Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara kwa kuwasilisha Hotuba yao ili tuweze kuijadili. Yapo mambo ambayo naomba kupata ufafanuzi na kuishauri Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Maboresho ya maabara katika shule zetu. Katika Mkoa wetu wa Iringa kuna shule nyingi sana za sekondari bado maabara zake hazijaweza kuboreshwa vizuri ili kuweza kumsaidia mtoto anayesoma masomo ya sayansi. Pamoja na kutokamilika kwa majengo kwa baadhi ya shule, lakini hata vifaa vya kutumia katika maabara kwa baadhi ya shule bado havikidhi haja. Vile vile pamoja na Sera ya Serikali kupeleka umeme wa REA katika taasisi kama shule zetu za sekondari na vyuo, bado hakuna umeme. Sasa tunategemea hawa watoto wakifanya mtihani kweli watafaulu kwa mtindo huu, tutapata kweli wataalam wa sayansi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule kongwe na maboresho ya shule maalum. Katika Mkoa wetu wa Iringa tunazo zile shule kongwe za sekondari kama Shule ya Lugalo, Shule ya Tosamaganga, Shule ya Malangali, hizi shule zinahitaji ukarabati wa hali ya juu.
Ningeomba sasa Serikali itoe kipaumbele katika ukarabati wa majengo ya shule hizi tu. Shule ya Sekondari Lugalo sasa hivi ni shule maalum, inachukua watoto wanaofundishwa elimu maalum, kama watoto wenye ulemavu wa ngozi, watoto viziwi, watoto wasioona, lakini inasikitisha sana kuona shule hii hawa wenye elimu maalum hawana vifaa vya kujifunzia. Je, ni utaratibu gani unatumika ili hawa vijana waweze kupata vifaa vya Walimu wao kuwafundishia na vifaa vya kujifunzia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, maboresho ya mitaala kwa Walimu. Serikali imekuwa ikibadilisha mitaala lakini Walimu hawapati semina au elimu kwa ajili ya kuweza kuielewa hiyo mitaala ili waweze sasa kufundisha kwa watoto. Hivyo, Serikali kama inabadili mitaala iende sambamba na kuwafundisha Walimu hao hiyo mitaala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, madeni ya wazabuni. Naomba Wizara ifanye utaratibu wa kulipa madeni yote ya wazabuni. Wazabuni wanapata shida kwa muda mrefu sasa. Ningeomba Waziri anapojibu atueleze mkakati wa Serikali wa kulipa madeni ya wazabuni, yamekuwa ni ya muda mrefu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.