Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Geophrey Mizengo Pinda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria

NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipitie maeneo machache ambayo Waheshimiwa Wabunge katika mjadala wa leo walijaribu kuibua hoja. Kwa ujumla wake tunawashukuru sana Wabunge wote waliochangia na ninadhani Mheshimiwa Waziri wakati atakapokuwa anahitimisha atatambua kwa majina mchango wa Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa eneo langu nitazungumzia hoja mbili; moja, ni msongamano wa mahabusu katika Mahakama zetu ambapo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walichangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi ni kweli kwamba kumekuwepo na msongamano wa mahabusu katika Magereza zetu. Hii kwanza ni kutokana na Magereza zetu kutokumudu hiyo namba ya wahalifu wanaopelekwa pale. Hii ni kwa sababu Magereza nyingi nchini zimejengwa muda mrefu sana na nyingi zilijengwa siku za nyuma, hata nchi yetu kabla ya kupata uhuru. Kwa hiyo, utakuta Magereza ilijengwa wakati ambapo Tanzania haina idadi ya Watanzania ambao sasa tuko milioni 60.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoa tu mfano, Gereza la Mpanda pale ambalo lilijengwa 1947 lilikuwa na uwezo wa kuchukua watu chini ya 200, lakini kwa sasa lina watu zaidi ya 800. Magereza kama hii, ziko nyingi hapa nchini na hivyo kusababisha mlundikano wa watu, lakini juhudi mbalimbali zinafanyika na kwa kushirikiana na taasisi nyingine kama Magereza ambayo iko Wizara ya Mambo ya Ndani, sasa hivi kuna program za kujenga Magereza mapya na yale yaliyopo kuyaongezea uwezo ili tuweze kumudu idadi ya wahalifu ambao kila uchwao wanaongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiki kitu cha kuongezeka kwa wahalifu hatuwezi kukikwepa kwa sababu idadi yenyewe ya Watanzania ni kubwa na ukubwa huu unasababisha misukumano ya hapa na pale ambayo inasababisha kwenda kwenye vyombo vya utoaji haki; na wakati wa taratibu zile za kusubiri kukamilisha eneo hili la utoaji haki, basi yule aliyetuhumiwa anakuwa amehifadhiwa mahali ambapo vilevile kwake ni salama kwa upande mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima Wabunge wote tushirikiane kwa sababu tunatoka kwenye maeneo hayo tuone namna nzuri ya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wetu ili wasiendelee kuingia kwenye makosa ambayo hawakuyatarajia, kusudi pamoja na mambo mengine tuendelee sasa kupunguza uhalifu nchini. Kwa sasa katika juhudi za kupunguza msongamano, tuna vyombo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, chombo cha kwanza ambacho kinatusaidia sana kupunguza msongamano ni pamoja na Mheshimiwa Rais kutoa msamaha kwa wale ambao vifungo vyao vinaonekana kufikia mwisho na kimsingi huko kumekuwa na idadi kubwa ya wafungwa ambao wanapata msamaha wa Rais. Vilevile kwa kupitia Mahakama, kujaribu kuziondoa kesi ambazo hazina mashiko. Vilevile tuna mfumo wa plea bargaining ambapo DPP kwa mamlaka aliyopewa amekuwa akijaribu sana kupunguza idadi ya wale mahabusu wetu ambao wengine wanasubiri kesi huko Mahakamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende eneo lingine la kubambikiwa kesi. Baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamesema kumekuwa na utaratibu wa kubambikiwa kesi kwa wananchi. Napenda kusema tu kwamba Serikali yetu tukufu kupitia chombo chake cha utoaji wa haki hakina utaratibu wa kumbambikia mtu kesi. Hizi kesi mara nyingi kama kuna sura ya kubambikiwa, wanaanzana huko walikoanzia safari ya kuchokozana, lakini huwezi kukamatwa kwa kesi ya wizi wa kuku, ukafika Mahakamani ukaambiwa unashitakiwa kwa kosa la kuiba ng’ombe, haiwezekani. Kwa Serikali yangu hiki kitu hakipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kwenye eneo hili la ubambikizwaji kesi, nawaomba Waheshimiwa Wabunge, ushirikiano ni kitu muhimu sana. Tushirikiane kwenye mazingira, kwa sababu unaposema kubambikiwa kesi, inahitaji ushahidi wa kutosha kuonesha kwamba kweli mtuhumiwa au mlalamikiwa kabambikiwa kesi. Kwa sababu, mbambikiaji, yule anayefanya zoezi la kumbambikia kesi ni mhalifu kama wahalifu wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tukipata taarifa za mapema, maana yake huyo aliyehusika kubambika kesi atatueleza nia yake, naye anatakiwa kwenye vyombo vya sheria ili tukamwelewe vizuri, kwa nini aliweka nia ya kubambika kesi? Kama ni sehemu ya watumishi wetu wa Serikali, tunachukua hatua za haraka sana, kwa sababu kwanza huko ni kuidhalilisha Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile suala la kubambika kesi lina uwezo wa kumalizika katika maeneo ya ngazi ya chini sana. Tukipata ushahidi wa kutosha kwamba, kweli katika mazingira yaliyo wazi au kulingana na mazingira yake inaonekana kuna watumishi wamejihusisha na kuwabambikia kesi wananchi wetu, kama nilivyosema mwanzo, hatua kali sana zinachukuliwa dhidi yao. Kwa hiyo, naomba sana tushirikiane.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kwenye ngazi ya Mahakama, sisi tuna Kamati ya Maadili ya Mikoa ambayo Mwenyekiti wake ni Mkuu wa Mkoa na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na kwenye wilaya hali kadhalika. Sasa mambo haya yanapotokea katika ngazi hizo, tukiwa na uhakika sisi Wabunge, tupeleke haya maelezo kwa Wakuu wa Mikoa ili kama ni Hakimu amehusishwa na jambo hili, basi kamati zile zipitie kupitia ile Kamati ya Maadili, ili tuweze kumbaini na baadaye hatua za kisheria dhidi yake ziweze kuchukuliwa. Kama ni Idara ya Polisi, nako huko vilevile. Tunapopata Ushahidi inasaidia kwa sababu, jambo la kubambikia linahitaji ukaribu sana katika suala la kulithibitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ile tu kwamba wamebambikiwa kwa maelezo ya mlalamikaji anapokuja kwako, inawezekana likawa na ukweli au lisiwe na ukweli. Hivyo, basi nawaomba tuwe na ushirikiano wa karibu sana. Mahakama ndiyo sehemu ambayo haki zote zinatolewa kwa kuzingatia sheria ambazo sisi Waheshimiwa Wabunge tumekaa hapa na tunazitunga ili ziende zikatumike vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyaeleza haya mawili kwenye maeneo yangu sasa niache nafasi kwa Mheshimiwa Waziri ambaye kwa kweli, ndiye alikuwa mtoa hoja, aweze kutusaidia kukamilisha hoja hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)