Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi siku ya leo kuweza kuchangia katika bajeti hii ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi nitumie fursa hii kwanza kumpongeza Waziri na Manaibu wake kwa kupata nafasi ya kuongoza Wizara hii nyeti katika Taifa letu, Wizara ambayo inatazamwa na Watanzania karibu asilimia 60.

Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze moja kwa moja kwenye hoja za msingi ambazo nataka nichangie. Kuhusu TARURA; fedha inazopata ni ndogo sana, tunaiomba Wizara iongeze fedha kwenye TARURA na ikiwezekana tuangalie kama tunaweza kuiwezesha, of course tunatambua TANROADS wanapata asilimia 60 mpaka 70 na TARURA wanapata asilimia ndogo ambazo zinaweza kuwafanya wakatengeneza barabara chache huku wakiwa na mtandao mkubwa wa barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuombe Wizara iliangalie kwa jicho la tatu. Ikiwezekana, kama hatuwezi kupata fedha za ndani, basi angalau tuangalie hata fedha za nje, tuweze kuboresha kuongeza Mfuko huu wa Fedha. Mfano mdogo nikichukulia Wilaya yetu ya Igunga, tunapewa fedha bilioni moja kama na milioni 200. Wilaya ina majimbo mawili, jimbo langu peke yake madaraja ambayo yanahitaji kujengwa ni zaidi ya manne.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Daraja la Mto Manonga pale kwenye Kijiji cha Mondu; kuna Daraja la Mazila kule kama unakwenda Buhekela kwenda kuunga Uyui, kule kuna madaraja matatu. Kila daraja moja linagharimu milioni 300 mpaka 500. Hapa kwenye haya madaraja manne ni zaidi ya bilioni moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tukisema tukatengeneze madaraja haya, hatuna bajeti ya kutengeneza barabara za mitaa. Hata tukienda kutengeneza barabara kuunganisha wilaya yetu na wilaya zingine, madaraja ndiyo kiunganishi cha barabara hizi tunazozitengeneza. Sasa tuiombe Wizara iongeze fedha kwa TARURA, lakini pia ituongezee fedha katika Wilaya yetu ya Igunga kwa ajili ya kujenga Madaraja kama ya Mondo, Ncheli, Mazila kule Buhekela na Madoke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe pia TAMISEMI waangalie utendaji kazi wa TARURA wenyewe. Hata kama fedha tunazipata, lakini bado wanapaswa kuwasimamia kwa karibu katika kuleta tija na ufanisi wa kazi zao. Hata kama ni fedha ndogo lakini bado usimamizi unatakiwa uwe wa hali ya juu. Wakiachwa wakajiendea wenyewe kazi na hizi fedha tunazowapa hatutaona tija ya fedha wanazozipata. Kwa hiyo niombe wasogeze jicho kwa ukaribu kuweza kuwaangalia namna gani wanaweza ku-perform katika maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta nyingine ambayo nataka kuchangia leo ni sekta ya elimu. Jimbo langu ni jipya na Mheshimiwa Waziri anatambua niliingia mwaka 2015, nilianza na ujenzi wa sekondari, kata nane hazikuwa na sekondari. Nimeweza kufanikisha kujenga kwa nguvukazi ya sisi na wananchi, angalau tuna madarasa mawili mawili. Nimefurahi kuona kwenye bajeti hapa imetengwa fedha, milioni 700, kujenga sekondari kwenye kila kata.

Mheshimiwa Naibu Spika, Nimwombe Mheshimiwa asije na ile programu ya kugawa kila halmashauri watoe mara shule mbilimbili, tatutatu au waje kama vile walivyofanya kwenye sekta ya afya, wanatoa zahanati tatutatu. Wakija na hiyo programu tutaathirika wengine kwa sababu mzigo tulionao ni mkubwa, hatufanani kwenye ujenzi wa sekondari za kata; kuna wengine wamekamilisha na wengine hatujakamilisha. Kwa hiyo waangalie uwiano wa kugawa fedha katika hizi shule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, nilimsikia Mheshimiwa Mbunge wa Dar es Salaam alisema, wao Dar es Salaam hawahitaji mbegu kwa sababu hawana mashamba. Kwa hiyo huwezi kuniambia utagawa shule kila mkoa, kila halmashauri, kwa sababu kuna maeneo mengine wana shule mpaka za maghorofa, kwa hiyo ukiwapelekea ni kama vile unawaongezea tu mzigo na hela ambazo hazina kazi katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba watuletee kwenye mahitaji kama kwetu ambako watu wanataka fedha hizi tujenge hizi shule. Mfano, tumejenga Shule za Sekondari Buhekela, Manonga, Mwamala, Tambarale, Ugaka; tumejenga Shule ya Sekondari imepewa jina la Seif Gulamali, tumejenga Shule ya Sekondari Borogero, ni shule mpya. Tunaomba fedha hizo walizotenga watupatie tuweze kuzikamilisha na wananchi wale wa vijijini wahisi kwamba na wao wana haki sawa kama vile watu wengine ambao wanapewa migao ya fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzungumzia pia kwenye ujenzi wa mabweni. Hivyo hivyo nimwombe Mheshimiwa Waziri, shule zetu vijana, watoto wa kike, wanatembea karibu kilometa tatu mpaka tano, mpaka kumi kufuata shule. Ukienda kuangalia kwenye kata zetu, tuna kata kubwa, tuna Kata inaitwa Mwashiku, kutoka kwenye kijiji kwenda kwenye shule ya kata mtoto wa kike anatembea umbali wa kilometa kumi, saba au tano, kufuata shule. Hivyo, wakituwekea bweni tutapunguza adha kwa mtoto wa kike kutembea…

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gulamali, kuna taarifa; Mheshimiwa Mbunge.

