najua hapa tumekwishajenga lakini bado kuna haja ya kuongeza fedha na kuhakikisha lile jengo linaisha hata tukalipa matumizi mengine.

Mheshimiwa Spika, suala la magari, bajeti iliyopita walisema watapata magari matano kutoka Nyumbu. Naomba Mheshimiwa Waziri aniambie kama magari hayo yamepatikana kwa kutoa taarifa mahali hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, magari ya Zimamoto, mikoani hakuna magari na kama yapo wafanyakazi ni wachache. Tunaomba ikama ya wafanyakazi katika idara hii iongezwe.

Mheshimiwa Spika, nikienda Magereza, leo hii watu walioko magerezani wafungwa ni nusu na mahabusu ni nusu. Tulisema wakati uliopita ni bora kukawa kuna kesi zile ambazo zinapunguza idadi ya mahabusu ili tuweze kupata nafasi ya kuwaweka wafungwa kwenye nafasi ya kutosha. Kama wafungwa ni zaidi ya milioni iliyotajwa, nusu 16 ni wafungwa waliohukumiwa na nusu 16 ni mahabusu. Kwa hiyo, mahabusu ni wengi tunaomba kesi zifanywe haraka haraka ili kusudi hawa mahabusu waweze kutoka na magereza yaweze kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kimsingi magereza mengi ni magereza yaliyojengwa enzi za ukoloni. Mimi sipendi watu wetu wafungwe lakini wafungwe katika staha, wakae kwenye magereza ambayo yana vyoo vya kutosha na wanawake waliokuwa kule magereza wapate stara ya kutosha. Tukiwa na magereza yenye maeneo madogo kama ni mahabusu kisaikolojia unakuwa umeshamfunga.

Mheshimiwa Spika, tumesema magereza itengeneze chakula. Gereza la Songwe ni kubwa na lina ekari nyingi lakini hawana vifaa vya kuwawezesha kulika. Ili ulime na uzalishe chakula lazima uwe na matrekta, wataalamu na fedha ya kununulia mbegu. Mmesema mmetenga mbegu lakini ni lini zitapatikana kwa sababu kila mwaka mnazungumzia kutenga mbegu. Songwe wana eneo kubwa lakini hawana trekta, vifaa vya kutosha na wataalamu, naomba Wizara itazame suala hilo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Sophia.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)