Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Agnes Mathew Marwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia bajeti hii. Kwanza nampongeza sana dada yangu, Mheshimiwa Ummy kwa kuteuliwa. Naamini kabisa wewe ni jembe, unaweza na yale mazuri yote yaliyoanzishwa naamini kabisa utayaboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini kabisa hapo ulipo presha inakupanda, unasema, huyu ndio Agnes wangu za zamani! Hivi kweli nini kinaendelea? Ila mimi ni Agnes mpya, nimefundwa na wewe, sasa hivi niko vizuri, usiwe na wasiwasi. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, dada yangu Mheshimiwa Waziri Ummy, , kama vile ulivyokuwa unafanya ziara kipindi kilichopita, nakuomba sana, ukipata nafasi dada yangu njoo Mkoa wa Mara, ikiwezekana niite nami nikuoneshe baadhi ya vichochoro kule kwetu vijijini; Wilaya za Serengeti, Rorya, Tarime, Bunda, Musoma Vijijini, Mwibara na kwingine uone jinsi barabara zetu zilivyokuwa mbovu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivi ili unielewe kwamba TARURA wana mzigo mzito sana. Waheshimiwa Wabunge wenzangu, bajeti ya TARURA ikiletwa ndogo kwa kweli inabidi tumrudishe kidogo Mheshimiwa Waziri aende akachakate ili airekebishe iongezwe. Kwa sababu TARURA wamepata mzigo mkubwa sana, lakini kutokana na kazi zao wanazozifanya, kwa kweli huwezi ukawalaumu kwa bajeti wanayopewa. Bajeti yao ni ndogo sana.

Mheshimiwa Spika, haiwezekani kubeba jukumu la kujenga kwenye mitaa na bajeti waliyopewa iwe ndiyo hii ambayo tumeiona, halafu tuseme kwamba TARURA watafanya vizuri, siyo kweli. Tutabaki kuwalaumu kila siku TARURA bila kujua tatizo liko wapi? Tunapaswa kwanza kutatua tatizo halafu baadaye tuone utendaji kazi wao ukoje?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nakuomba sana dada yangu, Mheshimiwa Ummy, jipinde sana uangalie kuhusiana na hili suala la TARURA. Siku ukirudi hapo mezani, basi utuelezee vizuri hili suala limekaaje na bajeti yao umeirekebisha vipi?

Mheshimiwa Spika, pia namshukuru mama yetu, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu. Kwa kweli hotuba yake ya jana ilikuwa nzuri sana. Binafsi nilifurahi kusikia akisema kwamba ataboresha mishahara ya wafanyakazi. Kwa kweli wafanyakazi hawa mama yetu wana imani sana na wewe. Siyo tu kwamba wana imani sana na wewe kwa sababu eti utawaongezea mishahara au kuboresha mishahara yao. Wana imani kubwa kwa sababu utendaji kazi wa mama wanaujua toka kipindi kilichopita akiwa na baba yetu Hayati JPM. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naamini kabisa wafanyakazi wana imani na wewe mama, kaa vizuri mama, angalia vizuri, chakata chakata na Wizara yako, hawa wafanyakazi kama ulivyosema nao wafurahi, kwa sababu kila kukicha bajeti zinazidi kubadilika na hasa bajeti za kifamilia zinakuwa kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, kwa upande huo wa wafanyakazi, nakwenda kwa Madiwani. Ndugu zangu, Wabunge wezangu, Madiwani wetu ndio wanaotulindia magoli. Wana kazi kubwa sana. Bila Diwani wewe ukitoka hapa Bungeni ukienda, unamwuliza Diwani, sehemu fulani kuna nini?

Mheshimiwa Spika, sehemu fulani kuna tatizo gani? Huyo ni Diwani, naye ndio yuko kule muda wote. Mtu akiugua anaenda kumdai yeye Diwani; akitokea Mjumbe amekuja; wale ambao si mnajua tena, Wajumbe noma, lakini Diwani anamtuliza yule Mjumbe wako. Pia hawa Madiwani ndio wametuweka sisi madarakani na ndio wameiweka Serikali hii madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa maana ya kwamba wao ndio wanaishi moja kwa moja kwa siku zote kule Majimboni kwetu au kwenye Kata zao na wananchi wetu. Kwa hiyo, ukweli ni kwamba Madiwani wanapaswa kuongezewa posho zao, kwani hazitoshi, hazikidhi mahitaji yao, kwa kweli wanapata kiasi kidogo sana ukilinganisha na majukumu waliyonayo.

Mheshimiwa Spika, namwomba sana dada yangu, Mheshimiwa Waziri Ummy, hili suala sasa aliangalie zaidi. Ikiwezakana jamani, kwenye Wizara basi mwangalieangalie, kwa sababu mmeshaona kule kwa Wakurugenzi kuna shida, basi mlipe moja kwa moja kutoka Wizarani wale Madiwani angalau wajue kwamba tuna mshahara wetu unatokea huku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hata kwangu, Mkoa wa Mara ni kati ya mikoa ambayo ni wahanga wa Madiwani kukopwa. Jamani, kweli tunawakopa Madiwani ambao ndio wanaofanya kazi kubwa sana. Hata huyo Mheshimiwa Mkurugenzi mwenyewe anamtegemea Diwani kule chini na Mheshimiwa DC anamtegemea Diwani kule chini, lakini bado. Siyo tu kwamba wanawakopa, hawajatuambia hizo fedha wanazowakopa ziko wapi? Wamepeleka wapi?

Mheshimiwa Spika, nakuomba dada yangu, Mheshimiwa Ummy, ukienda kawaangalie hawa Wakurugenzi, ukawafanyie ukaguzi. Utakuta uharibifu mwingi sana na upotevu mwingi sana wa fedha ambao wanaufanya na hasa pale wanapowafanyia uonevu Madiwani. Kwa kweli haikubaliki, Wabunge wenzangu, haikubaliki, tukatae kabisa wasiwaonee hawa Madiwani.

Mheshimiwa Spika, kipekee niende moja kwa moja kwenye suala la shule. Shule zetu na hasa za vijana wetu wa kike zimekuwa ni nzuri sana ambapo kwa sasa vijana wa kike wamejitahidi, kiasi fulani kwa kweli wamepanda katika ufaulu, wameanza kuwa na ufaulu mzuri, lakini changamoto inayokuja ni pale ambapo vijana wetu wa kike wengine ambao hawawezi ku-afford kupata taulo za kike, inawapa shida, wanapata shida.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali yangu sikivu, moja kwa moja kama vile tunavyoweka bajeti nyingine za shule kwa watoto wa shule kama watoto wa kiume wanavyowekewa zile packages zao, basi tuangalie na kwa watoto wa kike wawekewe moja kwa moja. Kama vile ambavyo Serikali inakuwa imewalipia ada, basi waangalie pia na kwa hawa watoto wa kike wawekewe ili wale watoto ambao hawajiwezi, umri ambao wanakuwa wameanza kupata hedhi, basi waweze na wao kujiangalia kwamba wanaweza kusoma na hawawezi kupata matatizo madogo madogo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante.