Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini

Hon. Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Ngara, napenda kukushukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Ngara ni miongoni mwa majimbo yaliyojaliwa na Mwenyezi Mungu kuwa na madini ya aina mbalimbali. Tuna madini ya manganese ambayo concentration yake kwenye jiwe ni asilimia 30 hadi asilimia 55. Tuna madini ya tin, concentration yake kwenye sampuli ya jiwe ni asilimia 50 mpaka asilimia 68. Tuna madini ya tungsten, concentration yake ni asilimia 65 kwenye jiwe. Tuna madini ya chuma, concentration yake kwenye sampuli ya jiwe ni asilimia 75. Mbali na madini hayo, Ngara tumejaliwa kuwa madani ya nickel, cobalt, palladium na platinum.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kujaliwa huko kuna tatizo kubwa sana la ukosefu wa takwimu za wingi wa madini hasa madini ya manganese, tin, tungsten pamoja na chuma. Tunakosa takwimu ambazo zinaweza kuwafanya wawekezaji kuja kuwekeza kwenye jimbo la Ngara ili tuweze kuchimba madini hayo na wananchi walionichagua waweze kupata ajira kutokana na madini haya. Wananchi wa Jimbo la Ngara tumechoka kuendelea kukalia madini, kijiji kiko juu ya mwamba ambao umejaa madini. Wakati madini hayo yanaweza kuchimbwa yakatoa ajira na nchi ikakusanya kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kuishauri Wizara ya Madini kupitia Geological Survey of Tanzania waweze kufika kwenye Jimbo la Ngara waje kufanya utafiti kwenye maeneo yote haya niliyotaja yenye madini haya; waweze kwenda Bugarama, Kihinga, Mgaza na Ntanga wakafanye utafiti na watuletee takwimu za wingi wa madini haya kwa maana ya mtandao mzima wa mwamba wenye madini haya. Tukiweza kupata takwimu hizo, tuweze kupata wawekezaji waje kuwekeza kwenye Jimbo la Ngara na hatimaye wananchi waweze kupata ajira na madini hayo yaweze kutumika kuchangia kwenye pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, naomba pia niongelee suala local content pamoja na CSR. Kwa vile Jimbo la Ngara kuna mgodi mkubwa sana wa Kabanga Nickel ambao unakwenda kuanza hivi karibuni na kwa kuwa kwenye Jimbo letu la Ngara huu ni mgodi wetu wa kwanza mkubwa unaoenda kuanza, na kwa vile Halmashauri ya Wilaya ya Ngara haiungi mkono wale wanaosema fedha ibakie kwa Mzungu, sisi tunataka fedha tuletewe kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, miradi yetu ya maendeleo tusimamie wenyewe.

Mheshimiwa Spika, kwenye michango ya hapo leo asubuhi, nimesikia baadhi ya Waheshimiwa wanalalamika kwamba kipindi kingine unaweza ukaambiwa na Mzungu unataka nini, unataja shule mbili, anakujengea shule mbili kwa shilingi milioni mia kwa shule moja wakati zingejengwa kwa shilingi milioni 50, matokeo yake unakuta kwamba mpaka chenji yenu imebakia kwa Mzungu. Kusema kwamba hizi fedha zibakie kwa hao wawekezaji ni kuendeleza mawazo ya kikoloni na kuonesha kwamba sisi kama Taifa hatuwezi…

SPIKA: Mheshimiwa Ndaisaba hebu rudia hiyo pointi yako, Waheshimiwa Wabunge muwe mnawasikiliza Wabunge wanachoongea, hebu irudie vizuri Mheshimiwa. (Makofi/Kicheko)

MHE NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nasema hivi, suala la kusema kwamba fedha ibakie kwa Mzungu ni kuendeleza mawazo ya kikoloni kuonesha kwamba sisi hatuna uwezo wa kusimamia rasilimalia zetu, mipango yetu na kwamba ili tuweze kufanya maendeleo inabidi watu wengine waweze kutufanyia maendeleo jambo ambalo halikubaliki. Kwa minajili hiyo Mgodi wa Tembo Nickel utakapoanza kwenye Jimbo la Ngara naomba sana Wizara ya Madini ije itupatie mafunzo Halmashuari ya Wilaya ya Ngara hasa Madiwani na wananchi ili tuweze kusimamia fedha zetu sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama tunasema kwamba fedha ibakie kwa Mzungu, tunasema kwamba hata fedha tunayoletewa na Serikali Kuu kwenye halmashauri zetu hatuwezi kuzisimamia. Fedha inayotoka kwa Mzungu kama CSR na ile inayotoka Serikali Kuu haina utofauti, fedha ni fedha.

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, mmeona jinsi nilivyoshangaa, nani yuko right kati ya makofi yenu na maelezo haya? Mimi niko na Mheshimiwa Ndaisaba, malizia Mheshimiwa. (Makofi/Kicheko)

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, Jimbo la Ngara tumejiandaa kunufaika na Mgodi wa Kabanga Nickel almaarufu kama Tembo Nickel. Wananchi na makundi mbalimbali ya wafanyabiashara tumejiandaa kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali kwenye mgodi huu. Huduma hizo ni pamoja na usafiri, ulinzi, kuuza bidhaa mbalimbali hasa mbogamboga, matunda na vyakula vya aina mbalimbali ambavyo vinahitajika mgodini.

Mheshimiwa Spika, kama Wizara ya Madini haiwezi kuja kuandaa wananchi ni ngumu sana kama mgodi unaanza mwaka huu kupanda parachichi likaota na tukaweza kuuza pale mgodini. Naomba Wizara ya Madini ije kwenye Jimbo la Ngara iandae wananchi ili tuweze kunufaika na Mgodi huu wa Kabanga Nickel ambao unakwenda kuanza hivi karibuni.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema mwanzoni, kwenye Jimbo la Ngara tuna madini mapya na mwenyewe nimeenda maabara kuhakikisha kwamba kweli haya mawe yana madini. Tuna madini ya tin, tungsten na manganese.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, naomba sana Wizara ije Ngara kuwawezesha wachimbaji wadogo wadogo tuanze kuchimba madini hayo.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)