Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Kwanza niipongeze sana wizara lakini, nianze nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Waziri kwa sisi tunaotoka kwenye maeneo ya madini ninaweza nikasema ni waziri wa kwanza umevunja rekodi hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niwapongeze wasaidizi wako Katibu Mkuu pamoja na timu yake na hili ni fundisho kwamba ukiangalia hii wizara, ni mjumbe wa kamati. Tunama- professor wa kutosha na kweli wameutendea haki u-professor wao. Ukiangalia tulikotoka na tulipo mwenyewe na-appreciate mchango wa ma-professor wa madini, wa wizara ya madini hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nianze kwa kusema tulipofikia sasa kwenye Wizara ya hii Madini tusirudi nyuma, tusikatishane tamaa, tuangalie wapi ambapo tuna mapungufu tubadilishe twende mbele. Na mfano mzuri unaweza ukaona leo wakati unatangaza wageni pale ni wizara ya kwanza ambayo mabenki yote yamehudhuria hapa kwasababu wanajua hii wizara ni pesa. Tusirudi nyuma turekebishe yale mapungufu ambayo yamejitokeza kwenye kipindi hiki cha miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nilitaka kushauri kwenye upande wa Tanzanite, ni mjumbe wa kamati, Serikali lazima tuje na utaratibu mpya na ni lazima tuambizane ukweli na Mheshimiwa Rais ametuambia tuseme ukweli. Ni aibu kubwa sana kuwa na Taifa ambalo lina-search watu kwa kuvua nguo hii haiwezekani! Sisi tumeenda kama wajumbe mimi nimejionea mwenyewe mwanajeshi ambaye ni jeshi ambalo tunaloliamini anafanya kazi ya ku-search wamasai hii ni dharau ya hatari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata kama kuna mtu alikamatwa nyie ambao hamjapita kwenye machimbo, mtu anaweza kukaa huko maduarani akakaa wiki nzima hajapata hata mia tano. Kwa hiyo, mtu ukimkamata anakagonga kashilingi 2000 inasababisha watu wa-search-iwe kuvuliwa nguo kweli una benefit nini nakajiwe kashilingi 2000. Na hata ukiangalia pale kesi nyingi anakamatwa mtu na vumbi kwenye koti linathamani ya Shilingi 700 halafu mnatumia difenda kutoa pale melelani kumpeleka kituo cha polisi hii ni kitu ambacho lazima tuone namna ya kubadilisha ule utaratibu wa pale tu-deal na wezi tusi-deal na watu wanaganga njaa. Lakini lingine…

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Kuna taarifa Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma Mheshimiwa Christopher Olonyokie Ole-Sendeka.

T A A R I F A

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kutoa taarifa kwa Mheshimiwa Mbunge, sio tu kwamba wananchi na wachimbaji wa Mererani wanavuliwa nguo, wakati ule kabla ya kamati zote mbili za Mbunge kufika, bali hata baada ya maelekezo ya Waziri wa Madini na maelekezo ya Kamati ya Madini, na baada ya ziara ya Kamati inayoshughulikia masuala ya ulinzi, mpaka leo watu 20 wanawekwa chumba kimoja, wanavuliwa nguo, zote halafu mnaambiwa mchuchumae halafu ukaguliwe na mtoto wa miaka 23, ambaye amevaa kombati za jeshi ni ukiukwaji wa haki za binadamu nchi yetu inaheshimu na kuthamini misingi ya utu, usawa na haki za binadamu. Kitendo hiki ni cha aibu ni fedheha, na mimi baadaye nitataka kujua Waziri mwenye dhamana… (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ole-Sendeka tusije tukafanya mambo kinyume na kanuni zetu sisi wenyewe, naona hapa na yeye ana fursa yake ya kuchangia baadaye, na hicho alichokuwa anakisema kwasababu kama ninavyosema siku zote sina taarifa hapa maana hizo ni tuhuma mahususi. Kwa hiyo, ndio maana sitamuuliza Mheshimiwa Musukuma kwamba anapokea hiyo taarifa au hapana. Kwa hiyo, Mheshimiwa Musukuma malizia mchango wako.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina dakika mbili nilizochangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nishukuru sana ile timu ya Spika, Mheshimiwa Ndugai, alipounda timu kwenda kuchunguza Mererani, ilifanya kazi nzuri sana, ikiongozwa nadhani na Mheshimiwa Doto na Wajumbe wengine na Tume ndiyo ilimuondoa hata ndugu yangu, Mheshimiwa Simbachawene. Baada ya hapo Mheshimiwa Rais aliunde Tume iliyoongozwa na akina Profesa Mruma na Mheshimiwa Profesa Kabudi ya kuchunguza mgogoro wa Mererani. Baada ya kutoa taarifa ilionekana yule ni mwizi na akakubali kulipa. Sasa tunatafutiana ajali, kama mtu amehojiwa na timu ya maprofesa na ameshakiri kuachia mgodi, anaitwa Bungeni kuja kuhutubia Kamati yaani criminals tunaanza kuwaleta Bungeni, tunarudi kubaya. Niombe, tulipo ni kuzuri, tusikubali tena kurudi nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine nizungumzie CSR. Mimi natoka Geita, tulipiga makofi mengi sana, Alhamdulillah tunapata CSR shilingi bilioni 10 kwenye halmashauri yetu. Hata hivyo, hii CSR haina mpangilio, ni kama likitu tu limetupwa, halina mwenyewe. Wizara ya Madini na TAMISEMI ni nini kiliwafanya mkatoa uhuru wa kumuachia Mkuu wa Mkoa anakuwa anatuamulia sisi? Mkuu wa Mkoa amepewa mamlaka ya kuamua hela za Halmashauri kajenge darasa, kajenge hoteli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vitu vingine vinauma, najua nachokiongea na Mheshimiwa Waziri anakijua. Mimi ninazo nyaraka hapa, kwa mwaka mmoja Halmashauri za Geita na Geita Mjini, Mkuu wa Mkoa na timu yake wamejilipa posho zaidi ya shilingi milioni 600; hiki kitu hakiwezekani, ninao ushahidi hapa. Kwa nini hizi pesa za CSR zisitumike kwenye Halmashauri yetu, watu wa GGM wao waje kufanya kama ukaguzi na manunuzi yote yafanywe na procurement yetu ya Halmashauri. Tofauti na ilivyo sasa, mmempa mamlaka Mkuu wa Mkoa kuingia kama Waziri anasema sitaki hiki, nataka hiki, sasa sisi tuna kazi gani kama Halmashauri? Niombe sana Mheshimiwa Waziri akinyanyuka hapa aje na hayo majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wachimbaji wadogo wanafanya kazi kubwa sana na tunapolilia maeneo mkubali kuyaachia. Natoa mfano kule Geita, kuna eneo kule Busolwa linamilikiwa na TLS, miaka nenda rudi. Wachimbaji wanachimba kama mbayuwayu, halafu hapa tunajisifu tunakusanya kutoka kwa wachimbaji wadogo. Mheshimiwa Waziri, ni kwa nini asitamke leo kwamba lile eneo mnawaachia vijana wetu waweze kuhangaika kwa sababu hata muda wa leseni umeshamalizika?

