Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani kwa kukumbukwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru kwa kupata fursa ya kuchangia katika Wizara hii ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri Ummy na Manaibu Mawaziri wake wote kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya na tunaendelea kuwashukuru sana kwa mchango wao kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe taarifa kuhusiana na wananchi wangu wa Jimbo la Kilombero ambapo jana kuna mvua zilinyesha na Mto wetu Lumemo ulijaa maji na maji mengine yakamwagwa kwenda kwa wananchi. Namshukuru Mheshimiwa Jenista kwa ushauri na msaada anaoendelea kutupatia kukabiliana na hali hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, michango mingi tumetoa hapa na michango mingi tunayotoa katika Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, inataka kutumia tu pesa. Nina maoni kwa Mheshimiwa Waziri na Wizara waangalie vipaumbele vya kuwekeza kwenye miradi mikakati ya kuzalisha mapato ya halmashauri. Watafute fedha katika bajeti yao wawekeze katika halmashauri ambazo zimeandika maandiko, zime-qualify, zina Hati Safi; kama Halmashauri ya Mji wa Ifakara wanasema tukiwekeza bilioni tano katika soko baada ya miaka miwili, mitatu zile fedha zitarudishwa kwa sababu Mji wa Ifaraka una biashara kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba tunazungumzia mahitaji lakini wazo langu la kwanza la msingi nataka kuwaomba muwekeze. Kwa mfano, sisi tuna andiko letu kuhusu soko la Ifakara. Soko la Ifakara pale mjini mvua ikinyesha ni balaa tupu na linakusanya millions of money kwa siku. Kwa hiyo, pamoja na kwamba tunataka zahanati, hospitali na kadhalika lakini pia wanaweza kuweka vipaumbele katika kuchangia miradi mikakati kama vile stendi, soko na kadha wa kadha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, Mji wetu wa Ifakara una mitaa 33, nimeona kwenye hotuba Mheshimiwa Waziri ameitaja ni zaidi ya mwaka mmoja mpaka sasa hivi hakuna Mtendaji wa Mtaa hata mmoja. Nimekaa na Wenyeviti wa Mitaa, barua imeandikwa na mimi nimekumbushia. Sasa Mheshimiwa Waziri kwa kweli mitaa 33 hauna Mtendaji wa Mtaa hata mmoja zaidi ya mwaka mmoja, Wenyeviti wanafanya kazi wenyewe, kwa kweli ni jambo ambalo linakarahisha. Tunaomba utusaidie na ile barua nitakuletea nakala unisaidie pamoja hizo posho za Wenyeviti wa Mitaa nazo wanalalamika sana kwamba zinachelewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru sana Serikali kwa kubadilisha kanuni ya mikopo hii ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. Sasa tumeambiwa watu watano, mwenye ulemavu mmoja anaweza kukopeshwa, hii ilikuwa changamoto kubwa sana kwa upende wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili nalotaka kuchangia ni kuhusu TARURA. Kwa mfano, Jimbo langu la Kilombero ni wakulima wa mpunga na miwa, barabara zetu zote ili tuzimalize lazima tuchonge, tuweke kifusi, tushindilie. Zamani halmashauri yetu ilikuwa na vifaa vya kufanyia kazi hizo, kwa sababu watu wa TARURA ni ma-engineer, kwa nini Wizara msione uwezekano wa kununua vifaa vinne tu wanaseme ma-engineer, wakivipata katika halmashauri na wilayani hata dharura za ukarabati wa barabara zikitokea watafanya. Kwa mfano, Jimbo la Kilombero tuna milima ina vifusi kibao mpaka wilaya nyingine zinakuja kuchukua vifusi kutoka kwetu. Tupate grader, shindilia (roller), excavator, tipper; vifaa vinne tukipata kama halmashauri mwaka mzima tutaweza kutengeneza barabara zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba TARURA, najua imepata bajeti ndogo sana, kwa mfano kwetu sisi kuna shilingi milioni 454 haiwezi kufanya kazi ya jimbo zima. Pamoja na kuongezewa bajeti lakini tungewekeza hizo fedha, kwa mfano, tukitengewa one billion tukapewa grader na excavator tutatafuta hata tipper zitachukua kifusi zitakwenda kumwagia kwenye barabara za wananchi mwaka mzima tunafanya hiyo kazi, Mbunge unapewa fedha za Jimbo unaweza kununua mafuta ukaweka kwenye grader ukaenda ukachonga, ukaweka kwenye tipper ukaenda kumwaga kifusi wananchi wakaendelea kupata huduma za barabara. (Makofi)

Mji wa Ifaraka unakua kwa kasi sana kiasi kwamba Jumamosi na Jumapili benki hazifungwi. Tunaomba hawa TARURA watuwekee taa za barabarani, zile lami za Ifakara Mjini zina mashimo, tuongezewe lami kwa mfano barabara za Posta kwenda Hospitali ya St. Francis, CCM zamani kwenda kwa Salewa, naomba tuweze kuwekewa lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo kwenye TARURA, tunaishukuru Serikali tunajengewa na TANROADS barabara ya Kidatu kwenda Ifakara. Katikati ya barabara hizi kuna Stendi Kuu kwa mfano Mwaya, Kidatu na Ifaraka Mjini, barabara zile za kuunganisha kutoka barabara kubwa kwenda kwenye stendi zile au masoko ni za TARURA. Kwa hiyo, kwa sababu kuna mradi mkubwa lami wa kilometa 66.9 ambao utatuunganisha na Mkoa wa Morogoro, TARURA waunganishe stendi na hiyo barabara kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme jambo moja kubwa sana tunaomba Waziri atusaidie na hapa kweli nitamshika kidogo ushungi, ni kuhusu mgawanyo wa mali katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara na Halmashauri ya Mji wa Mlimba. Sisi ni Wilaya ya Kilombero, tuna Jimbo la Mlimba na Jimbo la Kilombero. Jimbo la Kilombero lina Halmashauri ya Mji wa Ifakara na Jimbo la Mlimba lina Halmshauri ya Mji wa Mlimba.