Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Awali ya yote nitumie nafasi hii kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Manaibu wake wawili, lakini vilevile na wataalam. Pia nitumie nafasi hii kukupongeza wewe kwa kweli kwa jinsi ambavyo unatuendesha ndani ya Bunge hili ugeni wangu huu mpaka nafarijika. Kwa muda mchache umenipa nafasi mara nyingi na wananchi wangu wanayaona haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitajielekeza katika maeneo machache sana; eneo la kwanza ni eneo la mabonde na mafuriko katika Mkoa wa Dar es Salaam. Hili ni tatizo sana, hivi pia sasa hivi tunazungumza ni nyakati za mvua kule wananchi wanalia sana. Niliwahi kusema kidogo kwenye eneo hili, lakini niseme tu kwamba mabonde sasa haya, kwanza niipongeze Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu pia, imefanya vizuri sana kwenye eneo la Mto Msimbazi, lakini pia hata kwenye Mto Jide pale ndani ya Wilaya yetu ya Ubungo ndani ya Jimbo la Rafiki yangu kaka yangu Proresa Kitila Alexander Mkumbo upande wa Ubungo, lakini bado tumebakiwa na Mto Mbezi. Naiomba sana Serikali ijielekeze vizuri ili tuone sasa mito hii inapanuka, taasisi zetu zinaondoka sasa na mafuriko. Sasa hivi tayari Shule ya Msingi Msigani pale inaondoka, Shule ya Msingi Matosa inaondoka, kwa hiyo na nyumba nyingi za wakazi wetu zinakwenda. Hivyo ni lazima, kwa sababu dhima yetu mojawapo ni kukuza uchumi pamoja na maendeleo ya watu. Kama watu hawaishi vizuri hawana maisha bora, nyumba bora maana yake tunaweza tukashindwa kwenda kwenye mpango wetu ule wa tatu ambao tumetoka kuujadili siku si nyingi.

Mheshimiwa Spika, miradi ya maboresho ya miji; Waheshimiwa Wabunge wengi wa Mkoa wa Dar es Salaam wamezungumza juu ya DMDP II, Dar es Salaam Metropolitan Development Programme II. Ya kwanza ilifanya vizuri sana, tumeona Dar es Salaam inang’aa kwa mataa mengi, Dar es Salaam inang’aa kwa barabara nzuri nyingi. Niseme ukweli Hayati alivyopita tarehe 24 ndani ya Dar es Salaam katika ziara yake alipita pale Jimboni Kibamba na nilipata bahati ya kusema kidogo, katika matatu niliyosema ukweli aliyakubali yote.

Nilisema kitakwimu ndani ya mzunguko wa barabara zinazozidi zaidi ya kilomita 350 ni kilomita tano tu ndiyo zenye lami katika Jimbo la Kibamba. Hii si sawa na ukweli Waheshimiwa Wabunge wengi hasa zaidi ya 40 na Manaibu Waziri na Mawaziri zaidi ya 10 wanaishi kwenye hili Jimbo. Naomba kabisa mnisaidie ndugu zangu Jimbo limekaa kwenye hali mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe na Waheshimiwa Wabunge wamesema huu mradi wa DMDP II naomba utoke huko uliko kama umesimama ili uje utuokoe. Wakati tunaomba kura za Mheshimiwa Rais aliyepo sasa hivi akiwa anagombea kama Makamu wa Rais, lakini na Waheshimiwa Wabunge tulionyeshwa mtandao wa barabara kilomita 107 za ndani ambazo chini ya TARURA kupitia DMDP II na wananchi wakafurahi, wakaona sasa ile hali ambayo ilikuwa inawasababisha wajifungue barabarani kwa sababu ya njia nyingi kuwa za tope, sasa wanaenda kuishi katika maisha yaliyo bora.

Mheshimiwa Spika, niombe sana, huu mradi kwetu ni muhimu sana ndiyo utaenda kuwaokoa wana Dar es Salaam, lakini mpaka sasa tumeshamaliza bajeti yetu ya TARURA katika ngazi ya Mkoa na niliona takriban kilomita 60 zimewekwa pale, nikaanza kufurahi sana, lakini sijui kama kweli kutakuwa na sintofahamu, niombe sana kama patakuwa na nafasi ya Mheshimiwa Waziri kwenye hili, kama anaweza kuligusia kidogo ili tuweze kuona kama kweli hii DMDP II inakuja Dar es Salaam au haiji.

Mheshimiwa Spika, natamani pia niseme kidogo juu ya madeni ya muda mrefu na hasa kwa watumishi wa umma. Profesa wa Moshi Vijijini, mzee wangu alisema vizuri asubuhi, nikasema ananinyang’anya ninalotaka kusema lakini akaelekea upande mwingine kidogo. Niseme kwamba, tunayo shida kwenye hili eneo, mpaka sasa kwa ripoti ya CAG anatuambia zaidi ya bilioni 190 ndiyo deni ambalo lipo mpaka sasa kama madeni ya watumishi; hapo wapo Walimu pamoja na watumishi wengine.

