Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Dr. Christina Christopher Mnzava

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia kwenye bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kwanza napenda nimpongeze sana dada yangu Ummy Mwalimu kwa kupata nafasi ya kutumikia katika Wizara hii ya TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine nimpe pole kwa sababu wizara hii ni wizara ambayo imebeba wizara nyingine nyingi. Elimu ipo kule, afya ipo kule, kilimo kipo kule, kila kitu kipo kule, lakini naamini kwa jinsi ambavyo anafanya kazi, anachapa kazi pamoja na timu yote ya TAMISEMI naamini Insha’Allah Mwenyezi Mungu atamsaidia kama alivyofanya vizuri kwenye Wizara ya Afya, basi na TAMISEMI atafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika bajeti iliyopita nimeona kwamba Wizara ya TAMISEMI iliidhinishiwa jumla ya trillion 5.26, lakini fedha ambayo ilitolewa mpaka inafika Februari, 2021 ilikuwa ni trillion 2.92. Ukiangalia ukubwa na majukumu makubwa ya Wizara ya TAMISEMI kwa fedha hii ambayo ni sawa na asilimia 39.8 haitoshi kukidhi yale yote tumeyazungumza mahali hapa. Waheshimiwa wengi wanalalamika kuhusu maboma wanasema kuhusu miundombinu ya vituo vya afya, miundombinu ya TARURA kwa kweli kwa kiasi hiki cha fedha hakitoshi kukidhi yale ambayo tunayatamani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana kuna Mbunge mmoja alichangia akasema ikiwezekana iletwe kanuni humu Bungeni au sheria ya kuishinikiza mamlaka inayohusika kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, itoe kadri ambavyo tumepanga.

Mheshimiwa Spika, katika sekta ya afya tumeona Wizara imejitahidi sana hospitali nyingi zimejengwa takribani 99 katika halmashauri lakini vituo vya afya 487, Hospitali za Kikanda tatu lakini haitoshi zahanati takribani 1,198. Pamoja na kujenga vituo hivyo lakini mahitaji bado ni makubwa sana ukilinganisha na jiografia ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika hospitali ambazo zimejengwa au zimekwishajengwa bado kuna changamoto ambazo zinajitokeza, miundombinu bado haijakamilika. Hiyo haitoshi, bado wafanyakazi, kwa sababu huwezi kujenga Hospitali ukaacha kupeleka watenda kazi. Kwa mfano, katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga tuna hospitali ambayo kimsingi haijakamilika bado inafanya huduma za OPD, lakini bado tuna maboma ya vituo vya afya na zahanati 42 ambayo mpaka leo hii hayajakamilika, mengine yameanza kujengwa toka mwaka 2012, 2013 na 2014, mpaka sasa hivi hayajakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nadhani katika bajeti hii na natamani sana nisitoe shilingi ya Waziri kuhusu haya masuala ya kumalizia majengo ya maboma. Yale maboma yana muda mrefu kama Butini kule, Kuni na sehemu zingine nyingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Sinyanga, hayajakamilika kwa muda mrefu. Tuliwahamasisha wananchi wetu, wakajitolea nguvu zao wakajenga yale maboma, lakini yamefika kwenye lenta mpaka sasa hivi bado hayajakamilika. Basi naomba katika bajeti hii inayokuja Serikali ione umuhimu wa kuweza kumalizia maboma haya na kuweza kuwatia nguvu wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kujenga vituo vya afya, hospitali, zahanati na kuweka miundombinu tuna wafanyakazi ambao tunawahitaji katika maeneo yale. Hata hao wachache waliopo kwa kweli tunahitaji tuwakumbuke kama Serikali. Wafanyakazi wengi madaraja hayapandishwi, wafanyakazi wengi haki zao za kimsingi kama fedha ya likizo,matibabu wengi wao wengine hawapati. Tufike mahali tuangalie tuwape motisha hata ng’ombe unapomkamua maziwa ni lazima umpe mashudu. Wafanyakazi wanafanya kazi katika mazingira magumu sana hasa sekta ya afya pamoja na Walimu wote ambao wanafanya chini ya TAMISEMI. Tunajua mazingira ambayo ni magumu, sehemu zingine hata usafiri haufiki. Sehemu nyingine kutoka Makao Makuu ya Wilaya kwenda kwenye kituo anachofanyia kazi ni karibia km100, 110. Kwa kweli inasikitisha sana unakuta mfanyakazi anafanya kazi peke yake katika zahanati lakini stahili zake anazostahili kuzipata hazipati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kwasababu inahusika na wafanyakazi wa Idara ya Afya wengine, inahusika na walimu, inahusika na Watendaji wa Kata, Watendaji wa Vijiji ione utaratibu wa kuwapa maslahi yanayostahili watumishi wetu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana. Ahsante Dkt. Mnzava.

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika ni dakika tano tu?

SPIKA: Sasa Mheshimiwa Dunstan L Kitandula

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nashukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)