Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Abdullah Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mahonda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia hidaya hii nami kusema maneno machache, cha msingi ningependa kuzungumza kuhusu mambo mawili; mchango wangu hautakuwa specific, mchango wangu ningependa uwe general. Na mambo makuu mawili ningependa kuyazungumza la kwanza ni amani, la pili ni utawala bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, amani hii ambayo tunajivunia sisi na kuna baadhi ya wenzetu ambao wanatuhusudu na amani yetu haikuja kwa bahati mbaya, imelelewa, ikatunzwa na hatimaye ikastawi mpaka hapa hii leo tukawa tunajivunia. Mwanzilishi wetu Baba wa Taifa aliitunza na kuilea hii amani kwa msingi mmoja mkuu msingi huo ni msingi wa utaifa. Baba wa Taifa kwa kipindi kikubwa sana cha awamu yake ya kwanza, nguvu nyingi sana za kifikra, za kifedha, aliziwekeza katika kujenga utaifa (national unit and cohesion) na alijenga hivyo kwa kufanya yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhakikisha Serikali Kuu; pili, Serikali za Mitaa na tatu, Taasisi na Asasi za Kiserikali zina sura ya kiutaifa. Hili jambo kwa kweli hatuwezi kulichukulia wepesi wa aina yoyote, ni zito mno, tukilega hapo hii amani ambayo tunajivunia inaweza ikapeperuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Askofu Bagonza anasema; amani ni tunda la haki, na haki hii aliyoitenda Baba wa Taifa kuhakikisha kwamba taasisi zote, Serikali yenyewe ipo na sura ya kiutaifa ndio zao lake hii amani. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri naomba nikukumbushe hili somo la kihistoria na sina shaka yoyote utalichukua kwa umakini na katika uboreshaji wenu wa taasisi zote za ndani mtazingatia sura ya kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina maana gani sura ya Kitaifa? Mheshimiwa baba wa Taifa alichukia ukabila, alichukia udini na alihakikisha taasisi za Kimuungano zina sura ya Kimuungano (national cohesion). Hili ni jambo la msingi sana hili amani idumu na itamalaki kama hivi leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ningependa kuzungumzia suala la utawala bora. Tumejichagulia sisi kama nchi kuendesha nchi yetu kwa misingi ya kidemokrasia, Serikali ya watu, kwa ajili yao na inayowatumikia wao (Government of the people, by the people, for the people) huu ndio mfumo wetu. Sisi tulibahatika kuwa viongozi tunadhamana hii ya muda mfupi tu na tupo hapa kwa ajili yao, tumejiwekea misingi ya utawala bora pasiwe na uonevu wa aina yoyote, tuwe tunalinda hii misingi iwalinde watu, hii misingi ilinde mali zao na misingi hii ilinde utu wao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mantiki hiyo basi ningependa kuona sheria ambazo zimetoka nje ya mlolongo huu, nje ya mfumo wa utawala bora ziletwe na tuzirekebishe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wale...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, imefika dakika saba?

NAIBU SPIKA: Tayari ahsante sana.

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)