Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. George Natany Malima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa sababu ya kunipa nafasi na mimi nichangie katika hotuba ya Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Nataka niwapongeze sana kwa kazi nzuri ambayo inaendelea kufanyika katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kuchangia katika Taasisi ya TAKUKURU. Taasisi hii inafanya kazi nzuri kwa ajili ya kupambana na rushwa na mambo ya ufisadi katika nchi yetu. Lakini katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri alikuwa amesema Taasisi moja ya Transparency International ilitupa alama ya 38; hii ni ishara kwamba bado tuna kazi kubwa ya kufanya kwa ajili ya kupambana na vitendo hivi vya rushwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi ninapenda kutoa ushauri kwa Serikali, TAKUKURU ijikite sana kwenye utafiti, tuangalie sana vyanzo vya rushwa viko maeneo gani na kusema kweli maeneo mengi ambayo yana shida ya rushwa ni yale ambayo yanatoa huduma kwa wananchi. Kwa hiyo, tufanye utafiti wa kutosha, tujue na kubaini maeneo ambayo yana mianya ya rushwa ili kabla ya kuanza kukimbizana na mla rushwa mmoja mmoja tupambane kwanza na kuziba hiyo mianya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wale wananchi wenye uzalendo ambao wanatoa taarifa sahihi zinazosaidia kupambana na vitendo vya rushwa. Najua taarifa hizi zinatolewa katika mazingira ya usiri mkubwa. Lakini ninashauri wawe motivated katika mazingira hayo hayo ya usiri ili waendelee kusaidia katika kupambana na vita ya rushwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumze kuhusu TASAF - Mpango wa Kusaidia Kaya Maskini. Mpango huu pia umeendelea vizuri na hasa kule jimboni kwangu vijiji vingi vimepata mpango huu. Lakini naomba sana katika Jimbo la Mpwapwa bado kuna vijiji 22 havijaingia katika huu Mpango wa Kusaidia Kaya Maskini.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nitoe ushauri, bado kuna malalamiko madogo madogo kwamba utaratibu mzima wa kutambua kaya maskini bado una kasoro ndogo ndogo. Wale walengwa wanaotakiwa kufaidika na mpango huu hawatambuliwi, matokeo yake unakuta kaya ambayo inapata huduma hii haina sifa ya kupata huduma hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo maana yake kuna wimbo la rushwa hapo limegubika, maana sioni mantiki ya mtu kwenda kuona kwa sababu utaratibu ni kwamba lazima maafisa wafike wakaone kaya ile ina hali gani ya kiuchumi. Sasa kama umekuta ina unafuu wa kiuchumi kwa nini uiandike katika orodha ya kaya maskini?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hilo ni jambo ambalo tunaomba Wizara iendelee kupambana nalo. Tunapenda sana watu wetu wale ambao kwa kweli wanahitaji msaada huu basi wanufaike na msaada huu, badala ya kunufaika watu wasiohusika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumze juu ya uongozi; katika bajeti ya TAMISEMI, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walichangia juu ya migogoro inayoendelea katika maeneo yetu. Unakuta DED hapatani na Mkuu wa Wilaya, hapatani na mwenyekiti wa Halmashauri. Mimi nafikiri haya yote yanatokana na ukweli kwamba wanapoteuliwa hawapewi semina ili wajue wajibu wao. Matokeo yake mtu ana-overlap mpaka kwenye kazi ya mtu mwingine halafu kunakuwa hakuna maelewano ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ule utaratibu wa semina elekezi mimi naomba urudishwe ili watu wakipata uteuzi au wakiajiriwa kwenye nafasi fulani basi apewe maelekezo namna ya kuenenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)