Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi kwasababu ya dakika chache nitakwenda moja kwa moja Jimboni na kabla sijakwenda huko kama Wabunge wengine walivyozungumzia kuhusu TARURA naomba kushauri mambo machache.

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba wahandisi waliochukuliwa kutoka kwenye Halmashauri sasahivi wako kwenye vyeo vya muundo wa TARURA. Kuna wengine ambao bado hawajaanza kulipwa kulingana na mamlaka waliyonayo. Sasa tusiweke hizo habari za mamlaka kana show. Kama tumeamua kusema kwamba huyu ni Meneja wa TARURA ngazi ya Halmashauri, alipwe kulingana na nafasi aliyonayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natambua kwamba kwenye ngazi ya mkoa tuna mratibu wa TARURA Mkoa. Yule mtu kuwa peke yake pale kunakuwa na changamoto kadhaa kwa sababu akiwepo pale peke yake yeye ndiyo anayehusika na manunuzi. Huyo huyo mratibu peke yake ndiyo anayehusika na kutangaza tender. Kumekuwa na changamoto kwa hawa wakandarasi na changamoto hizo zinaenda kuathiri wananchi moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nashauri, ni vizuri tukaangalia muundo wa TARURA upya ili kuweza kutimiza malengo ambayo tulikusudia baada ya kuanzisha chombo hiki.

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia maeneo machache, kuna barabara ya Kirando – Korongo na leo nimekushuhudia Mheshimiwa Naibu Waziri ukiwa unajibu hilo swali ambalo kuna daraja la Kavune. Nitambue mchango wa Serikali kwenye jambo hili kwamba wamepeleka fedha kiasi kwa ajili ya ujenzi wa hili daraja lakini uhitaji wa daraja hili na hiyo barabara kwenye lile eneo ni muhimu sana.

Niwaombe TAMISEMI kuna mambo ambayo hayahitaji kufanya siasa, kuna maeneo tunayotoka pembezoni. Tukileta siasa kwenye afya, tukaleta siasa kwenye elimu, tukaleta siasa kwenye miundombinu tutawaumiza wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninasema hivyo kwasababu leo tuna Sera ya Afya ambayo inataka zahanati kwa kila Kijiji, inataka kituo cha afya kwa kila Kata. Wilaya yangu ya Nkasi ina Kata 28, kata zenye vituo vya afya ni kata tatu tu. Tukianza kuzungumzia habari ya Ilani miaka yote walikuwa Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi, kwanini mlishindwa kutekeleza jambo hili. Kwasabbau hiyo, nataka nishauri tu kwa nia njema, basi hizo kata tatu zenye vituo vya afya basi zitoe huduma kulingana na level ya Kata kwa maana ya kituo cha afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukija kwa wauguzi bado kuna changamoto, pamoja na kwamba hatujatimiza, hiyo sera haijatekelezeka lakini katika hizo chache tulizonazo basi angalau tupeke huduma zinazoweza kujitosheleza kuwasaidia wananchi wetu. Natambua kwamba wananchi wamehamasika kuweza kuanzisha maboma mbalimbali kwa ajili ya zahanati na vituo vya afya, ni vizuri! Pamoja na kwamba uhitaji ni mkubwa, fedha mnayopata TAMISEMI ni ndogo. Lazima tuwe na kiipaumbele, na kipaumbele ni kuanza kuheshimu nguvu za wananchi ambazo wanakuwa wamezianzisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kata ya Kabwe, Waziri Mkuu amekwenda pale akaahidi kwamba kituo cha afya kitafunguliwa mapema kwasababu ya bandari iliyoanzishwa kule. Mpaka leo ninavyozungumza hakuna fedha yoyote tumeona baada ya tamko lile na haya matamko sio mabaya lakini yamekuwa yanaathiri mambo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naweza nikarudi tu hapo kwenye masuala ya TARURA, unakuta kuna matamko au maagizo au ahadi za viongozi wa Kitaifa. Ahadi sio mbaya lakini ahadi hizo zinavyokuja zinatekelezwa kwa kiasi gani ahadi za viongozi wa Kitaifa na wakati mwingine zinakwenda kuharibu bajeti za halmashauri, kwa hiyo inakuwa ni ugomvi kati ya wananchi pamoja na viongozi waliopo kwenye kada hizo. Kwa hiyo, ni vizuri hata hizo ahadi zikawa kwenye kumbukumbu maalum. Tunapokuwa tunaandaa bajeti tunakuwa tunajua kuna ahadi ngapi za viongozi wa Kitaifa ili utekelezaji unakuwa unaeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo jingine naomba nizungumzie kwenye elimu. Pamoja na kwamba elimu inatolewa Tanzania nzima kuna maeneo ambayo yanahitaji mkakati za ziada, hasa sisi ambao tunatoka pembezoni. Mpaka hivi ninavyozungumza kwenye Wilaya ya Nkasi kuna kata nne ambazo watoto ili wakafanye mtihani wanatakiwa wapite kwenye maji, yaani wavuke maji wakafanye mtihani sehemu nyingine. Leo unazungumziaje matokeo chanya kwa watoto hawa? Anavyopita kwenye maji akafanye mtihani kwanza tumem-disturb, arudi tena nyumbani, kesho tena aende apande boti, maboti yenyewe hayapo, Serikali hamjapeleka boti. Lakini na sisi tunataka Marais watoke kwetu yaani mnaamini kwamba Nkasi Rais hawezi kutoka? Lakini kama tunaamini hivyo, lazima tutengeneze mazingira rafiki kwa watu hawa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, wanapozungumzia watu wengine kwamba kuna wengine wamekufa kwa kung’atwa na fisi, Wilaya ya Nkasi watoto wanang’atwa na mamba isivyo kawaida! Leo ni kosa la nani? Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha watoto wanatengenezewa mazingira rafiki kwa ajili ya kupata elimu kwasababu elimu sio fadhila, elimu ni wajibu wa Serikali iliyopo madarakani kutoa elimu kwa watu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika,…

SPIKA: Mheshimiwa Aida, unga mkono hoja. (Kicheko)

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Ahsante. (Kicheko/Makofi)