Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Awali ya yote, nami namshukuru Mwenyezi Mungu kuwepo mahali hapa wakati huu. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Serikali za Mitaa, kwa misingi hiyo, mambo mengi tunayoongea haya tulipata nafasi ya kuyajadili katika ngazi ya Kamati.

Mheshimiwa Spika, niendelee kushukuru katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali kwa maana ya fedha iliyotoa…

SPIKA: Nawaomba Wabunge ambao mmesimama upande huu, mnaopiga soga, kwanza mkae kwenye viti vyenu ili uchangiaji uweze kuendelea vizuri.

Mheshimiwa Kapufi, endelea.

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali kwa maana ya lile zoezi la ukarabati wa shule kongwe. Zoezi hili limekwenda vizuri. Kote tulikopita; Jangwani, Azania, Kilakala, tumeona kazi nzuri iliyofanyika. Pamoja na kazi nzuri hiyo, changamoto hazikosekani, ni pamoja na eneo hilo la force account kama walivyozungumza Wajumbe wengine.

Mheshimiwa Spika, rai na ushauri wangu kwa Serikali, force account linaweza likawa ni jambo jema, lakini tusipojikita kwenye thamani ya fedha, suala la force account naliona lina matatizo pia. Tuliweza kupita kwenye shule moja, kama sikosei kama siyo Kilakala itakuwa ni Mzumbe; jengo la nyuma wataalam walishindwa kutindua cement. Walishindwa kutindua sakafu kwa sababu ya uimara wake, kiasi kwamba wakaamua kuiacha ilivyo.

Mheshimiwa Spika, sasa kuna baadhi ya majengo yanajengwa leo, kesho sakafu ni mbovu. Narudia kushauri suala la thamani. Tusipojikita hapo, tutajikuta tuna idadi kubwa ya vitu vilivyotengenezwa vyenye ubora hafifu. Naomba sana hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo, mimi ni Mwenyekiti wa Chama cha Kibunge cha Idadi ya Watu na Maendeleo. Kwa nyakati tofauti tumekuwa tukikuita kushiriki katika semina zetu. Kama Mwenyekiti wa Chama hicho, nataka kusema nini kwenye Bunge hili? Idadi ya watu siyo tatizo, lakini ukiwa na idadi kubwa ya watu ambao ni tegemezi, tatizo linaanzia hapo. Tafsiri yangu ni nini? Leo tutaishia kutamani kujenga madarasa mengi, kuongeza madawati, lakini bila kwenda kuzingatia suala la idadi ya watu, kwa sababu kwa kupitia idadi ya watu ndiko huko ambako tunaweza tukapanga mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikilisema hilo namaanisha nini? Unapokuwa na kundi kubwa la watu ambao ni tegemezi na wachache ambao ni wazalishaji, hapo lipo tatizo; lakini kwa maana ya idadi ya watu na maendeleo, bado inaweza ikatumika vizuri ikawa ni chanzo cha maendeleo pia. Ikitumika vizuri! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikilisema hilo naendelea kumaanisha nini? Tukijikita kwenye kujua idadi ya watu, leo hatuna sababu ya kukimbizana na kufanya mambo kwa design ya zimamoto. Unajua kabisa tuna idadi hii ya watoto ndani ya muda huu watatakiwa kufika shuleni, ndani ya muda huu watahamia hapa, na hapa na watakwenda pale. Kwa hiyo, mipango yetu yote italiangalia hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaendelea kushauri, katika hilo, tukiwa na idadi ya watu, bado mimi naweza nikasaidia kuishauri Serikali, tunafanya nini katika hili? Ni pamoja na kutoa elimu. Tusiache elimu kwa watoto wa kike. Mtoto wa kike tunapompa elimu maana yake ni nini? Kwanza ule muda atakaokaa shuleni na akapewa elimu nyingine ya kumsaidia kuepuka mimba za utotoni na ndoa za utotoni inatusaidia kuepuka kuwa na idadi ya watu wengi ambao baadaye wanakuja kuwa tegemezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitoke hapo. Wengi wameongelea habari ya TARURA. Namkumbuka Marehemu Baba wa Taifa, alisema hivi, “ukiwa kiongozi, ukapita mtaani, ukamwona mtu mmoja labda hana chakula, yule hana nguo, mwingine hajapata dawa hospitali, kiongozi unatakiwa kusema, huu ni mzigo au msalaba wangu.”

Mheshimiwa Spika, tafsiri yake ni nini? Leo ukienda kwa mfano Manispaa ya Mpanda, ule mji siyo tu kwamba barabara hazipo, lakini kwa mvua zinazoendelea kunyesha tumetengeneza mitaro. Kwa hiyo, TARURA wasipoongezewa fedha ile shida iliyokuwa inajitokeza ya mitaa ambayo barabara zake hazieleweki, tunakuja kwenye tatizo lingine, nyumba za wananchi wetu zimekuwa zikining’inia.

