Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuwa mzungumzaji wa kwanza jioni hii. Kwanza nishukuru Wizara chini ya Mheshimiwa Waziri na Manaibu wake na Makatibu Wakuu kwa sababu tunawafahamu record yao ya uchapakazi, tunaamini watakwenda kufanyia kazi changamoto zote ambazo ziko pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo machache. La kwanza iko changamoto kwenye Halmashauri zetu, pesa hazitoshi, ikifika karibu na mwisho wa mwaka tunaambiwa pesa zimerudishwa, shida ni nini wakati mahitaji yapo na miradi bado haijakamilika? Tunamuomba Mheshimiwa Waziri atusaidie jambo hili lisijitokeze. Kama changamoto ni fedha zinachelewa kupelekwa, basi angalau ziweze kutumwa katika muda muafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, tunayo changamoto ya miradi ambayo haiishi. Akipita huko kwa navyofahamu uchapakazi wa dada yetu atapata nafasi ya kufanya survey kutazama miradi gani ilianza lini na kwa nini haijakamilika. Mimi nimefanya ziara kule kwangu kuna miradi mingine ina miaka mpaka 10 haijakamilika, hii si sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kuzungumzia ni la kupima ardhi, wananchi wanahitaji sana wapimiwe ardhi yao. Kwanza inaondoa migogoro, pili ni chanzo cha mapato cha uhakika cha Serikali yetu. Napenda Mheshimiwa Waziri anapokuja hapa kwa ajili ya kuhitimisha atuambie mpango wa Wizara suala hili wanalianzaje na pengine watalikamilisha lini.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini eneo lingine ni changamoto ya ofisi zetu za Wakuu wa Wilaya. Katika mwongozo wa kuandaa bajeti tunaambiwa agenda namba moja ni suala la ulinzi na usalama. Hata hivyo, ukitazama Ofisi za Wakuu wa Wilaya kirasilimali zina changamoto kubwa sana. Mimi nashauri kwa kuwa ofisi za Wakuu wa Wilaya ndiyo wasimamizi wa Halmashauri Mheshimiwa Waziri atazame kama inawezekana asilimia sehemu ya mapato ya ndani iwe allocated kwa ajili ya kuendesha ofisi za Wakuu wa Wilaya kwa ajili ya mafuta na vitu vingine vidogo vidogo, tutawasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, agenda nyingine ambayo imezungumzwa na watu wengi hapa ni TARURA, ni changamoto kubwa sana. Suala hili naomba Mheshimiwa Waziri alichukue kwa namna tofauti. Barabara zikiwa mbovu zina uhusiano wa moja kwa moja na mapato hafifu ya Halmashauri. Barabara zikiwa mbovu zinaharibu magari ya Halmashauri, sasa kumbe kwa kuwa TARURA imewekwa ndani ya TAMISEMI, kama Serikali Kuu haiwezi kuongeza fedha basi ni vema ikatoka circular kwamba asilimia fulani ya mapato ya Halmashauri iende ikasaidie TARURA, Wakurugenzi wapewe na CAG anapokagua atazame, je, to what extent jambo hili limefanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo maalum kule kwangu, tunazo changamoto kwenye baadhi ya maeneo; mambo kama mawili hivi. Moja, Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anajibu au itakavyompendeza, naomba atusaidie vituo vya afya kwenye maeneo ambayo ni yako very critical. Mfano, tunayo Kata ya Mtwango ambayo waliojiandikisha kupiga kura ni zaidi ya 17,000, kumbuka Jimbo langu ni la vijijini lakini pale hakuna hata kituo cha afya na pembeni yake kuna kata zingine zaidi ya tatu, ikiwezekana na ikimpendeza atupatie vituo vya afya maeneo ya Mtwango, Idete na Itandula. