Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuweza kuchangia. Kwanza kabisa nianze kwa kuishukuru na kuipongeza Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi kwa mambo ambayo waliweza kutufanyia katika Jimbo la Momba katika Awamu ya Tano, na mambo ambayo wanaendelea kutufanyia katika Awamu hii ya Sita; tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kumpongeza dada yangu, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, kwamba tuna imani sana na wewe kwenye Wizara husika ambayo umepewa kuisimamia, lakini pia kuendelea kuwapongeza kaka zangu, Manaibu hodari sana ambao wanamsaidia dada yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mbele ya Bunge lako Tukufu, naomba niwasilishe baadhi ya changamoto za wananchi wa Jimbo la Momba kama ifuatavyo. Nitaongelea kwenye miundombinu ya barabara pamoja na madaraja; miundombinu ya elimu; miundombinu ya vituo vya afya pamoja na zahanati na muda ukiwa Rafiki nitamalizia na namna gani kuendelea kuwawezesha akinamama wa vijijini katika ubunifu wao mbalimbali walionao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Momba ndilo jimbo ambalo tuseme kwa Mkoa wetu wa Songwe linaongoza kwa kiasi kikubwa sana kulima mpunga, maharage pamoja na mahindi. Na tunaweza kusema ndilo jimbo ambalo linalisha Mkoa mzima wa Songwe kwa mbegu, au tuseme kwa zao la mchele. Lakini pamoja na nchi ambazo ni Jirani kama Kongo na Zambia, wanategemea sana mchele pamoja na maharage kutoka kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa basi, kutokana na mambo ambayo Waheshimiwa wenzangu ambao wametangulia kueleza hapa. Ufinyu mkubwa uliopo kwenye bajeti ya TARURA ni wazi kwamba hata nitakapoeleza changamoto nyingi ambazo zinalipata Jimbo la Momba sitaweza kumaliza. Kiukweli Jimbo la Momba ni miongoni mwa majimbo ambayo yana changamoto kubwa sana ya miundombinu ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata sasa ambavyo ninaongea hapa ni kweli ziko kata ambazo ziko pia visiwani, zimebaki kwasababu hakuna madaraja, barabara siyo rafiki, hawawezi wakatoka kwenda kijiji kingine, hawaweze wakatoka kwenda kata nyingine, wanaendelea kusubiri mpaka mvua zitakapokauka ndipo waendelee kupitia kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Hali hiyo imeendelea kusababisha kudorora sana kwa mapato ya halmashauri yetu, pamoja na kwamba jimbo linaendelea kuhudumia na nchi nyingine ambazo zipo mpakani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali; kwa kuwa network ya barabara ambazo ziko ndani ya Jimbo la Momba ni barabara 57 zenye urefu wa kilometa 647.21, ninajua kwa ufinyu wa TARURA barabara hizi haziwezi kutekelezeka. Niende kwenye uhalisia; tunaomba tuombe barabara chache za kimkakati ambazo kuwepo kwa barabara hizi Serikali itakapotuwezesha, kunaweza kukachangia kwamba halmashauri ikaongeza mapato yake, lakini pia ikavutia maana zitakuwa ni barabara za kimkakati. Lakini pia inaweza ikafanya hata wafanyakazi ambao wanafanya kazi katika maeneo hayo, yakawavutia kuendelea kubaki hapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kwanza ambayo nianze kuiombea ni barabara ya Makamba – Ikana. Na barabara hii sababu ya kuiombea barabara hii ni kwamba ndiyo barabara ambayo inaunganisha Jimbo la Momba kwa ukanda wa juu na wa chini na soko la kimataifa la mifugo na mazao limejengwa katika Tarafa ya Ndalambo ambalo tunalitegemea sana katika kupandisha mapato ya halmashauri na kuliongezea Taifa mapato yake kwa kuwa tutaendelea kusambaza kwa wingi na kwa ubora kwenye nchi zetu ambazo ziko Jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii tutakapokuwa tumeipata barabara hii, itakuwa imerahisisha Tarafa za Msangana na Kamsamba ambazo zina