Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Ummy Hamisi Nderiananga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

NAIBU WAZIRI, OFISI WA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kuniwezesha leo hii kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Vile vile niwatakie mfungo mwema wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan Waislam wote duniani na katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Hayati Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuniamini ili niwatumikie Watanzania katika nafasi hii ya Naibu Waziri, Watu Wenye Ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda vile vile niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuamini katika uwezo wangu na kuweza kunibakiza ili niweze kutumikia watu wenye ulemavu, Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile kwakuwa sisi ni watu wenye ulemavu, napenda niendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwateua wenzangu wenye ulemavu kuwa Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu na katika maeneo mengine. Tunamhakikishia tutaendelea kuchapa kazi kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa niende kujibu maswali ambayo yaliulizwa, mojawapo likiwa ni suala la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu na kutatua migogoro yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nipende kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba tumetambua vyama 14 vya watu wenye ulemavu wa aina tofauti na tunaendelea kufanya nao kazi kwa karibu kuhakikisha kwamba migogoro haipo.

Mheshimiwa Spika, vile vile tumefanya chaguzi na tumevisimamia vyama hivi viweze kuiendesha vizuri. Hali kadhalika nimefanya ziara katika mikoa takribani tisa ambapo nimefanya vikao vya kujengeana uwezo na viongozi wa vyama hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lipo pia swali liliulizwa na Kamati kuhusu Mfuko. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshatoa maelekezo ya kuhusu Mfuko, tutaleta pia maelekezo ya ziada hapo ambapo tutakuwa tumepata utathmini utakaoturuhusu sasa kuzindua Mfuko wa Taifa wa Watu Wenye Ulemavu na tutawakaribisha pia wadau waweze kuchangia katika Mfuko huu ili tuweze kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na suala la register ya watu wenye ulemavu na ni eneo ambalo tuliona ni la muhimu sana, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwa haraka sana tumefanya utambuzi wa watoto wenye ulemavu ambao mpaka sasa tumefanya utambuzi wa watoto 28,698 wenye ulemavu, ambao wengi wao walikuwa wamefichwa ndani na sasa wametolewa na tutahakikisha wanasoma kweli kweli.

Mheshimiwa Spika, vile vile kuwepo kwa mwongozo wa utambuzi wa watu wenye ulemavu ambao ni register maalum sasa kwa wale ambao wana umri mkubwa wa ujana na kuendelea, tumeshatoa maelekezo kupitia TAMISEMI tarehe 8 Aprili, 2021 wameshateremshiwa viongozi ili wayafanyie kazi. Nitoe rai waendelee kukusanya takwimu hizo na nitakuwa nafuatilia kwa ukaribu sana katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile suala la asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu; baada ya kufanya tathmini ya kina na kuzunguka katika Mikoa hii niliyoitaja, ya Simiyu, Mara, Dar es Salaam, Kilimajaro na kadhalika. Tumepata maoni ya watu wenye ulemavu na tukaona kwa haraka sana sisi ndani ya Serikali tubadilishe pia kanuni. Hivyo, tumebadilisha kanuni na kwa sasa watu wenye ulemavu zile asilimia mbili zao wataweza kupata kwa mtu mmoja mmoja na wakitaka kikundi mwisho ni watu wawili, wakitaka zaidi sawa, lakini kikubwa sisi tunatii kiu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye hili tutaendelea kujipima kuona namna ambavyo fedha hizi zinakuwa na ufanisi. Mimi binafsi nitoe rai watu wenye ulemavu wapewe fedha ambazo zinaweza kuwaletea matokeo badala ya kupewa fedha kidogo kidogo, wasaidiwe kupata miradi ambayo ni mizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la ajira, mwezi Januari na Februari tuliajiri Walimu 243 wenye ulemavu. Vilevile upande wa Internship tumeingiza Walimu 100. Niseme kwamba, tutaendelea kusimamia upande wa Serikali ajira zote zinazotoka, kipaumbele kiwe ni kwa watu wenye ulemavu na tutawaingiza kwa wingi na kwa kadri ambavyo ajira hizo zitatolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa taasisi binafsi na mashirika kuendelea kuajiri na kuwaamini watu wenye ulemavu kama sisi ambavyo tumeaminiwa hapa na tunafanya kazi hii nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la unyanyapaa na ubaguzi dhidi ya watu wenye ulemavu hususan kwenye eneo la elimu, liliulizwa swali hili. Napenda niseme kwamba, Serikali tunaweka mkazo sana katika kuhakikisha wanafunzi wenye ulemavu wanapata elimu. Kwa mwaka huu wa fedha 2020/2021 tumeshanunua vifaa saidizi 51,339 na tumevigawa katika shule za msingi na sekondari na tutaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho kabisa ni suala hili la unyanyapaa na ubaguzi. Tutaendelea kufanya kaguzi za mara kwa mara kuhakikisha hakuna mtu anayewanyanyapaa na kuwatumikisha watu wenye ulemavu kama tukio lililotokea Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)