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vivyo hivyo kwenye upande wa ambulance, tunazo changamoto kubwa sana kuanzia eneo hilo lakini eneo lingine ni ukanda wa Mgololo ambako kuna kata karibia tatu na kuna kituo cha afya kimoja. Eneo lile hata nikikutumia picha hapa barabara ni mbovu, kuna kiwanda kikubwa cha karatasi kule kina wananchi zaidi ya 40,000 kwenye eneo lile, kuwatoa wagonjwa kule mpaka makao makuu ni changamoto kubwa mno, wakipata gari ya wagonjwa tutakuwa tumewasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo naomba kuchangia ni issue ya Taasisi zinazo-operate katika nchi yetu. Kwanza, nchi nyingi kama ni International NGO inakwenda kwenye nchi husika cha kwanza unapewa condition lazima ushirikiane na NGO au Institution iliyopo pale ndani. Kwanza hiyo ina ensure security kuwa monitor wale watu wakifika hapa wanafanya nini. Hapa kwetu kuna changamoto kidogo, nimuombe Mheshimiwa Waziri aweke mkakati mzuri zaidi, kama ni USAID au whatever wakifika washirikiane na taasisi za hapa kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kutumia mfano mmoja, ni declare interest mimi ni Rais wa Red Cross, taasisi ya Kitanzania na inafanya kazi ya Watanzania, imeanzishwa kwa sheria ya Bunge na ikitaka kufutwa itafutwa Bungeni. Hata hivyo, kuna changamoto, kuna programu ambazo ilitakiwa izifanye yenyewe inafanya taasisi za nje matokeo yake wale hawawezi kuwa na uchungu; kama ni kutibu watu hawawezi kuwa na uchungu kama walivyo Watanzania wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine napenda kuzungumzia maafa. Sheria Na.7 ya mwaka 2015, Disaster Management Act, imetaja na imefafanua Kamati za Maafa kuanzia ngazi ya Taifa mpaka ngazi ya kijiji. Kwenye ngazi ya Wilaya imemtaja Mkurugenzi kama Mwenyekiti na wajumbe wengine. Leo tuna maafa kwenye kila kona ya nchi hii, ni kwa kiwango gani Halmashauri zina-respond kama hazimuachii Waziri Mkuu pamoja na mama Jenista pale? Ni vyema zikatenga fungu na fungu lile lisibadilishwe likafanye kazi ya maafa. Leo kuna mafuriko kila sehemu kwa hiyo, tunajikuta tunakwepa jukumu letu la msingi tunawaachia watu wengine tunashindwa kutimiza jukumu letu ambalo tunatakiwa tulifanye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ambayo napenda kuchangia ni effective control ya Council, ni vyema Wizara ika control vizuri Halmashauri zake. Naomba nitolee mfano na limezungumzwa hapa ndani suala la Makao Makuu, mfano sisi pale kwetu Mufindi kwa lengo la kupeleka huduma kwa wananchi ilikubalika tuanzishe Halmashauri nyingine lakini Makao Makuu inayojengwa ni kilomita 6 kutoka ilipo Makao Makuu ya Halmashauri ya zamani, hapa ni kwa faida ya nani? Naomba Mheshimiwa Waziri na timu yake ikiwezekana maeneo kama haya wayaundie timu maalum wakayatazame, je, ni kwa maslahi ya wananchi? Hoja siyo wapi ikae lakini inapowekwa Makao Makuu itazame maslahi mapana ya walio wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho siyo kwa umuhimu napenda pia kuongezea kwenye kifungu ambacho kimezungumzwa na wenzangu tukatazame maslahi ya Madiwani wetu, Wenyeviti wetu wa Vijiji na Wajumbe wa Serikali ya Vijiji, hawa ndiyo wanafanya kazi kubwa Zaidi. Hili tunaweza kulifanya kwa namna kuu mbili; moja kama kutakuwa na pesa za Serikali Kuu ziende, lakini pili kuzibana Halmashauri zipeleke kama ni posho au nauli ili wale wanaohangaika na wananchi kimsingi waweze kupata posho kama hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)