Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi hii. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Msalala, naomba na mimi nichangie katika hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nianze kwa kuipongeza Wizara kwa kazi kubwa inayoendelea kuifanya, lakini pia ni ukweli usiopingika kwamba tunaona kabisa Wizara ya Madini inavyofanya kazi kubwa katika kuhakikisha kwamba inachangia pato la uchumi wa nchi yetu katika kuimarisha mambo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuipongeza Wizara ya Madini kwa kuanzisha masoko mbalimbali na hasa katika Jimbo langu la Msalala, tumeona Waziri wa Madini ameweza kutoa maelekezo na Serikali imeweza kuanzisha masoko ya madini katika Kata za Bulyanhulu na Segese. Niombe tu Mheshimiwa Waziri baada ya kikao hiki cha Bunge basi uweze kutembelea ili kusikiliza changamoto za wachimbaji wadogo katika maeneo hayo, hususan Kakola, Bulyanhulu na Kata ya Segese.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona hotuba ya bajeti ilivyoelezea juu ya namna gani Wizara imejipanga katika kuhakikisha kwamba inakwenda kuwawezesha wachimbaji wadogowadogo. Niipongeze Wizara inafanya jitihada kubwa katika kuhakikisha kwamba inawawezesha wachimbaji wadogowadogo, lakini ni ukweli usiopingika kwamba bado kuna changamoto ndogondogo ambazo kimsingi niombe Wizara iweze kuzishughulikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii STAMICO wameonesha mkakati wao kwamba wanakwenda kujipanga katika kusimamia na kuwawezesha wachimbaji wadogo. Hata hivyo, katika maeneo yetu wachimbaji hawa wamekuwa wakinyanyasika sana kwa kukosa mitaji au mikopo kutoka katika taasisi mbalimbali. Niiombe Wizara iweze kufikiria sasa namna gani wanaweza kuanza kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo ambao ndiyo shokomzoba ya Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ametueleza hapa mchango wa wachimbaji wadogowadogo katika kuchangia uchumi wa pato la Taifa. Ni ukweli usiopingika kuwa hawa watu wanafanya kazi ngumu sana. Naomba nishauri twende tukaweke mkakati kuhakikisha kwamba tunakabiliana na matapeli kwa sababu wamekuwa wengi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri ametueleza hapa namna gani wamefanya jitihada kuwapatia wachimbaji wetu wadogo leseni, niipongeze Wizara katika baadhi ya maeneo yangu hususan Nyangarata na maeneo mengine katika Jimbo la Msalala, Wizara wamefanya hivyo lakini namna gani wanakwenda kutoa leseni hizi lazima tukueleze leo na tutoe ushauri, kwamba watu wanaokwenda kupata leseni katika maeneo haya ni watu ambao kimsingi sio original katika maeneo yale na wengi wao ukiwatafuta unakuta ni madalali. Leo hii unakuta mtu anamiliki shamba, lakini siyo shamba tu ameanzisha uchimbaji na akagundua madini katika maeneo yale, anatoka mtu anakotoka anakuja na leseni kujitambulisha pale na anasema yeye ndiyo mmiliki halali wa maeneo yale. Hii inamnyima haki mchimbaji wetu na tunampa kazi ngumu katika kuhakikisha kwamba anachangia pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe Waziri wa Madini wakae kama Wizara waone namna gani wanaweza wakauboresha huu mfumo wa kuomba kwa mtandao (portal). Watu wetu huko vijijini network hakuna Mheshimiwa Waziri inawanyima haki ya wao kumiliki leseni hizi. Niiombe Wizara iweze kuona namna gani wanaweza wakaweka mfumo mzuri ili iweze kuwarahisishia wachimbaji wetu wadogo, hususan wakazi wa Bulyanhulu, Nyangarata, Segese na maeneo mengine katika Jimbo langu la Msalala kuwa na haki hii ya kuweza kupata leseni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali, imefanya kazi kubwa kuhakikisha wanaunda ubia kati ya Twiga na Serikali na nipongeze jitihada ambazo zimesemwa. Mimi nizungumzie suala hili katika maeneo mawili; katika local content na fedha za CSR.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Musukuma amesema hapa katika Jimbo lake la Geita wanapewa fedha za CSR kiasi cha shilingi takribani bilioni 10, lakini inasikitisha kuona Jimbo langu la Msalala ambalo tunamiliki Mgodi wa Bulyanhulu, tunapokea fedha za CSR bilioni 2.5 tu na wakati migodi yote ipo Tanzania. Kwa nini Geita wapokee bilioni 10 na sisi tupokee bilioni mbili? Namwomba Mheshimiwa Waziri akimaliza hapa tufanye ziara tuone ni kwa nini kuna tofauti hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo yote tunayojadili hapa ni ukweli usiopingika kwamba watumishi wa kwenye Tume ya Madini ni wengi lakini bajeti yao ni ndogo. Ukiangalia watumishi katika Wizara ni wachache lakini bajeti kubwa inakwenda Wizarani na hii inasababisha Tume ya Madini isifanye kazi zake kiuhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, makampuni haya; GGM na makampuni mengine yote, hususan nizungumzie katika Jimbo langu la Msalala, Bulyanhulu pale, kumekuwa na uvunjaji mkubwa wa sheria ya local content. Leo hii tunazungumzia namna gani ya kuwakuza wachimbaji wadogo kutoka katika ngazi ya chini kwenda ngazi ya kati na tuwafanye wachimbaji hao wawe wakubwa lakini ni ukweli usiopingika tunaona kabisa migodi hii wanachangia kwa kiasi kikubwa kuvunja Sheria ya Local Content. Tuna wafanyabiashara wana uwezo wa ku-supply katika migodi yetu hii hawana kazi, kumekuwa na matapeli katikati hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nikiwa bado M-NEC nilimsikia Mheshimiwa Waziri akitoa maelekezo katika Mgodi wa GGM waweze kutekeleza sheria hiyo ya local content kuhakikisha kwamba wazawa wanapewa nafasi lakini watu hawa wana kiburi, hawajatekeleza yale aliyowaambia. Watu hawa wana dharau kubwa, nenda kawaeleze kwamba sisi kama wananchi tunaoishi katika maeneo yale ya mgodi tuna-play part kubwa ya kuhakikisha usalama wao na mali zao na ni lazima sasa wakazi tunaoishi katika maeneo yale hususan Bulyanhulu na meneo mengine kama ya Bugarama tunanufaika na migodi hiyo. Kama leo hii hawataweza kutekeleza sheria hii ya local content…

