Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi kwa siku hii ya leo kuweza kuchangia bajeti yetu ya TAMISEMI. Naomba nimshukuru sana Mungu ambaye ametupa uzima na uhai hatimaye tuko leo hapa tukiendelea kutetea wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri Ummy kwa kazi kubwa, tunamjua, tunamfahamu alifanya kazi kubwa akiwa Wizara ya Afya, ni mwanamke ambaye ni shujaa, ni Hodari; tunajua kabisa kutokana na jitihada zake, hii wizara ataiweza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi wamezungumzia kuhusu suala la TARURA. Kwangu kuna maeneo, kata nyingine sasa hivi wako kisiwani kabisa. Madaraja yote yamechukuliwa na maji, barabara zote zimehama, maana sijui niseme nini? Sina hata la kusema, maana tunaonekana kama vile hatufanyi kazi kabisa. Hii ni kutokana na uwezo wa TARURA. Maana yake hata TARURA wa wilaya na wa mkoa wanashindwa hata kujitokeza kwa sababu hawana fedha ya kwenda kurekebisha mambo mbalimbali ambayo yanatokea katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa sababu Wabunge wengi wamezungumzia TARURA tunaomba kwa unyenyekevu mkubwa sana, Serikali iongeze fedha kwa TARURA kwa sababu maendeleo yote yanatokea ndani ya vijiji vyetu. Vijiji vyetu sasa hivi wamelima, lakini maeneo ya kupitishia mazao yao hakuna, siyo barabara wala madaraja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi nikikwambia, madaraja sijui mangapi huko yamekatika, wananchi Kata hii na hii hawaonani, kijiji hiki na hiki hawawasiliani, ni shida. Naomba kwa unyenyekevu mkubwa sana, TARURA iongezewe fedha ili waweze kutekeleza hii miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi barabara miaka miwili sasa hazijatengenezwa. Sasa mvua ya mwaka juzi, 2019, mvua ya mwaka jana, 2020 na inayoendelea, basi mambo yamezidi kuharibika zaidi. Serikali tunajua ni sikivu, lakini kwa TARURA safari hii tunaomba muipe kipaumbele cha kwanza. Kipaumbele cha kwanza ni TARURA ili njia zetu ziweze kupitika. Kata yangu ya Itenka ambayo ni kata ya uchumi sasa hivi wako kisiwani. Ninaomba sana tusaidiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niingie kwenye upande wa Watendaji. Tuna vijiji na kuna maendeleo mbalimbali ambayo tunapeleka ndani ya vijiji vyetu, lakini hatuna watendaji. Utamkuta Mtendaji Kata ndani ya vijiji sita au saba ana Watendaji wa Vijiji wawili au watatu. Unakuta vijiji vine au vitano hakuna watendaji, wanachukuliwa walimu ndio wanakuwa mbadala wa watendaji. Wabunge wengi wamesema kuhusu watendaji, tunaomba mtuongezee Watendaji wa Vijiji, hatuna kabisa katika maeneo yetu ambapo ndiko kunapelekwa miradi mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta wakati mwingine Mwenyekiti wa Kijiji hana msaidizi, inabidi aombe msaada kwa mwalimu akaenaye kwa ajili ya miradi mbalimbali ambayo inayofanyika katika eneo la kijiji husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile utamkuta huyo Mwenyekiti wa Kijiji hana posho, hana mshahara, wanapewa fedha nyingi za miradi, lakini yeye mwenyewe; Mwenyekiti wa Kijiji au Kitongoji hana mshahara. Nilikuwa naiomba sana Serikali, kwa sababu miradi mingi inakwenda vijijini na hao Wenyeviti wa Vijiji ndio utakuta wakati mwingine yeye mwenyewe ndio Mwenyekiti wa Kijiji, yeye ndio mtendaji, hana posho wala kitu chochote.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali, tuwaangalie Wenyeviti wa Vijiji ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi wapatiwe posho. Wengi wamezungumza kwamba wengine wanachukua rushwa kwa sababu hawana posho. Tukiwatazama kwa umakini zaidi na tukawapelekea posho, wanaweza kufanya kazi kwa umakini Zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile naomba niungane na Wabunge wenzangu kuhusu Madiwani. Madiwani wanafanya kazi nzuri sana na utamkuta Diwani ana vijiji 16 au vijiji 10, lakini umbali wa kutoka kijiji kwenda kijiji posho yake ni ndogo. Tunaomba Madiwani waongezewe posho ili ufanisi uweze kuwa mzuri, waweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Halmashauri zetu magari hakuna. Miradi mingi inaenda katika Halmashauri zetu, lakini kutokana na uhaba wa magari kwa ajili ya kuzungukia kukagua miradi, Mkurugenzi pamoja na watendaji hawana usafiri. Tunaiomba Wizara iangalie upya kuwapa Halmashauri zetu vitendea kazi kwa ajili ya kukagua miradi mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri mnaona sasa hivi fedha nyingi tunapeleka kwa kutumia force account. Sasa force account, tunapeleka fedha huko, lakini kama mtendaji mkuu hana usafiri kwenda kuangalia kwa umakini ujenzi wa shule na madarasa itakuwa ni shida. Fedha nyingi zinapotea na miradi mingi inajengwa chini ya kiwango. Naomba sana magari kwenye Halmashauri zetu yapelekwe ili ufanisi wa kazi uweze kuwa mzuri na miradi mbalimbali ifanyike kwa ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wameongea kuhusu uboreshaji wa bima. Mfuko wa Afya wa Jamii ni shida. Kwenye zahanati zetu, vituo vya afya hakuna vifaa tiba, hakuna dawa, mgonjwa akienda pale anaambiwa kipimo hakuna, hakuna dawa, sasa ni shida. Jamani tunaomba tujitahidi kwa hili. Kwa sababu tunaenda kuwaambia watoe shilingi 30,000; tulianzia shilingi 10,000 tukawaambia mtoe shilingi 30,000 kwa sababu bima hii imeboreshwa; utatoka ndani ya zahanati, utaenda kwenye kituo cha afya, utaenda wilayani, utaenda mkoani, lakini matokeo yake anakwenda kote kule, hapewi huduma ambayo inastahiki. Naiomba Serikali iangalie upya uboreshaji wa hii Bima upya kwa sababu nayo inaleta shida kwa ajili ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Jimbo langu la Nsimbo, naomba niishukuru Serikali imenijengea Hospitali ya Wilaya ingawa haijakamilika. Ila kuna kata ziko mbali kama Kata ya Ugala. Kutoka Kata ya Ugala mpaka ufike kwenye Makao Makuu ya Wilaya au kwenye Makao Makuu ya Kituo cha Afya, wanatembea kilometa 80. Mtu anatoka kwenye zahanati kwenda kwenye kituo cha afya, anatembea porini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Kata ya Ugala nijengewe kituo cha afya kwa sababu watu wanatembea umbali mrefu, watu wanakufa. Acha Kata ya Ugala, kuna Kata nyingine ya Stalike. Kutoka Stalike mpaka uikute Hospitali ya Makao Makuu ya Wilaya ni kilometa 50. Naiomba Serikali iangalie haya maeneo yenye mazingira magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Itenka kama sasa hivi wako kisiwani, wana zahanati ndogo ambayo haina huduma nzuri. Naomba Kata ya Itenka nayo ijengewe kituo cha afya ili sasa kuweza kupunguza yale matatizo. Hata kama watu wako kisiwani, basi wawe na huduma bora, safi na salama katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)