Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Angelina Adam Malembeka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini pia nichukue nafasi hiyo hiyo kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri, Manaibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianzie na suala zima la utumishi kuhusiana na suala la uhamisho. Kumekuwa na tabia ya kuwaambia watumishi akatafute mtu wa kubadilishana naye. Kwa kweli kitendo kile mimi binafsi naona kwamba ni kumsumbua mtumishi lakini pia kumfanya asifanye kazi zake. Mtu yuko Mwanza anataka kwenda Mtwara anaambiwa akatafute mtu wa kubadilishana naye.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikichukulia mfano wa walimu ule muda ambao alitakiwa awe anafundisha inabidi atoke aende kwenye halmashauri kuangalia kama kuna mtu anayetaka kuja Mtwara na halmashauri nyingine zipo mbali na kituo cha mtumishi. Naomba Wizara iwe na mbinu mbadala, badala ya kumwambia mtumishi akamtafute mwenzie wa kubadilishana naye basi Wizara iangalie nani anataka kwenda Mtwara apelekwe na yule wa Mtwara anayetaka kwenda Mwanza apelekwe badala ya jukumu lile kumuachia mtumishi mwenye ahangaike nalo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine nizungumzie posho za Madiwani, imekuwa ni utaratibu kila Bunge tukija tunazungumzia posho za Madiwani. Wale ni wenzetu tunafanya nao kazi, tunapokuwa tunasema halafu hawatekelezewi tunaonekana pia Wabunge hatuna maana tuna ubaguzi. Naomba Wizara isimame kidete kushughulikia posho za Madiwani na ikiwezekana wawape mshahara maalum ijukane Diwani ana mshahara shilingi ngapi kwa mwezi halafu hizo posho aendelee kuchukua kutokana na vikao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nalisema hili kwa sababu kuna vikao vya Madiwani vinafanyika hawapewi hata hiyo posho yenyewe ya kikao, wanasema halmashauri haina fedha. Madiwani wanakopwa, wanakwenda kwenye vikao wengine wanatoka mbali nauli hawana, wanapata usumbufu lakini wapo chini zaidi kwa wananchi hata mwananchi akimwambia tunataka timu yetu ya kwenye mtaa tupate mpira fedha ya kununua mpira hana. Kwa nini tusiwafikirie Madiwani ili na wao waweze kufanya kazi zao kwa umakini zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika suala zima la uandikishaji wanafunzi wa darasa la kwanza. Halmashari nyingi zimeonesha kwamba zinaandikisha watoto wengi lakini ukifuatilia wanapofika mwisho ile idadi inapungua na inapungua kuanzia darasa la tano, la sita mpaka darasa la saba. Ukiangalia sababu kubwa ni utoro na mimba za utotoni au mimba zisizotarajiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niziombe basi halmashauri ziweke mkakati wa dhati kati ya halmashauri na wazazi kuhakikisha wale watoto wanaoandikishwa wafike shule na ikibidi kama kushtaki basi na mzazi naye ashtakiwe. Kuna wazazi wanaojua kabisa mtoto wangu haendi shule na yeye yupo kimya, kama elimu imetolewa bure kwa nini halmashauri ziandikishe watoto 600 halafu mwisho wa siku watoto wako 200 hao wengine wamekwenda wapi? Ni lazima tujizatiti kuhakikisha kwamba wanafunzi walioandikishwa wamalize kama ilivyotarajiwa badala ya kuwa na sifa kwamba tumeandikisha watoto kadhaa lakini mwisho wa mwaka tunajikuta watoto wako kidogo kwa sababu ya utoro na mimba zisizotarajiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilizungumzie suala la uwezeshaji kiuchumi kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Zipo halmashauri zilizofanya vizuri lakini kuna halmashauri zingine hazitoi zile asilimia 10, wanajipangia wanavyotaka wao. Ukiangalia makusanyo yao ya mapato ya ndani hayalingani na zile pesa wanazozitoa. Ni vizuri suala hili lisimamiwe ili zile asilimia 10 zitolewe kama zilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika utoaji wa asilimia hizi haki itendeke kuna vikundi ambavyo viko ndani ya halmashauri havijawahi kupata mikopo hii.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Boniphace Getere.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nataka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba hii kero ya asilimia 10 kwa halmashauri zote nchini Tanzania ili imalizike inatakiwa kuwepo na akaunti mbili benki; akaunti hiyo ya asilimia 10 na akaunti ya Halmashauri. Kila fedha ya halmashauri inayoingia kwenye akaunti ile asilimia 10 iende kwenye akaunti. Hilo ndiyo itakuwa suluhisho ya kero hii. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Getere huo ni ushauri kwa mchangiaji au ni taarifa kwa mchangiaji?

