Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii kuchangia hoja iliyoko mbele yetu ambayo ni uwasilishaji wa hotuba ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ningependa kutolea ufafanuzi wa baadhi ya hoja ambazo zilijitokeza wakati Waheshimiwa Wabunge wanachangia katika hotuba ya Wizara yetu.

Mheshimiwa Spika, Wabunge wengi walichangia kuhusu miundombinu katika shule zetu na miongoni mwa mambo ambayo walikuwa wamechangia; moja walipendekeza kwamba kwenye hizi shule kongwe za msingi ambazo nyingi ni mbovu, walikuwa wanaomba Serikali izingatie na izifanyie ukarabati. Mpaka ninavyozungumza sasa hivi Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeshazitambua shule 722 nchi nzima, shule kongwe na shule hizi ni zile ambazo zilijengwa kabla ya uhuru na nyingine zilijengwa mara baada ya kupata uhuru. Tumekubaliana kwamba wanafanya tathmini na baada ya kumaliza tathmini tutatumia hii miradi ambayo tuko nayo; tuna Mradi wa GPE-LANES II, Mradi wa Shule Bora, Mradi wa Boost na Mradi wa EP4R kuhakikisha hizi shule zinakarabatiwa kama Bunge linavyohitaji.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kuonyesha kwamba Serikali bado inahangaika na miundombinu na kuhakikisha watoto wetu wanasoma katika mazingira bora. Mwaka huu wa fedha ambao tunakwenda kuupitisha kama Bunge lako litaidhinisha, tumedhamiria kujenga shule 300 kati ya shule 1,000 complete school na shule hizi zitajengwa katika zile kata ambazo hazina sekondari. Shule hizi zitakuwa za kidato cha kwanza mpaka cha nne, madarasa yatakuwa nane mpaka 12 na shule hizi shule moja itagharimu shule milioni 650 mpaka 700 mpaka inakamilika.

Mheshimiwa Spika, na zoezi hili ni endelevu tutalifanya Mwaka huu wa fedha, tutalifanya mwakani, tutalifanya mwaka kesho kutwa. Baada ya kukamilika kwa shule zote hizi maana yake tunatarajia kuwasaidia watoto wa masikini 400,000 kwa kujenga shule 1,000 katika safari hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile, Serikali kwenye kuhakikisha kwamba tunaboresha miundombinu na tunamsaidia mtoto wa kike, tumekubaliana kwamba tutajenga shule 26 maalumu za kimkoa na mwaka huu tunaanza shule 10 kati 26 na mwakani tutafanya 16 kuhakikisha kwamba kila mkoa unakuwa na shule ya wasichana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, shule hii ya wasichana itakua inachukua watoto 1,000 mpaka 1,200 nchi nzima, shule itakuwa complete itakuwa na kila kitu na tunajenga shule ya kisasa kweli kweli, kwasababu gharama ya shule moja hizi ni bilioni nne, ni kitu ambacho nafikiri kwa mara ya kwanza katika Serikali yetu tunafanya kitu kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, walijaribu kuzungumzia kuhusu ujenzi wa mahabara, ninafikiri kama kuna kazi kubwa Serikali imefanya ni kujenga mahabara za kisasa kwenye shule zote nchini. Na kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu Mwaka 2020, hakuna mwanafunzi hata mmoja aliyefanya mtihani wa alternative to practical, kwa hiyo, haya ni mapinduzi makubwa kabisa katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana utaona kabisa kwamba kwenye bajeti yetu tumetenga pale, mwaka huu wa fedha tunakwenda kufanya ukamilishaji wa mahabara 1,043, tunakwenda kumalizia maboma yale ambayo wananchi wameanzisha na kila boma litagharimu milioni 12.5 na mahabara moja tumepeleka kwa ajili ya kwenda kuzikamilisha milioni 30 na shule sekondari 1,841 na kwenye bajeti yetu, tumetenga bilioni 89.9 kuhakikisha zoezi hili linakamilika. kwa hiyo, tumedhimiria kabisa kuibadilisha sekta ya elimu katika ngazi ya elimu msingi ambayo tunaisimamia.

Mheshimiwa Spika, kwenye uhaba wa nyumba za walimu ni hoja ambayo hata Mheshimiwa Spika ulizungumza hapa na sisi tumeipokea kwakweli kuna changamoto kubwa. Tulikuwa tunazungumza na wataalam pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, tumekubaliana kuangalia namna bora ambayo tunaweza kuwasaidia walimu hasa walioko katika mazingira magumu kuhakikisha kwamba, sasa hii adha tunawaondolea. Kwa hiyo, tumedhamiria na tumekubaliana baada ya bajeti yetu tutakwenda kuanda mpango maalumu ili tuwasaidie walimu ambao zaidi wanakaa katika mazingira magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja ajira za walimu ni kweli kabisa kwamba bado tunachangamoto ya walimu katika maeneo mengi, lakini tukiri wazi kwamba Serikali itaendelea kuwaajiri walimu kila mwaka kulingana na mahitaji na hali alisi ya kibajeti. Kwa hiyo, hilo ni kwamba kwa sasa hivi na ndiyo mpango wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, kwamba kila mwaka tutaajiri moja kwa kufanya replacement ya wale walimu ambao wanastaafu, wanafariki, wanaacha kazi, au wanafukuzwa kwa mambo mengi yaani hatutakua tunaacha kwamba wanastaafu halafu atuajiri, sisi tumesema kila mwaka tutaajiri kwa kufuatia hivyo.