jumla ya kata nane, kwa hiyo watapandisha mazao yao kwa urahisi kwa ajili ya kwenda kufika kwenye soko la mifugo na mazao ambalo lipo Kakozi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine ninayoiomba ni barabara ya Chindi – Msangano ambapo kuwepo hapo kuna daraja kubwa ambalo limetenganisha Halmashauri ya Wilaya ya Momba pamoja na Halmashauri ya Mji wa Tunduma. Kwa hiyo kama barabara hii itafunguka, na tutakapopata daraja katika eneo hilo, itatusaidia sana wananchi kuendelea kuwa na options mbalimbali kwa ajili ya kupeleka mazao mengine au na shughuli nyingine za kiuchumi kwenye Mji wa Tunduma ambao tunautegemea kama mji ambao uko mjini kwa ajili ya kuendelea kupata mahitaji mbalimbali, ikiwa na hospitali ya wilaya iko kwenye Mji wa Tunduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine ninayoiombea ni barabara ya Ivuna – Chole. Barabara hii inaunganisha Halmashauri ya Wilaya ya Momba pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Songwe. Na wananchi ambao wapo katika Kata ya Mkomba wanatenganishwa na daraja kubwa. Mwenyewe kipindi cha mvua nikienda kufanya ziara ni lazima nibebwe mgongoni kwasababu baiskeli haiwezi kupita, pikipiki haiwezi kupita, gari haliwezi kupita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini barabara nyingine ambayo naomba ushughulikiwe ni barabara ya Kakozi – Ilonga. Barabara hii ndiyo ambayo inaunganisha Mkoa wa Songwe pamoja na Mkoa wa Rukwa. Barabara hii pia Mheshimiwa baba yangu Mheshimiwa Kandege naye ninajua itamsaidia sana kuja kutumia lile soko la mifugo na mazao kwa sababu ataleta mazao yake pale. Vilevile barabara hiyo ndiyo ambayo inapita mpaka kufika kwenye Bandari ya Kalemii.

Kwa hiyo, itasaidia wananchi wa Jimbo la Momba na Majimbo mengine ambayo yapo kwenye Mkoa wa Songwe na kwenye Halmashauri zingine wanaweza wakaitumia kwa ajili ya kufikisha mazao yao au vitu vyovyote kwenye bandari hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe ushauri kidogo kwa Serikali namna gani inaweza ikatusaidia kuongeza pato kidogo kwa TARURA. Nitolee mfano wa wananchi wangu wa Jimbo la Momba. Wananchi wa Jimbo la Momba kwa asilimia ni wachache sana ambao wana simu za smartphone, kwa hiyo, mtu anaponunua kifurushi anapewa dakika za maongezi, SMS za ku-chat pamoja na MB lakini kwa sababu ni watu wa kupiga tu hata ku-chat kwa SMS za kawaida hawa-chat, inapofikia kile kifurushi kina-expire anakuwa ametumia dakika lakini MB pamoja na SMS zinakuwa zimebaki lakini mtu yule anakuwa ameshalipia na kodi ya Serikali amekatwa kwenye ule muda wa maongezi. Mnaonaje kama TAMISEMI wataamua kwamba kile ambacho kinakuwa kimebaki kwa sababu ni cha mwananchi na alikilipia kwa pesa yake halali akatolea na kodi kwa nini isirudi ili ije kwa ajili ya kusaidia vitu kama hivi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata kwa Waheshimiwa Wabunge tuna experience kitu hiki, umenunua dakika, SMS na MB unatumia kidogo vinabaki vinaenda wapi? Kwa hiyo, tunayafaidisha makampuni ya simu ambayo yameshatuchaji na tunawaachia bure, hivi viki-expire tuwekeane mwongozo vinarudi kwa Serikali kwa sababu itakuwa ni changizo halali la mwananchi huyu. Kwa hiyo, mimi naona inaweza kutusaidia kukusanya na kuboresha barabara na katika hilo dada yangu Mheshimiwa Ummy mtukumbuke huko Momba, ahsante sana. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kwenye miundombinu ya elimu, kutokana na Jimbo la Momba kuwa na changamoto nyingi za barabara imepelekea mazingira ya walimu wengi ambao wanafanya kazi ndani ya Jimbo la Momba yanakuwa si Rafiki. Walimu hawa kuna wakati wanakuwa wananung’unika, hawana motisha ya kufanya kazi vizuri. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)