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali paligawanywa mali Kata 9 za Mji wa Ifakara na Kata 26 za Jimbo la Kilombero. Baadaye Mheshimiwa Rais akatengua mgawanyo huo akaiongezea Halmashauri ya Mji wa Ifakara Kata 10 na Mlimba akaipunguzia ikabaki na Kata 16. Sasa mgawanyo ulifanyika wakati Halmashauri ya Mji wa Ifakara ina Kata 9, Makao Makuu ya Wilaya yote yale ya Halmashauri ya Ifakara ndiyo yalikuwa Makao Makuu ya Wilaya yana nyumba za Serikali, nyumba za taasisi, nyumba ya Mkuu wa Wilaya na ofisi zote za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimelisema mara kadhaa hili tunaomba zile nyumba za Serikali ambazo ziko Ifakara zitumiwe na Halmashauri ya Mji wa Ifakara kwa sababu Halmashauri ya Mlimba ni mpya imeanza kujenga kila kitu na juzi Serikali imepeleka one billion kujenga makao makuu ya halmashauri mpya. Sasa hapa Halmashauri ya Mji wa Ifakara inabidi tuanze kuomba upya fedha Serikalini tujenge tena nyumba za Serikali na za Wakuu wa Idara. Hivi Mheshimiwa Waziri navyozungumza TAKUKURU wamepangishiwa nyumba halmashauri, Mbunge nimetafuta ofisi ya vyumba viwili naambiwa nyumba zote zinamilikiwa na Halmashauri ya Mlimba wakati zipo Halmashauri ya Ifakara, imebidi nimuombe Mkuu wa Wilaya kanimegea kichumba ndiyo ofisi ya Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nachokiomba chonde chonde kwa sababu mnapeleka fedha Mlimba, basi hii Halmashauri ya Mji wa Ifakara iweze kutazamwa vizuri na ipate hizi nyumba zote, zibadilishwe au zifanyiwe hata tathmini ikipatikana kama ni shilingi bilioni 2, 3, Halmashauri ya Mlimba wapewe fedha hizo sisi tupewe zile nyumba ziendelee kutumika kwa sababu sasa hivi zina popo na zimekuwa mapori wakati huo Mkurugenzi wa Ifaraka hana nyumba; nyumba kagaiwa Halmashauri ya Mlimba ambayo ni kilometa 20 kutoka Ifakara. Hii ni Serikali moja lazima kwa kweli tujipange pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la msingi ambalo naomba kuchangia ni michango ya elimu ya madawati na viti. Kule tunagombana na wananchi kwa sababu ukienda wana-play video ya Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli amemwita Waziri wa TAMISEMI na Waziri wa Elimu kawafokea Ikulu hataki michango ya shule. Tena ana-play kabisa anasema Mbunge wewe wa CCM umekuja, angalia Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli huyu, apumzike tu kwa amani, wanalalamika wanachangishwa wapeleke viti na meza wakati wamemsikia Mheshimiwa Rais anasema hataki michango na mwenye mchango apeleke kwa Mkurugenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wangu pamoja na kwamba hawana sekondari na wanataka sekondari, wanasema walau hii michango ingekuja wakati tunavuna mpunga sio Januari na Februari tunaenda kulima tunachangishwa tunaambiwa Sh.50,000, Sh.60,000 na lazima uje na kiti na meza. Mheshimiwa Waziri amesema atanunua madawati, atatusaidia madarasa, katika uongozi wake akiweza kutatua changamoto hii ya michango atakuwa ametusaidia kiasi kikubwa sana. Naomba utoke ufafanuzi wananchi wanaruhusiwa kuchangia namna gani? Kama Serikali inasimamia ile elimu bila malipo tuambiwe wazi kwa sababu kuna mkanganyiko. Maelekezo ya Serikali yanatoka kwamba Februari ikifika wanafunzi wote waingine form one, Mkuu wa Wilaya hana bajeti, Mkuu wa Mkoa hana bajeti, anarudi kwa Wenyeviti wa Vijiji anaenda kuomba michango ambapo mwanakijiji mmoja akitoa anataka na wenzake wote watoe hata kama ana uwezo ama hana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kidogo kuhusu afya. Sisi Ifakara tuna hospitali ya St. Francis, ni hospitali ya Mission, Serikali itatuchukua muda mrefu sana hata kama tunajenga hospitali yetu kuifikia hospitali hii. Hospitali hii ina gharama kubwa, inahudumia Jimbo la Mlimba, Ulanga, Malinyi, Kilombero na wakati mwingine mpaka Mikumi, zamani walikuwa wanapewa OC shilingi milioni 4 au 5, lakini sasa hivi imeshuka mpaka Sh.100,000. Umeme wanatumia shilingi milioni 10 kwa mwezi hawajapunguziwa. Tunaomba Serikali muiangalie hospitali ya St. Francis ili iweze kupunguza gharama wakati tunajenga hospitali yetu ya Jimbo. Jimbo letu lina Kata 19, tuna vituo vitatu vya afya, hivi navyozungumza Kituo cha Mang’ula wodi ya kina mama bado ina changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu spika, nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)