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine naomba Serikali mzungumze lugha moja. Mheshimiwa Spika jana amezungumza kitu kizuri sana kwamba Serikali ni moja, inakuwa na kauli tofauti, Wizara ya Madini inatoa leseni, ukipewa leseni ukiipeleka kule unakutana na DC naye ana maamuzi yake. Mimi sitaki kuwa muongo, Waziri nenda Bariadi leo, leseni zina karibu miezi sita DC amekataa.

Sasa nauliza Wizara na DC nani mkubwa? Zungumzeni lugha moja, kama mnataka leseni atoe Mkuu wa Wilaya tusihangaike kuja kutupa nauli zetu huku, tukae na Wakuu wa Wilaya wamalize. Mtu anakuja anakaa mwezi, anarudi kule tena anakutana na DC naye ana masharti yake anataka kufuta leseni, Tanzania gani hii? Ni vizuri sana tukazungumza lugha moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba shemeji yangu, yeye ni Mjumbe mwenzetu…

MBUNGE FULANI: Nani?

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Anajijua, amezungumza kuhusu TEITI. Mimi nadhani ungeshauri waongozwe hela, sisi wote tunasoma, tunaletewa ripoti Pamoja, tunachoangalia hapa OC ya TEITI wanapewa asilimia 100; tunazo taarifa. Wamefanya utafiti kwa kum-consult Mzumbe, amelipwa shilingi milioni 250 mwaka jana na sasa wanaendelea. Tunaposema hawana hela, mimi nadhani…

T A A R I F A

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Musukuma, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jesca Kishoa.

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nataka nimpe taarifa mzungumzaji anayeendelea kuzungumza sasa hivi, yeye anazungumzia fedha za OC, mimi nazungumzia fedha za maendeleo ambazo zimeweza kuwawezesha TEITI kuendelea kuboresha majukumu yao.

NAIBU SPIKA: Kwanza kabla sijakuuliza Mheshimiwa Musukuma, nilikuwa najiuliza, hapa nimemtambulisha Mwenyekiti wa Bodi ya TEITI, siyo? Ama mimi ndio nilikuwa nimesoma vibaya, si yupo?

WABUNGE FULANI: Ndiyo.

NAIBU SPIKA: Sasa kama anayosema Mheshimiwa Jesca Kishoa yako sawasawa, hii taasisi hapa ilikuwa inafanya nini? Kwa sababu si maana yake hawafanyi kazi yoyote kwa sababu hawana hela, ndiyo maana yake. Kama hawafanyi kazi sasa hapa wamekuja kufanya nini?

Mheshimiwa Waziri atatupa maelezo baadaye kwa sababu kama hawafanyi shughuli yoyote wanatumia hela zetu kwa ajili ya nini? Maana mchango unaonesha hakuna fedha isipokuwa za kula, si ndiyo Other Charges. Hakuna shughuli yaani, si ndiyo maana yake? Amesema hapa mwishoni ili wafanye kazi, maana yake hawafanyi kazi. Mheshimiwa Waziri, atatufafanulia jambo hilo.

Mheshimiwa Musukuma endelea na mchango wako.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, simuelewi Mheshimiwa Jesca, hii kazi inayofanywa na Mzumbe ni matumizi ama ndiyo kazi ya TEITI? Sasa sielewi, lakini najua kinachomsumbua shemeji yangu, wala msiwe na wasiwasi, ni kukaa mbali na shemeji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)