T A A R I F A

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kassim, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Musukuma.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nampa taarifa mzungumzaji kwamba baada ya tamko la Mheshimiwa Naibu Waziri kule GGM kwamba GGM watekeleze local content, walitekeleza kwa kutoa zile kazi kama ku-supply nyanya na vitunguu, zile kazi zenye maslahi zote wanafanya Wazulu.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea taarifa hiyo ya Mheshimiwa Musukuma kwa mikono miwili na sisi Wanamsalala tulishafikisha kilio chetu …

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kassim, inabidi usubiri kwanza nikuite tena ndiyo uzungumze. (Kicheko)

Mheshimiwa Kassim Iddi Iddi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupokea taarifa hii kwa mikono miwili, lakini unisamehe kwa sababu ya unjuka, nitazoea. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana asilimia 100 na Mheshimiwa Musukuma. Leo hii makampuni haya ni ukweli usiopingika Mheshimiwa Waziri anafahamu, baada ya kuona Wizara imeweka mifumo ya kudhibiti utoroshaji wa madini sasa wameamua kuja na mfumo mpya kuhakikisha wanatupiga sisi Serikali lakini pia Halmashauri yangu ya Msalala.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili nimeshalifikisha kwa Waziri na naomba alishughulikie haraka iwezekanavyo. Tumekuwa wavumilivu sana wananchi wa Bulyankhulu na Msalala. Tunatamani mgodi huu uendelee kuwepo, leo hii tulikuwa tunazungumza kwamba kampuni hizi zimeanzisha kampuni ndogo pale Dar es Salaam, TCL Mheshimiwa Waziri, tumeshalizungumza hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii mama anayelima nyanya katika Jimbo langu hawezi ku-supply nyanya kwenye mgodi mpaka aende Dar es Salaam. Hivyo mnatutoreshea mapato katika Halmashauri yetu. Naomba Mheshimiwa Waziri alichukue hili haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri suala la barabara, fedha nendeni mkatekeleze haya barabara ianze kupitika. Mimi na wananchi wangu tumekubaliana ikifika mwezi wa Saba barabara haijatengenezwa, fedha hazijatoka, Mheshimiwa Waziri sisi tutaziba barabara, kwa sababu wananchi wangu wanahangaika mno. Tunanufaika vipi na madini haya kama wananchi wetu wanakula vumbi? Kwa hiyo, naomba Wizara ya itekeleze haya ili wananchi wetu waweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja asilimia mia moja na mbili. (Makofi)