Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini

Hon. Catherine Valentine Magige

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini

MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza nianze kwa kumpongeza Waziri na timu yake nzima kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, moja kwa moja nijielekeze kwenye mchango wangu. Naipongeza Serikali kwa kutenga masoko ya madini karibu nchi nzima. Tumeshuhudia masoko ya madini katika mikoa mbalimbali. Serikali imeshirikiana na Makatibu Tawala wa Mikoa mbalimbali, wametenga masoko ya madini na tumeshuhudia masoko hayo zaidi ya 25 na vituo mbalimbali vya madini, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kanuni za uendeshaji wa masoko haya, tunafahamu kuwa majengo mengi ambayo yana masoko haya ni ya Serikali. Mfano tu ni jengo la National Housing la Dar es Salaam PSSSF ya Arusha na AICC. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa kwa wafanyabiashara wa madini ya vito ni kwamba wanalipa VAT asilimia 18 Serikalini. Wanatozo nyingi sana ambazo wanatozwa, lakini wanapokuja kulipa majengo yale ambayo ni ya Serikali, wanapokuja kulipia kodi za majengo, wanalipa 18% ya VAT na bado wanatozo nyingine nyingi ambazo zinaenda huku huku Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais, mama yetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alisema, lazima tutengeneze mazingira rafiki ya biashara. Wafanyabiashara hawa wa madini kwa kweli mazingira haya ambayo wanapitia sasa hivi siyo rafiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali ni kuhakikisha hii VAT ya asilimia 18 ambayo wanatozwa kwenye kodi ya majengo, iondolewe kabisa wabaki na kodi nyingine. Kwa sababu zote hizi zinaenda Serikalini. Kwa hiyo, inakuwa kama tunawatoza wafanyabiashara hawa kodi mara nyingi hali ambayo inapeleka wanashindwa kabisa kufanya biashara zao; na inasababisha wafanyabiashara ambao sio waaminifu wanatorosha madini. Kwa hiyo, ukiangalia sisi wenyewe tunatengeneza hali ngumu ya wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine ni juu ya malipo ya PAYEE kwa wachimbaji wadogo wa Tanzanite. TRA imekuwa inawalazimisha wachimbaji kulipa PAYEE ya shilingi 200,000/= mpaka shilingi 400,000/= kwa wafanyakazi kila mwezi. Kibaya zaidi, hakuna uhalisia wa makadirio ya PAYEE ambayo wanalazimishwa kulipa kwa wafanyakazi kila mwezi. Kibaya zaidi na ni double standard ni wafanyabiashara wa Tanzanite Mererani tu ndio ambao wanalipishwa hii, lakini wafanyabiashara wa dhahabu, almasi hawalipishwi hii PAYEE kwa ajili ya wafanyakazi wao, ni wafanyabiashara wa Mererani tu, kwa hiyo, hii ni double standard.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, TRA watafute njia nzuri ya kutafuta kodi, siyo kuwaonea hawa wafanyabiashara. Wanaweza wakawalipisha hata asilimia moja ya madini yaliyothaminishwa, kuliko hivi ambavyo wanafanyiwa na ni wafanyabiashara walioko Mererani tu, yaani wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite, lakini kwa akina rafiki yangu Mheshimiwa Musukuma hapa Geita na sehemu nyingine nyingi hawalipishwi. Kwa hiyo naiomba Serikali iangalie hiki kitu, inakuwaje na ni kwa sababu gani, wafanyabiashara wa Tanzanite wa Mererani ndiyo wanalipishwa peke yao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mchango wangu nijielekeze kwenye malipo ya fidia ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF). WCF wamekuwa wakitaka wafanyakazi kukatwa, kuna malipo ambayo wanatakiwa walipe ambayo hayaeleweki. Hayaeleweki haya malipo ni ya namna gani, wanakatwa wanavyotaka wao. Sasa naomba Serikali ikae iangalie haya malipo ya WCF yanawekwaje wekwaje! kwa sababu, ili yaweze kuwa na uhalisia kamili na vile vile, ili tutende haki kwa hawa wafanyabiashara na tutende haki kwa hii WCF. Kwa hiyo, ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba wakae waangalie haya malipo yako vipi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais, mama Samia Suluhu Hassan alisema, kumekuwepo na madini kwenye hifadhi zetu. Hifadhi zetu zinafahamika na akasema madini yachimbwe. Ushauri wangu kwa Serikali, tuwatumie GST - Wakala wa Jiolojia na Utafiti, waende kule kwenye hifadhi zetu maana zote zinajulikana, waangalie sehemu zenye madini. Bila kutumia GST watu wataenda watafanya tu uchimbaji holela, maana hawajui wapi kuna madini wanaenda kwa kukisia, lakini GST wakifanya utafiti tutajua moja kwa moja wapi kuna madini na vile vile itatusaidia kuepukana na uharibifu wa mazingira kwenye mbuga zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, GST kama hawana pesa Wizara, Serikali iwapatie GST pesa, wakafanye utafiti, tujue maeneo haya ya hifadhi, ni wapi kuna madini na wapi hakuna madini ili tuepuke uvamizi. Maana watu wanaweza tu kwa kuwa wameambiwa hifadhi hii ina madini, wakaenda wakavamia bila kuwa na utafiti hasa eneo gani, matokeo yake tukasababisha uharibifu wa mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie mchango wangu kwa kumpongeza mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassani, nimpongeze sana kwa kuwa Rais mwanamke wa kwanza, wanawake tunajivunia kuwa na Rais mwanamke. Vile vile, nimpongeze Mama Samia kesho anaenda kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi. Naomba nimpongeze sana maana najua tunampa kura zote za ndiyo tukiwemo na sisi wanawake, tuko mstari wa mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue pia nafasi hii kumpongeza mama Samia na nimwambie hatutamwangusha, tunajua utendaji wake wa kazi na tupo naye. Nina imani na haya niliyoyaongea hapa, Wizara itayafanyia kazi, Mheshimiwa Doto Biteko namwamini, najua haya mtayachukua na mtayafanyia kazi kwa haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)