Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini

Hon. Prof. Shukrani Elisha Manya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kujibu baadhi ya hoja ambazo zimechangiwa na Waheshimiwa Wabunge. Pia, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliotoa mchango wao.

Mheshimiwa Spika, utaona kwamba, wengi wa Waheshimiwa Wabunge wametoa michango ya kujaribu kuboresha na kuendeleza sekta yetu ya madini, wakitambua kwamba ni moja ya sekta ambazo kama ikisimamiwa vizuri ni kweli kwamba itachangia pato la Taifa kwa kadiri ya malengo yaliyo katika sera. Pia ni sekta ambayo katika nyakati ambazo hazitabiriki inaweza ikawa ndiyo sekta mkombozi kwa ajili ya kuchangia uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nitaanza na hoja ya Mgodi wa WDL ambao ni kweli kwamba umeacha uzalishaji kwa muda. Pia ni kweli kwamba kuacha uzalishaji kwa Mgodi huu wa WDL ambao Serikali ina hisa, inatokana na sababu ambazo ziko nje ya uwezo wetu. Kwa sababu, janga la Covid 19 ndilo ambalo lilisababisha kuanguka kwa soko la almasi kwa sababu walaji wengi wa madini haya ya almasi walikuwa wako katika lock down na kwa jinsi hiyo wakawa wameshindwa kununua almasi na soko la almasi likaanguka. Hata hivi tunavyoongea, ni kweli kwamba soko hili halijatengemaa sana na hivyo linakuwa ni sababu ambazo ziko nje ya uwezo wetu.

Mheshimiwa Spika, napenda kupokea maoni ya Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara ya Madini itakuwa bega kwa bega na kusaidia kuwezesha WDL ili kuweza kupata fedha katika benki zetu.

Mheshimiwa Spika, tukupe tu taarifa kwamba katika siku za karibuni benki zetu za ndani zimepata mwamko mkubwa sana wa kuona kwamba, biashara ya madini ni biashara inayolipa nao wameanza kuwekeza fedha katika sekta ya madini. Hili jambo halikuwa huko nyuma na tukubali kwamba, maisha ni dynamic, maisha yanakwenda, hatimaye benki zetu zimeelewa kwamba wanaweza wakakopesha wachimbaji nao pia wakapata faida na Wizara ya Madini iko nyuma ya Mgodi wa WDL na tunaamini kwamba wataweza kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kuongea pia hoja ya Geological Survey ambayo imechangiwa na Wabunge wengi pia, kwamba Geological Survey ndiyo taasisi ya Serikali ambayo inaweza ikafanya utafiti na hatimaye kutoa takwimu na ramani za kuonesha wapi madini yalipo.

Mheshimiwa Spika, napenda kusema tu kwamba pia Serikali imeendelea kutambua umuhimu wa GST. Katika mwaka wa 2020/2021 GST ilipewa fedha maalum kiasi cha shilingi bilioni 3.3 na fedha hizi zilielekezwa katika kuboresha miundombinu ya maabara, vifaa vya ugani, ilipewa magari sita na pia vifaa vya kuratibu matetemeko ya ardhi na vifaa vya jiofizikia. Kwa mtindo huo basi, GST imeendelea kujizatiti kuona kwamba itaendelea kufanya utafiti na kutoa taarifa za awali na kutoa ramani ambazo kimsingi zinapatikana pale GST.

Mheshimiwa Spika, wawekezaji wakubwa wale ambao sasa wanaweza wakaja kuleta taarifa zinazotaka feasibility study wanaweza wakatumia taarifa hizo za awali na wana ramani na hatimaye kuwapa wawekezaji wakubwa ili tuendelee kupata madini mengine yaliyotafitiwa vizuri kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge wa Ngara amesema kwa ajili ya Tin, Tungsten, Iron pamoja na madini mengine.

Mheshimiwa Spika, pia katika habari ya utafiti wa GST ni kweli kwamba utafiti katika hifadhi zetu umeshafanyika mahali mahali na hivi tunajua kabisa mahali ambapo kuna madini katika hifadhi za Selous, Rungwa, Moyowosi, Lukwati, Kigosi. Hivyo, Wizara itawasiliana na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuweka utaratibu bora wa kuendelea kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais ili tuweze kufanya uchimbaji katika maeneo haya ya hifadhi huku tukizingatia usalama wa mazingira ya hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nipende pia kusema kwamba tayari GST imeona umuhimu wa changamoto za wachimbaji wadogo kwama sio wote wanaoweza kufika Dodoma na kuleta sample zao kwa ajili ya kufanya analysis katika maabara. Kutokana na hali hiyo, tayari GST imeanza kupeleka huduma za maabara na jiolojia katika maeneo ya Geita na Chunya kwa kuanzisha ofisi za muda, na zoezi hili litakuwa endelevu ili kuendelea kupeleka huduma katika maeneo ya uchimbaji.

Mheshimiwa Spika, napenda pia niongee hoja iliyoletwa na Mbunge inayohusu helium gas; ni kweli kwamba katika Ziwa Rukwa tunao wingi wa gesi ya helium na wakati mwingine tujue tu kwamba ipo katika hatua ya utafiti wa kina, maana utafiti hadi kufikia uzalishaji lazima upitie hatua. Kwa hiyo tunapoongelea geli ya helium ni kweli kwamba mwekezaji yupo, Kampuni ya Helium One ipo na walishafanya utafiti ule ya preliminary na sasa wapo katika infill drilling. Infill drilling ni kuonyesha kwamba baada ya kuona kwamba mashapo yapo, sasa wanakwenda katika hatua ya kuthibitisha. Sasa wakimaliza hapo ndipo wanapoweza wakaja na feasibility study ambayo sasa ndio itatuonesha jinsi uzalishaji utakavyofanyika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni kweli kwamba helium gas ipo, uzalishaji haujaanza na kabla ya uzalishaji kuanza ni kweli kwamba Wizara itatoa semina elekezi kwa watu wanaozunguka maeneo ya uzalishaji ili kwamba waweze kunufaika na gesi hii ya helium.

Mheshimiwa Spika, pia Wabunge wameongelea juu ya kwamba hatujaanzisha migodi mipya siku za karibuni, ni kweli na kwamba pia tumekuwa na utegemezi sana juu ya madini ya dhahabu; naomba nitoe mfano kidogo ambao unaweza ukaleta perspective katika eneo hili. Tuna Madini ya aina nyingi, makaa ya mawe tani moja ni Dola 45, kilo moja ya dhahabu ni Sh.140,000,000, kwa vyovyote vile wawekezaji watapeleka fedha zao katika madini yanayolipa. Kwa hiyo, kwa msingi huo ndio maana dhahabu imeendelea ku-attract investment kwa sababu ni madini yatakayolipa na kurudisha fedha haraka. Kutokana na hilo ndio maana yameendelea kuchangia kwa wingi katika pato letu linalotokana na madini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kuamini kwamba kwa kuingia ubia na Tembo Nickel tukaiingiza aina mpya ya madini katika uzalishaji wa nchi yetu, lakini pia napenda kuamini kwamba Serikali inafanyia kazi utoaji wa leseni mpya mbili siku za karibuni, ambazo ni Mradi ya Nyanzaga uliopo Sengerema kwa Mheshimiwa Tabasam lakini pia na Mradi wa Rare Earth uliopo Songwe. Kwa kuingiza miradi hii pia tutaanza kuingiza maingizo mapya ya uchimbaji na uzalishaji katika nchi yetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Profesa.

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga hoja mkono. Ahsante sana. (Makofi)