Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami nichangie kuhusiana na hoja iliyopo mbele yetu. Nianze kwanza kwa kumpongeza Waziri wa Sheria na Katiba pamoja na Naibu Waziri na Watendaji wote wa Mahakama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kupongeza Bunge lako, kukupongeza wewe na Mheshimiwa Spika kwa ajili ya kutunga Sheria ya Matumizi ya Kiswahili katika Mahakama zetu na vyombo vingine vya utoaji haki. Kwa kweli kutunga sheria huku kumesaidia sana wananchi wengi kupata haki kwa sababu wengi walikuwa wanahukumiwa kwa kutojua tu lugha inayozungumziwa katika Mahakama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie kuhusiana na kesi za ubakaji hasa katika Mkoa wetu wa Iringa. Tuna kesi zaidi ya 400 katika mkoa wetu, lakini naona zinachukua muda mrefu sana. Nilikuwa najiuliza ni kwa nini kesi hizi zisiwe na limit? Kwa sababu kuna nyingine ambazo zinakuwa tayari zimeshakuwa na vidhibiti, lakini tunaona kwamba zinachukua muda mrefu. Kesi hizi zimekuwa zikiwadhalilisha sana watoto na hata akina mama wanaobakwa, kwa sababu zimekuwa zinanyima hata haki zao za binadamu kwa kuchukua muda mrefu. Sasa naona ifike sehemu ziwe na time limit. Ziwekewe limit za kuhukumiwa hizi kesi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie kuhusiana na msaada wa kisheria. Pamoja na kuwa nimeona kwamba limezungumziwa katika hotuba ya Waziri, lakini bado msaada wa kisheria umekuwa ukiwanyima wananchi wanaoshindwa kuweka Wakili kwa ajili ya kupatiwa haki. Sasa tulipitisha hapa Bungeni kwa nia nzuri kabisa na tulikuwa tunajua kwamba baada ya kupitisha, zile changamoto pengine zingeweza kukamilika kwa wakati, lakini unaona bado kabisa wananchi wanakosa msaada wa kisheria na wanakosa haki zao na kwa sababu wanashindwa kuweka Wakili kwa ajili ya kuwatetea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani tathmini ifanyike katika mikoa na hasa sehemu ambazo zina kesi nyingi, kwa mfano mkoa wetu wa Iringa ambao una kesi nyingi sana na tunaona kuna mashirika ambayo yanasaidia msaada wa kisheria, lakini bado wananchi wanalalamika kwa kukosa haki kwa kutokuwa na Wakili wa kuwatetea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia pale Mkoani kwetu Iringa kuna changamoto. Tuna kesi nyingi sana za mauaji ambazo kutokana na kutokuwa na fungu la kutosha kuendesha hizi kesi, basi unaona wale wafungwa kule mahabusu wanakaa muda mrefu, kesi hazikamiliki. Naomba kesi za mauaji pia zipewe kipaumbele, fungu lipelekwe ili zihukumiwe haraka. Kama mtu amefanya kosa, basi aweze kuhukumiwa na kama hana hatia aweze kuondolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia kuhusiana na sheria kandamizi kwa wanawake. Wanawake wengi wanakandamizwa sana kwenye mambo ya mirathi, ndoa, talaka; maeneo haya matatu tunaona yanaongoza, hasa kuna sheria tatu. Kwanza, kuna sheria ambayo tumekuwa tukiitunga hapa Bungeni kuna sheria nyingine ni za kidini na sheria za kimila.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria za Bunge siyo mbaya sana, lakini sheria za kidini sitaki kuzisema kwa sababu zenyewe zinaenda kiimani zaidi. Sheria ambazo ni kandamizi ni hizi za kimila kwa sababu zinafuata mfumo dume kwa kuwa zimejikita sana katika mila na desturi zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali ni je, Sheria za Kimila haziwezi kurekebishwa ziendane na wakati? Ni dhahiri kuwa Sheria hizi za Kimila utaona nyingi sana zinafafana, yaani hazipo uniform katika kila maeneo. Kwa kutambua hilo, nafikiri sheria zilizoingizwa kwenye sheria ya kimila ndani ya mfumo wa Sheria za Tanzania (Judicature and Application of Laws Act) ya 11 na 12 zimeeleza kwamba Halmashauri za Wilaya ziwe na utaratibu wa kupitia hizi sheria na maeneo ya halmashauri zao, lakini tunaona bado halmashauri nyingi hazijaweza kuzipitisha hizi sheria za kimila. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utaona sasa wanawake wengi sana na hata watoto wanapata shida kwa sababu sheria hii bado haijaweza kupitiwa ili iendane na mila na desturi ambazo wananchi tumo. Je, sasa ni lini Waziri wa Sheria ataweka huu mfumo kwamba ziweze kupita katika halmashauri zetu ili zitendr haki kwa wananchi ambao tunaoishi nao?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anakuja kuhitimisha hoja yake hapa, atueleze kwa sababu hizi Sheria za Kimila zimekuwa zikimkandamiza sana mwanamke kwenye mambo mengi, kwenye mirathi na mambo mengi sana. Kwa hiyo, naomba atakapokuja hapa kutuelezea, aelezee kuhusiana na hii Sheria ya Kimila kuingizwa katika sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nielezee kuhusiana na uadilifu wa kutoa haki katika vyombo vya haki. Ni muhimu sana na ninaomba suala hili liende moja kwa moja na maboresho ya maslahi ya wafanyakazi au Mahakimu ambao wanahukumu kesi zetu. Tunaona kwamba watumishi wa kada hii ya sheria au Mahakimu ni muhimu wakaboreshewa, hata alivyokuwa anaelezea Mwenyekiti wa Katiba na Sheria ameona kuna tatizo kwamba bado hawajaboreshewa maslahi yao. Sasa inakuwa ni shida sana kutenda haki kama Mahakimu wenyewe. Wanahukumu kesi za mabilioni ya fedha lakini wao wenyewe bado hawana mshahara wa kutosha, pengine bado hata mazingira yao hayako vizuri, ni rahisi sana kuweza kukubaliana kuchukua rushwa na kutotenda haki kwa yule mtu wanayemhukumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nielezee kuhusu miundombinu na maboresho katika Mahakama hasa ya Mwanzo. Mahakama za Mwanzo kwa kweli katika sehemu nyingi, hata katika Mkoa wetu wa Iringa zina hali mbaya sana. Mahakama za Mwanzo nyingi wamepangisha au nyingine zina majengo ambayo siyo mazuri. Kwa hiyo, naomba kuwepo na maboresho makubwa katika Mahakama zetu za Mwanzo kwa sababu ndicho chombo cha kwanza ambacho mwananchi anakwenda kudai haki yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, utakuta Mahakama ina nyufa, hata anaye hukumiwa anaweza akafiri jengo linaweza likambomokea wakati wowote hata bado haki haijatolewa. Kwa hiyo, ni muhimu sana hizi Mahakama zikaboreshwa kwa sababu ndizo Mahakama ambazo mwananchi anakwenda kudai haki yake na ni Mahakama ya Mwanzo kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri aone umuhimu wa kuja kuboresha hasa Mahakama zetu za Mkoa wa Iringa ambazo nyingi kabisa zipo katika hali mbaya na kwa kweli ni kitu ambacho naomba kizingatiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haya niliyozungumza, naunga mkono hoja. (Makofi)