Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii. Awali ya yote, nampongeza sana Waziri Mheshimiwa Ummy pamoja na timu yake siyo tu kwa kuwasilisha bajeti yao vizuri sana, maana yake kwa kweli wamewasilisha vizuri, lakini pia hata kwa kazi ambazo tumeshawaona wakizifanya ndani ya muda mfupi toka wameingia kwenye nafasi hizo, nikiwatazama hawa naona matumaini kama ninavyoitazama timu yangu ya Simba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naungana na wote waliozungumza juu ya kuongezea nguvu TARURA, suala la dawa kwenye Hospitali zetu, watumishi mbalimbali na kuwaongezea uwezo pia Madiwani wetu, hayo yote nayaunga mkono kwa asillimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikija kwenye Jimbo langu la Mwanga, naomba kusema kwamba ipo ahadi ya Hospitali ya Wilaya iliyotolewa na Mheshimiwa Rais wakati wa Kampeni. Kama alivyosema Mheshimiwa Rais, Mama Samia, yeye na Mheshimiwa Hayati Dkt. Magufuli ni kitu kimoja, kwa hiyo, kwa vile Mheshimiwa Dkt. Magufuli alitoa hiyo ahadi, basi ahadi hii ni ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na tunaiomba itekelezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Mwanga walirukaruka sana baada ya kupewa ahadi hiyo kwa sababu ilikuwa ni kilio cha muda mrefu, wakaibana Halmashauri yao, ikatenga ekari 54 za ardhi ambazo zipo tayari kwa ajili ya mradi huo. Namkaribisha Mheshimiwa Waziri pamoja na Manaibu watuletee huo mradi.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili juu ya sekta ya afya, ni Kituo cha Afya cha Kigonigoni ambacho ni moja kati ya vituo vya mkakati. Serikali ilileta kwanza shilingi milioni 400 kikajengwa kikafikia hatua iliyofikiwa, lakini tangu hapo kimesimama. Yale majengo na vitu vingine vyote vilivyojengwa vinazidi kuharibika. Tusipomalizia kile kituo cha afya tutazidi kupata hasara na wananchi wa Kata ya Kigonigoni na maeneo yote ya ile Tarafa ya Jipendea watateseka kwa sababu walikuwa na matumaini makubwa ya kituo hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo mawili ya Jimbo langu la Mwanga, yapo mengi, lakini mengine ninaamini Mheshimiwa Waziri na timu yake watakuja kuyaona na mengine tutazungumza, nizungumze moja tu la Kitaifa. Nina imani kabisa hili suala la matumizi ya force account yanaweza yakatupeleka mbali, lakini tukitaka mafanikio makubwa kwenye suala hili ni vizuri basi Halmashauri zetu zikawa na jopo zima linalohusika na ujenzi. Lazima Halmashauri ziwe na ma-architect, ma-quantity surveyors na ma-engineer. Bila hivyo miradi hii itakuja kutupa shida baadaye.

Mheshimiwa Spika, tungependa majengo haya yanayojengwa wajukuu zetu wayakute, lakini kwa mfumo huu wa kumwachia engineer peke yake au pengine hata engineer hakuna, asimamie mradi ya shilingi bilioni moja, kwa kweli hatuwezi kufika vizuri. Wataalam wa ujenzi walitengeneza mfumo wa jopo linaloweza kusimamia kazi ya ujenzi hata mikataba ambayo inatumika kwa nchi nzima; mikataba ya FIDIC na NCC yote inazingatia kwamba lazima kuwe na jopo la hao wataalam ili kazi iende vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati tunasubiri kupata wataalam hao, Serikali inaweza kuamua kutumia bodi mbalimbali za wataalam wa hizi fani kama CRB, AQRB, ERB hizo zote zinaweza zikaratibu kwa kutumia wataalam waliopo kwenye zone mbalimbali ili kuhakikisha miradi hii inasimamiwa vizuri ili tuweze kupata value for money.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, Wizara hii ni moyo wa maendeleo, yapo mengi ambayo tunaweza tukasema, lakini kwa timu hii ambayo Serikali imetupatia, tunaamini watakuja huko kuyaona ili tuweze kufanya mambo.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Nakushukuru sana. (Makofi)