Mheshimiwa Spika, leo ukipita Mbunge, kama nilivyosema, Baba wa Taifa alikuwa anasema huu ni mzigo wangu, nami kama Mbunge, japo ule ni mzigo wangu, lakini nimetimiza haki yangu ya Kikatiba ya kulisemea suala hilo hapa Bungeni. Kwa hiyo, nisaidieni kunitua mzigo wataalam ninyi kwa sura ile iliyopo ya barabara pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili Mtendaji Mkuu wa TARURA ni mtu rahimu, lakini peke yake bila kumpa fedha atafanya nini? Kwa hiyo, naomba sana. Wakati wote tukipiga kelele TARURA iongezwe fedha, tunaishauri nini Serikali katika suala la kuongeza fedha eneo la TARURA? Wapo wanaozungumzia labda kwenye miamala ya simu tukiongeza kidogo hapo, sasa wataalam nendeni huko mkatusaidie kwamba chanzo gani kingine tunaweza tukakibuni kikatusaidia watu hao wakapata fedha ili wakati tunatafuta haki na wajibu uwepo pia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa eneo la elimu; mimi kwangu Katavi ni bahati mbaya yale maeneo yanasomeka kama maeneo ya pembezoni. Kipindi cha nyuma wakati wa Awamu ya Nne ilikuwepo mikakati ya makusudi ili kuikomboa mikoa ya pembezoni. Leo maeneo yetu yale, kwa mfano, ukiacha tatizo la barabara, leo unaweza ukakuta hata kama mmeipatia fedha Halmashauri jirani ya Nsimbo kwa barabara moja, mfano barabara ya kutoka Mpanda kwenda Mtapenda, barabara ile ukiwa umeipa Halmashauri ya Nsimbo fedha, wakati yule mtu lengo lake aje mkoani nami wa Manispaa hujanipa fedha na daraja halipitiki, bado ile thamani ya fedha hutaiona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hayo mambo yanafanyika maeneo mengi. Tanganyika likewise; unakuta mwenzangu amepewa fedha lakini hawezi kuunganika kuja mjini. Barabara za kuja mjini hazipitiki. Kwa hiyo, naomba sana hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la elimu kama nilivyosema, kuna mazingira ambapo baadhi ya watendaji; walimu, mimi mwaka 2014 ndiyo mara ya mwisho kupata walimu wa Shule ya Msingi. Mpaka leo sijawahi kupata walimu wa Shule ya Msingi. Walimu wa Shule ya Sekondari unaweza ukaletewa wanne. Kwa sababu sisi ni mikoa ya pembezoni, inafika mahali wengine wanahama, kwa hiyo, kuna shida kubwa katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la afya, wengi wameongelea. Nami pale Manispaa ya Mpanda nina kituo kimoja tu cha afya. Sasa unapokuwa na kituo kimoja, hospitali ya mkoa haijaisha, mnafanya tunakuwa pembezoni zaidi. Tungeweza kupunguziwa upembezoni huo kwa kusogezewa huduma hizi karibu na maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafahamu eneo la miradi mingineyo, sisi leo tunakwenda karibia awamu ya pili upande wa barabara za lami. Sisi ni Manispaa. Manispaa nyingine wanabahatika kupewa kilometa chache za lami, lakini Mpanda sijui tumesahaulika katika nini? Naomba nalo hilo lijaribu kuangaliwa.

Mheshimiwa Spika, mara ya mwisho tulipiga kelele, hata fedha tu za maendeleo kwa maana ya Mpanda Manispaa hatukuletewa. Ni baada ya kupiga kelele ndiyo tukaletewa fedha hiyo. Ni bahati mbaya, kuna kipindi fedha ikipelekwa ambayo leo ni Tanganyika, kipindi hicho ikiitwa Mpanda kama sisi; au ikipelekwa maeneo mengine, watu wa Manispaa tunaonekana tumeletewa fedha. Hilo tatizo limetuathiri sana. Mgao kwa maana ya Manispaa, tumeathirika sana katika eneo hilo. Kwa hiyo, naomba, kama nilivyosema upande wa walimu na mambo mengine ya namna hiyo, naomba sana tujaribu kuzingatiwa hapo.

Mheshimiwa Spika, nimalizie, kipindi cha nyuma walikuwa wanasema usiniletee biashara ya nyanya. Tafsiri yake ilikuwa nini? Maana yake katika ubovu wa barabara, unaweza usiifikishe nyanya sokoni. Leo hii katika mazingira ya barabara nzuri, hata nyanya bado ni biashara. Kuna maeneo mbalimbali, Ilula huko na kwingineko, miji imekua, biashara ya nyanya imesababisha maendeleo ya watu. Kwa hiyo, hata ile kauli iliyokuwa ya kubeza biashara ya nyanya imetoweka baada ya uwepo wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)