Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Rose Vicent Busiga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. ROSE V. BUSIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia tena kwa mara nyingine. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa namna ambavyo ametulalia siku ya leo.

Pia nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu kwa namna ambavyo ameendelea kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa sana pamoja na timu yake nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona nikikaa kimya nitakuwa sijawatendea haki watendaji wenzangu nchi nzima wa Kata na Vijiji kwa sababu Wizara hii ya TAMISEMI inawagusa wao.

Mheshimiwa Spika, nakumbuka niliwasilisha wasilisho langu la kuomba Wizara ya TAMISEMI iangalie vizuri namna ambavyo inaweza kuwasaidia Watendaji wa Kata pamoja na Watendaji wa Vijiji kulingana na jinsi ambavyo wanafanya kazi katika mazingira magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona wazi kabisa watendaji hawa ndio wanaosimamia maendeleo katika kata zao, katika vijiji vyao, lakini pia nikijikita kwenye suala la ukusanyaji wa mapato, Watendaji hawa wa Kata na Vijiji ndio wanaokusanya mapato na wanakusanya mapato katika mazingira magumu sana. Naweza kutoa mfano mmoja tu, katika ukusanyaji wa mapato wa kodi ya jengo. Kodi ya jengo ilikuwa ni ngumu sana kuikusanya kwa upande wa TRA, lakini Watendaji wa Kata na Vijiji waliweza kukusanya kodi ya jengo vizuri na wakafikia malengo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni nini Serikali ifanye; naiomba Serikali yangu kupitia Wizara ya TAMISEMI, namwomba Mheshimiwa Ummy Mwalimu aweze kuwasaidia watendaji wa kata waweze kupatiwa pikipiki kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa maendeleo katika kata zao. Hii itaweza kuwafanya watendaji hawa wafanye kazi kwa kujituma.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali yangu iangalie ofisi zao. Ofisi zao zinatia aibu, hazifai. Mimi mwenyewe nikiwa Mtendaji wa Kata siku moja mvua ilinyesha, nilitaka kuangukiwa na lile boma. Kwa hiyo, mimi mwenyewe ni shahidi mkubwa, ofisi zinazotumika na wao ni haya majengo ambayo ni ma-godown. Kwa hiyo niiombe sasa Serikali waweze kuwasaidia Watendaji wa Kata waweze kupata ofisi nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiangalia Watendaji wa Kata hawa ndio wakurugenzi kwenye kata zao. Niiombe Serikali iangalie namna ya uendeshaji, watendaji waweze kupata motisha ya kila mwezi kama wanavyopata waratibu wa elimu kata. Ukiangalia mtendaji huyu anafanya kazi katika mazingira magumu. Naiomba Serikali kwa uchungu mkubwa, wawaangalie sekta hii ya utawala.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Waziri, Mheshimiwa Ummy, yeye mwenyewe amekuwa shahidi wa watendaji, wanalia kila siku awatazame. Naamini dada yangu, mtani wangu, Mheshimiwa Ummy, kwa namna anavyojua kuchapa kazi mwaka huu wa 2021 kilio cha watendaji kitakwenda kufutika. Namwomba mtani wangu, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, asiniangushe.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)