Mheshimiwa Spika, jingine bajeti na mahitaji tutaongeza namba kulingana na mahitaji yaliyopo kuhakikisha kwamba tunaongeza ajira za walimu nchini. Katika kuondoa urasimu, tumeanzisha mfumo wa ajira ya mambo ya kazi unaitwa Online teacher application system na lengo la mfumo huu, moja ni kuondoa urasimu, pili ni mfumo ambao unawapangia walimu vituo moja kwa moja yaani unakwenda pale unapo- apply unaona mpaka shule unayotaka kuchagua. Kwa hiyo, kama kuna halmashauri zimeja maana yake ule mfumo utakuwa unakuonyesha huku kumejaa Kongwa au maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunawasaidia watu wote. Tumekubaliana kwamba tutaendelea kuzingatia walimu wanaojitolea mashuleni kwa muda mrefu, tutazingatia mwaka wa masomo wa wa wale wanafunzi kwa maana walimu wanafunzi waliohitimu, kuna walimu wameitimu 2012,2013,2014, hawajaajiriwa. Kwa hiyo, tumesema sasa hivi tutakwenda kuwazingatia hao kwanza, lakini wote tunahakikisha tuna wa-accommodate katika mfumo wetu na watu wote wanapata hiyo ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye issue ya uhamisho ni moja ya ajenda ambayo ilizungumzwa sana na Wabunge, nieleze tu kweli kuna changamoto kubwa sana ya uhamisho hususani wa walimu na ndiyo moja ambayo imekua kero kubwa sana. Kwa hiyo, tumekubaliana Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Utumishi, tumeandaa mfumo unaitwa Human Capital Management Information System. Mfumo huu ni kwamba mtumishi atakuwa na uwezo wa kujiamisha online yani straight bila kuja huku chini uonge, fedha sijuwi ufanye kitu gani ndiyo upate uhamisho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na huu mfumo uko katika hatua za mwisho na sasa hivi tunachokifanya, tumemaliza kutoa mafunzo katika ngazi za halmashauri sasa tunakuja katika ngazi ya juu ili watu wote waanze ku-apply kupitia huu mfumo. Kwa hiyo, lengo moja mtumishi atahama kupitia online; lakini pili taarifa mara yule mtumishi atakapokua amedhibitishwa kuhama zitaamishwa mara moja ikiwemo na mshahara wake yaani tukimuamisha tunamuhamisha moja kwa moja. Kwa hiyo, tunaamini kwa hili tutaondoa changamoto ya watumishi kuchelewa kupata majibu yao ya kuomba utumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile, tutoe rai tumesema kabisa katika huu mfumo ni lazima tuweke masharti vile vile, moja ya sharti tukalo liweka sasa hivi tumekua tukiajiri walimu, mwalimu akishafika kwenye kituo kwa mfano amepangiwa Kasulu, akishapata check number kesho yake anataka kuhama, tumeweka condition kwamba mtumishi hatahama kituo mpaka amalize miaka tatu kwenye kituo chake cha kazi. Kwa hiyo, na mfumo uta detect hili jambo kwamba huyu mtumishi bado muda wake wa kuhama, kwa hiyo ataendelea kukaa kwa hiyo mfumo utamkataa direct, tumekubaliana tutafanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika bajeti yetu ya mwaka 2021/2022 tumetenga bilioni 50 kwa ajili ya kununua vitabu vya kujifunzia na kujifundishia kwasababu kumekua na changamoto kubwa sana na Wabunge wamezungumza, shule zetu nyingi hazina vitabu katika maeneo husika na mawili ya mwisho ni kwamba kumekua na madeni ya wastaafu ambayo yamezungumziwa. Na ninavyozungumza sasa hivi kuna baadhi ya halmashauri zimeanza kuwalipa watumishi baada ya kusikia mjadala unavyoendelea Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI, na Waziri husika tumesha pitia yale madeni tuna wastaafu walimu 2,822 ambao wanadai Serikali bilioni 3.9 kwa hiyo tunamalizia hatua za mwisho ili kuhakikisha watumishi wote waliofanya kazi kwa Amani kulitumikia Taifa letu nawenyewe wote wanalipwa kuhakikisha kwamba hatuendelei kuwasumbua kama ambavyo imekua ikitokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho mwaka huu Serikali inatarajia kupandisha madaraja, watumishi zaidi ya 90,000 nchi nzima, lakini kwenye hao watumishi wako na walimu kuna fifty-three, percent asilimia 53 ya hao watumishi ni walimu, kwa hiyo tuseme tu jamani Serikali imesikia mambo ya Wabunge, Serikali inafanya kazi, Serikali inajiamini kwa kitu ambacho tunajipanga na sisi tunawaomba Waheshimiwa Wabunge mtupitishie hii bajeti yetu ili twende tukatekeleze tumejipanga na tuko tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru naunga mkono moja ahsante. (Makofi)