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa na mimi ni Mbunge wa Jimbo la Igunga Mjini pale, ambaye ni Mbunge mwenzangu, kwenye hizo kilometa kumi wanazotembea wanafunzi wakiwa wanakwenda shuleni, wanakutana na mito imejaa maji na hakuna madaraja ambayo anasema Mheshimiwa. Kwa hiyo kama anavyosema Mheshimiwa kuhusu TARURA waongezewe fedha kuweza kujenga hayo madaraja, naomba kumpa taarifa hiyo Mheshimiwa. Ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Kweli TAMISEMI kumekucha. (Kicheko)

Mimi mwenyewe nataka nimpe taarifa Mbunge, sasa hapo ndiyo mtihani; Mheshimiwa Gulamali, malizia mchango wako.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, nimeipokea taarifa hiyo. Niseme tu, tupewe fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni haya, lakini itasaidia kuwaokoa watoto wa kike na mimba na uhai wao, lakini pia utawapa utulivu na kuweza kufaulu na wao kufikia malengo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la ajira katika sekta ya elimu. Wapo Walimu wanajitolea kufundisha katika hizi sekondari; hao wangepew kipaumbele cha kwanza. Mtu anafundisha mwaka mmoja, miaka miwili, miaka mitatu, zikija kutoka ajira wale wanakosa wanapata wengine ambao hata hawakuwahi kufikiria kujitolea. Kipaumbele cha kwanza wafikiriwe Walimu wanaojitolea kufundisha. Kwenye Wilaya ya Igunga wapo Walimu wa aina hiyo wengi sana. Nimwombe Mheshimiwa Waziri alichukue hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nikumbushe katika sekta ya afya; alipokuja Waziri Mkuu jimboni, Kituo cha Afya cha Choma cha Nkola aliahidi kutupa milioni 300 kwa ajili ya kupanua majengo ya maabara, jengo la mama na mtoto na mambo mengineyo. Nikumbushe ahadi hii, TAMISEMI watupe hiyo fedha tuweze kujenga hayo mahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia alipopita Rais wakati akiomba kura, alisimama Ziba akawaambia wananchi nipeni kura, mpeni kura Mbunge, wapeni kura Madiwani, hapa Ziba tutajenga kituo cha afya. Kwa hiyo niwakumbushe ahadi hizi za viongozi wetu wa Kitaifa wasizisahau. Tunahitaji hizo fedha na tumeona wametenga fedha kwenye bajeti, kwa hiyo katika kupanga kwenu kupeleka fedha basi watupe Choma, Ziba, Kitangiri na Uswaya. Vituo hivi vya afya vitatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nipende kusema, pia Mheshimiwa Rais, Hayati Dkt. Magufuli, wakati anapita kwenye kampeni alisimama pale Ziba akawaambia wananchi wa Ziba na Igunga kwamba hapa Ziba panafananafanana kuwa na wilaya na mkitupa sisi tutawapa Wilaya.

Vilevile pia alipofika Nzega alisema hapa panafananafanana na mkoa. Tulikuwa tumeomba Mkoa wetu wa Tabora ndiyo mkoa mkubwa kuliko mikoa yote Tanzania, ukifuatiwa na Mkoa wa Morogoro, mkoa wetu una zaidi ya square meters 75,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutoka Igunga kwenda Tabora Mjini ni kilometa 200; tunaomba huo Mkoa; tunaomba watupatie Mkoa wa Manonga ambao Makao Makuu yatakuwa pale Nzega. Kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa atupatie huo mkoa ili tuweze kurahisisha huduma za wananchi, tusogeze huduma za wananchi karibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulipata taarifa hivi karibu za Hati ya CAG natambua kuna maeneo ambayo yamezungumzwa sehemu mbali mbali katika Taifa hili. Lakini hata wilaya yetu ya Igunga imeguswa tumeona pale tumepewa hati chafu hii si sifa nzuri, na hii haipendezi, lakini niwaombe Mheshimiwa Rais, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alivyopita alimtumbua yule Mkurugenzi. Ninamshukuru sana kwa kumtumbua yule lakini najua bado majibu yapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nakuomba TAMISEMI muangalie kwa macho manne manne mtumbue sana. Mlete pale viongozi wengine, mlete wakurugenzi na wadau wengine, ninakushukuru kwa kunipa muda wako ahsante sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa…

MHE. SEIF KHAMIS S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi/Kicheko)