Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Janejelly Ntate James

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kunipa Afya na leo na mimi nichangie kwenye bajeti ya TAMISEMI. Lakini nikupongeze Mheshimiwa Ummy kwa kuteuliwa na kuendelea kuaminika kuisaidia Serikali pamoja na wasaidizi wako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze pia walioandaa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, hawa kweli kweli walikuwa na fikra zilizo sahihi, kwa mara ya kwanza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ukurasa 180 -181 inaongelea maslahi ya watumishi wazi kabisa, na niwashukuru waliochangia kwa kusema maslahi ya watumishi wa Tanzania. Hasa wengi mlijikita kwa walimu lakini niipongeze pia Serikali imefikia uchumi wa kati kabla ya mwaka 2025, lakini waliofanya hii kazi ni watu gani, ni watumishi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na nilipokuwa naangalia makundi yangu ya watumishi hata Wabunge mpo ni watumishi wangu wa miaka mitano mitano, lakini kuna wale watumishi wanaotoka baada ya miaka 60 kustaafu. Lakini watumishi hawa walikuwa wanafanya hivi vyote kwasababu gani, walikuwa na maagano na Serikali, Serikali kupitia vyama vya wafanyakazi iliwaomba watumishi, kwamba tuvumilie kwa miaka mitano tujenge Uchumi, baada ya kumaliza kujenga uchumi tutakuja na maslahi yenu na ndio maana Ilani ya Uchaguzi imeyasema tumezungusha hapa tunaongea matatizo ya watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa unjuka wangu mheshimiwa Jenista ulipokuwa unawasilisha bajeti yenu ya Waziri Mkuu niliangalia angalia sikuona suala la nyongeza ya mshahara lakini nikasema ngoja ninyamaze labda ndio style, TAMISEMI mmekuja na bajeti bado haioneshi ukiangalia vifungu vya mishahara kama kutakuwa na nyongeza, na jambo hili tusipoliangalia na kulisemea tunasema mtatizo matatizo lakini hatuangalii chanzo cha tatizo. Yawezekana hata kushuka kwa utendaji ni watumishi wamefika mahali wamekufa ganzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ebu tujiulize kwenye miaka mitano ni watumishi wangapi wamestaafu kwa mshahara wa zamani ambapo tunajua sheria kikokotoo hufanyika kwenye mshahara, waheshimiwa Wabunge niwaombe kwenye hili wote mni-support tuongelee suala la nyongeza ya mshahara, nyongeza ya mshahara kwa mtumishi inaongeza hata mafao yake, lakini miaka mitano watumishi hawa walivumilia ili tujenge uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tumeshajenga uchumi umefika uchumi wa kati tena kabla ya muda wake, na ukiangalia mambo ya kufanyia watumishi kwenye Ilani yapo 16 sasa kama tukipita bajeti hii bila kulisema hili, ambalo limeandikwa pale naomba kunukuu; “kwamba Serikali itaboresha mishahara ya watumishi wa umma kwa kuzingatia ukuaji wa uchumi wa Taifa na tija ya wafanyakazi,” tija wameifanya watumishi wamefikisha uchumi wa kati kabla ya muda wake na uchumi umefika uchumi wa kati. Sasa tunasubiri nini kuongeza mishahara? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuongeze mishahara watumishi, Waheshimiwa Wabunge na nyie linawahusu, watumishi wakiongezewa na nyie mtaongezewa kwasababu na nyie ni watumishi wa miaka mitano lakini naona tunalifumbia fumbia macho. Sasa kwa sababu nimetumwa kuwakilisha watumishi leo ngoja nilisemee hilo la mishahara ya watumishi na nimeona Waziri wa Fedha anaondoka na begi lake lakini nadhani atanisikia alipo kama bajeti yake itakuja haina nyongeza ya mshahara… (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ngoja ngoja Mheshimiwa Janejelly, waheshimiwa wabunge huwa narudia mara kadhaa, Mbunge unapochangia zungumza na kiti na sio Mawaziri.

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

NAIBU SPIKA: Kwasababu ukizungumza na Waziri asipofanya usije ukalidai Bunge, ongea na kiti ndicho kinachotunza kumbukumbu ni nani ambaye ameomba kitu gani. Hata Mheshimiwa Ummy hapa akinyanyuka akaenda usiseme Waziri ametoka namsubiri atayapata tu, kwa hiyo, wewe zungumza na mimi usimwangalie Waziri yupo katoka taarifa zake atazipata.

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongee na kiti chako, niseme hivi kama Wizara ya Fedha ikija haina nyongeza ya Mishahara ya watumishi kwa kweli kwa bajeti hiyo wabunge mni-support tukamate shilingi watumishi wanaumia kwa nyongeza ya mishahara na yawezekana haya yote tunaona utendaji unashuka, Wakurugenzi wanafanya vibaya, unajua msongo wa akili unaweza ukafanya, ukafanya mengi, yawezekana wengine wanakaa kimya, wengine wanakuwa na hasira lakini wengine wamedumaa utendaji umedumaa. Hapa nina meseji nilikuwa ninazisoma watumishi wanasema miaka mitano tuliyoahidiana imekwisha kuja jambo letu ebu liongee jambo letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na jambo la watumishi ni nyongeza ya mshahara, jambo la watumishi ni kupandishwa vyeo, jambo la watumishi ni kuangalia hayo maslahi yao, nguzo yao kubwa ni mshahara maisha yanapanda, kodi za nyumba zinapanda ada za shule zinapanda lakini mshahara upo vile vile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee na suala la walimu hakuna mtumishi anayeumia kama mwalimu na hii haina mwalimu yupo Dar es Salaam haina mwalimu yupo Tabora. Walimu sasa hivi nauli ya likizo imekuwa ni kitendawili, ni neno gumu kwenye kamusi mtu anakwenda likizo tatu nne hajawahi kulipwa nauli ya kwanza ya likizo. Wakistaafu nimeshuhudia Mkurugenzi mmoja anawaambia nitawatafutia roli sasa, na hakunijua kama ni Mbunge wa Wafanyakazi lakini nilimwambia hakuna mwalimu atakayekwenda na roli, alisema nitawapakia kwenye roli sina fedha TAMISEMI hawajaleta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwalimu aliyefanya kazi akafikisha umri wa miaka 60 leo unamwambia utampeleka na roli, utampeleka na roli wapi lakini wanawapiga dana dana akienda Manispaa wanamwambia TAMISEMI ndio wana fedha zako, akienda TAMISEMI wanamrudisha. Jana nilikuwa na walimu ambao ni tatizo wanaongezwa vyeo lakini mishahara haibadilishwi, mpaka amefikia kustaafu wapo watano na ni Manispaa ya Ilala inabidi niseme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wamenifuata Bungeni hapa wamelipwa pensheni lakini wa mishahara ya zamani lakini Manispaa inawaambia mfuko ndio una tatizo, namshukuru sana Mkurugenzi wa Mifuko, tumeenda pale ametupokea aka-print barua zote ambazo alikuwa anaandikiana na Manispaa kwamba ebu lipa mapunjo yao, lipa faini mnazotakiwa hawa wapewe tofauti zao. Lakini ebu fikiria mstaafu amepanda gari kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma na unamdanganya tu unamwambia mfuko ndio unashida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu walipandishwa vyeo miaka sita mtu hakubadilishiwa mshahara na amefikia kustaafu. Naomba Wabunge tuwe wakali Wabunge kazi yetu ni kuishauri Serikali tuwashauri haya wayaangalie na sio kwa walimu yanawapata watumishi wengi, watumishi wengi, wengi mno wapo kwenye tatizo hilo la kulipwa pungufu ya pensheni kwasababu wanapopandishwa madaraja mishahara yao haibadilishwi lipo kabisa hilo. (Makofi)

Mheshimia Naibu Spika, mwisho naunga mkono hoja lakini tuliangalie la nyongeza ya mshahara naunga hoja mkono. (Makofi)