Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Kwanza naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pili kwa sababu leo nimesimama naomba nitoe pole zangu kwa Watanzania wote kwa kumpoteza Rais wetu mpendwa, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpe pongezi mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kushika kijiti cha kuliongoza Taifa letu la Tanzania. Sisi kama Watanzania, kama wanawake kwa ujumla tuko naye bega kwa bega kumuunga mkono Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo niwape pole wananchi wangu wa Mchinga, hasa wale wa Kata ya Milola ambao wamekumbwa na kadhia ya tembo na mtu mmoja amefariki kwa kukanyagwa na tembo usiku wa jana kuamkia leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nianze kwa kuzungumzia suala la TARURA. Karibu Wabunge wote wa Bunge lako Tukufu waliosimama hapa walikuwa wanazungumzia suala la TARURA, pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri wetu na watendaji wake wameeleza vizuri sana na wao wameshika hiki kijiti vizuri sana na wao wameshika hiki kijiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara baada ya Mheshimiwa wetu wa Awamu ya Sita kumuona dada yetu, mama yetu, mwanetu wetu, kwamba hapa anayefaa si mwingine bali ni Ummy Mwalimu. Naamini na najua Ummy ni mchapakazi mzuri, ni hodari na ni mfuatiliaji, ukimwomba jambo hakuna anapokuachia. Ninachopenda kusema tu TARURA inabidi iongezewe pesa. TARURA ndio kila kitu, asilimia kubwa ya wananchi wanaishi huko vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni lazima tutengeneze aidha azimio kama tulivyotengeneza wakati ule kwenye eneo la maji ili tumtue mama ndoo kichwani. Tukachukua pesa kutoka eneo fulani tukasema hizi ziingizwe kwenye eneo hili ili wananchi tuwatue ndoo kichwani. Kwa hiyo ushauri wangu ili tufanikiwe kwenye hili, tunabidi tuweke hilo azimio kwamba tunataka TARURA iongezewe pesa kwa uchache hata iwe asilimia arobaini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kwenye Jimbo langu la Mchinga; Ukizunguka jimbo zima hakuna hata kipande cha sentimita moja chenye barabara ya lami. Sasa kwa misingi hii sio rahisi, halafu Jimbo lile yaani ukitoka kata moja kuelekea kata nyingine lazima upitie jimbo lingine ndipo uweze kufika. Sasa ushauri wangu na ninachoomba kwa Mheshimiwa Waziri, tuunganishiwe zile barabara zetu na TARURA, lakini kama TARURA hawajaongezewa pesa sio rahisi, siku zote zitakuwa ni barabara ambazo hazipitiki na haziunganishi hilo Jimbo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kutoka Nangalu kwenda Milola huwezi kufika kutoka Mipingo kwenda Namapwiha huwezi kufika kutoka Moka kwenda Mtumbukile ni tatizo. Naona yanakufurahisha, hayo ndio majina ya Mchinga. Kwa hiyo kule kuna changamoto kubwa zisizomithirika. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nataka nizungumze mradi wa EP4R. Tunaishukuru sana Serikali waliweza kutupatia hizo pesa na hata 2017/2018 walitupatia hizo pesa na walijenga mabweni mawili pamoja na vyoo, lakini mabweni yale hayajakamilika. Kuna bweni la wasichana na bweni la wavulana kwenye Shule ya Kitomanga hayajakamilika, tunaomba Mheshimiwa Waziri atuangalie kwa jicho la huruma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kibaya zaidi kama Mheshimiwa Waziri anavyojua matatizo ndani ya Mkoa wetu wa Lindi na Jimbo letu la Mchinga, wanafunzi wanasoma pale wanatoka maeneo zaidi ya kilomita 10. Hivi juzi wanafunzi wameambiwa wabaki nyumbani kwa sababu walihamia kwenye majengo ambayo yaliachwa na Wachina wakati wanajenga. Kikubwa zaidi hata Mwalimu Mkuu wa Shule ile anakaa kwenye nyumba hizo hizo ambazo zimeachwa na hao Wachina.

Mheshimwa Naibu Spika, sasa wakaguzi walipokuja wakasema nyinyi hamjajisajili kama bweni, kwa hiyo rudini nyumbani. Sasa naomba hilo nalo walitazame kwa jicho la huruma ili watoto wale waje wasome pale kwa muda, hatimaye wakitumalizia hayo mabweni, tutafanya jitihada nyingine na zilizokuwa bora zaidi sio kwamba walikaa pale kwa kupenda bali ni kwa matatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nataka nizungumzie suala la vyombo mbalimbali ambavyo Mwalimu anaitika; vyombo hivi ni vingi kuna TAMISEMI, Wizara ya Elimu, TSC - Tume ya Utumishi wa Walimu na sasa kuna chombo kingine kinachokuja kinaitwa Bodi ya Kitaalam ya Mwalimu. Sasa hivi vyombo ni vingi, Walimu wenzangu wameniagiza kwa sababu mimi kwa taaluma ni Mwalimu, wanachohitaji hapa wabaki na chombo hiki kimoja wabaki ambacho ni TSC na sio Bodi ya Kitaaluma ya Mwalimu. Wanahitaji hivyo kwa sababu TSC inahudumiwa na Serikali, lakini hiki chombo kikishaundwa na Serikali anatakiwa Mwalimu huyu mwenyewe akiendeshe na ni ngumu sana ukizingatia hata hali yenyewe ya Mwalimu nayo ni mtihani kwake. Tunaomba waliangalie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nataka nizungumzie Walimu kutopandishwa madaraja kwa wakati na kutorekebishiwa mishahara yao kwa wakati. Naomba hili jambo waliangalie kwa utete wake ili Walimu wapandishwe madaraja yao kwa wakati na warekebeshiwe. Kwa mfano, kuna Walimu wa 2014/2015, hawa hawa hawajapanda kabisa madaraja na hata wale wa mwisho kupanda madaraja 2014 imekuwa mwisho. Naomba Serikali waliangalie hilo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa kwa unyenyekevu wake mkubwa utupe jibu sahihi kuhusu TSC na atupe jibu sahihi kuhusu hiyo Bodi kwani hawaitaki kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, nikushukuru sana kwa kunipa fursa, nitasubiri Wizara nyingine ili niweze kuchangia hoja zangu Ahsante sana. (Makofi)