Mheshimiwa Spika, bilioni 190 si nyingi sana, najua kwa kipindi cha mwaka 2018/2019 tulikuwa na deni au na madeni karibu bilioni 207. Utaona zimepungua kwa bilioni 16, hii niipongeze sana sana Wizara ya Kisekta kwamba imefanya jambo jema, imepunguza bilioni 16 katika mwaka mmoja, kwa hiyo si jambo dogo, wamefanya vyema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo lakini bado kuna kazi ya kufanya. Asubuhi Profesa alishauri kidogo, anasema tunaweza tukaachaacha barabara kule na nini na ni kweli ndiyo ushauri. Sitaki kuelekea kwenye ushauri wa CAG amesema nini, lakini niwashauri tu, tunajielekeza sana, tunayo miradi mikubwa sana ya mabilioni ya namba na ni mizuri kweli na naipongeza ile miradi yote. Hata hivyo, hebu tutafiti jinsi ya mkakati mzuri wa kuondoa hili deni la bilioni 190, tukiamua kweli tunaenda kuzilipa zote.

Mheshimiwa Spika, hizi bilioni 190 ukiwalipa Walimu na watumishi wa umma, maana yake umepeleka hela mtaani. Ukizilipa bilioni 190, maana yake ile hali ambayo tunaitaka sisi sasa ya kukuza uchumi na kuinua maisha ya watu, kweli yanaenda kuwagonga watu. Hii ndiyo dhamira ya Rais, mama yetu Samia Suluhu Hassan, unamwona anataka sasa kuzileta hela mifukoni kwa watu, yaani uchumi wa fedha uende kwenye mifuko ya watu na ndiyo maana ameelekeza hata madeni mengine ya wazabuni na kadhalika yalipwe.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe sana ukiona inafaa hili jambo liende na niseme mpaka sasa tunatenga bilioni sita za kulipa madeni, hazitoshi na bilioni nne ndiyo za ndani (own source), lakini bilioni nne ni za maendeleo, hazitoshi tukapunguze katika baadhi ya vifungu katika mafungu mengine huko, tutoe kwenye posho tulete hapa ili hawa watumishi wa umma waweze kulipwa hizi bilioni 190, sioni kama ni nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme kidogo juu ya Dar es Salaam kuhusu mradi huu wa DART, wa mabasi yaendayo kasi, yuko Mbunge mmoja siyo wa Dar es Salaam lakini nimefurahi sana, wanasimama Wabunge wengine na wenyewe wanaisemea Dar es Salaam, ndiyo maana nafurahi uwepo wa Wabunge wengi wanaoishi Dar es Salaam. Kweli ule mradi ni mzuri na najua unaendelea, lakini hata wewe umewahi kusema, miradi hii inayoendelea miundombinu ni ya kwetu Serikali, hebu tuone jinsi gani huduma hizi zitolewe kwa ushindani. Leo tunayo miundombinu mizuri, tumetoka awamu ya kwanza tunaendelea awamu ya pili ya ujenzi wa miundombinu, lakini ukweli mabasi hayatoshi, wananchi wa Dar es Salaam leo wanateseka kwa nini tumezuia mabasi yale ya vituo vya basi kwenda Mjini Kariakoo. Tumezuia tukisema tunaweza kuwamudu wote waingie kwenye mabasi ya mwendo kasi, haiwezekani! Kwa nini tusiseme ya kijani ni ya Serikali, wengine waje na mekundu, wengine waje na ya njano ili tukashindane kwenye ile barabara.

Mheshimiwa Spika, lakini zaidi niombe sana, leo hii barabara imekuwa ni mateso kwa hata wanaochangia kodi yenyewe. Leo kuna wagonjwa wanapata rufaa kutoka Mloganzila wanaenda Muhimbili, lakini unaambiwa hata yale magari ambayo ni ambulance hayawezi kupita kwenye barabara ile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hiki ni kilio kikubwa kweli, kwa hiyo mgonjwa ambaye sehemu yake ya kodi ndiyo inajenga barabara ile, leo na yeye ili awahi maisha yake apate uhai, inawezekana asipite ile barabara na akafa kabla hajafika kwenye hospitali nyingine! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili ninasema si kwa kubahatisha, ndani ya jimbo langu Hospitali ya Mlonganzila iko hapo, na nilipata bahati kuwatembelea Mwezi Januari, na moja ya kikao changu na menejimenti ya pale hiki kilikuwa kilio chao.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikuombe kwa jinsi ambavyo utakapoona inafaa tupate maelekezo mazuri, siyo sisi viongozi tupite mule wala siyo wengine, haya magari kwa ajili ya usalama wa maisha ya watanzania waishio Dar es Salama wapite kwenye njia ile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, binafsi kwa siku ya leo niliona niyaseme hayo ya mabonde, mafuriko, DMDP ll, eneo la madeni ya Watumishi wa Umma na hili la ushauri na maombi juu ya barabara yetu ya DARTS, baada ya kusema hivyo nakushukuru kwa kunipa nafasi, ahsante sana. (Makofi)