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Angelina Malembeka, malizia mchango wako.

MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Taarifa hiyo nimeipokea kwa mikono miwili kwa sababu inaleta tija kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mgao huo huo wa asilimia 10 napenda kuongezea kwamba utaratibu ufanyike. Kwa sababu kuna Halmashauri ambazo unakuta kuna kikundi kinapata mara mbili mpaka mara tatu lakini kikundi kingine mpaka miaka mitano inapita hawapati. Kama wanakosea kufanya utaratibu mwafuate, mwaeleze jinsi gani wafanye ili na wao wapate ile mikopo. Badala ya kuwa wanaomba miaka yote hawapati lakini makundi mengine yanapata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hilo, pia ni vizuri basi Halmashauri zijipange tuone zile fedha za marejesho zinazorudishwa, ziko wapi na zinafanya nini? Isiwe kila mwaka wanapanga shilingi milioni tano, mwaka unaofuatia milioni tano, mwaka unaofuatia milioni tano, lakini zile zinazorudishwa hazionekani ziko wapi na zinafanya nini? Ni vizuri zionyeshwe na tujue zinafanya nini; kama zinaongezwa kwenye mikopo au zinafanya kazi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia suala zima la ukarabati wa shule kongwe na baadhi ya Vyuo vya Ualimu. Kazi imefanyika nzuri sana, lakini hapa hoja yangu ni kwamba, tusiwe tunasubiri tu kukarabati shule kongwe na zile zilizopo ukarabati mdogo mdogo uwe unaendelea kufanyika ili kuondoa madhara makubwa. Kwa sababu unapokuta labda jengo limebomoka mlango mmoja, siyo tunasubiri mpaka milango yote ivunjike na madirisha yote yavunjike, haitaleta tija. Ni vizuri hizo shule ambazo bado ni mpya lakini zimeanza kuonesha matatizo zianze kukarabatiwa mapema ili kuondoa athari kubwa kwa siku za baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuzungumzia suala zima la ukamilishaji wa maboma ya majengo mbalimbali yaliyoanzishwa na wananchi. Wananchi waliitikia mwito wa kujitolea wakajenga nyumba mblimbali; kuna nyumba za walimu, zahanati, shule na vituo vya afya. Sasa yale maboma kwanza yanawatia uchungu wananchi. Wameacha shughuli zao ku-support Serikali halafu Serikali mpaka sasahivi wanayatazama. Ni vizuri tujipange ili yale majengo yaliyoanzishwa na wananchi yakamilike ili waweze kuyatumia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa ili niache fursa kwa wenzangu kuchangia, nizungumzie suala zima la mama wajawazito na watoto hususan kwenye vituo vya afya. Kuna maeneo ambayo wanasema huduma hii inatolewa bure, lakini ukienda unakuta huduma hizo zinalipiwa kwa njia ya ujanja ujanja. Mtoto ana tatizo hili, anaambiwa chukua karatasi nenda kanunue kitu fulani. Mtoto ana tatizo hili, nenda kanunue dawa fulani, wakati hizo dawa wakati mwingine zinapatikana kwenye lile eneo na wazee wanafanyiwa mambo hayo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri pia tujipange tuangalie jinsi gani ya kukamilisha hili zoezi bila kutia kero kwa wananchi kwa sababu kama tumekubaliana elimu bure, afya bure kwa wale ambao wana sifa za kupata wapate bure kweli. Siyo wanaenda pale wanalipishwa kumwona daktari na kadhalika, halafu na dawa zenyewe hawapati wanaambiwa wakanunue. Hiyo siiafiki, tujipange vizuri, Halmashauri zifanye kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na afya yangu, leo naomba niishie hapo. Naunga mkono hoja. (Makofi)