Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kupata nafasi ya kufunga dimba kwa leo. Naomba nianze kwa kuwapa pole wananchi wote wa Mkoa wa Singida na hasa Waislam kwa kufiwa na Shehe wetu wa Mkoa na kesho tunakwenda kumzika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze moja kwa moja kwenye hotuba ya Waziri Mkuu, japo imegusa mambo mengi ya msingi, lakini nataka niende kwenye kipengele cha afya hasa katika suala la maboma ya zahanati. Wananchi wetu walihamasishwa sana kipindi cha nyuma kwamba wajenge zahanati kwenye vijiji na vituo vya afya kwenye kata, wakifika hatua ya lenta Serikali itamalizia. Wananchi wangu wa Mkalama walifanya hivyo na tuna maboma zaidi ya 19.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimwambie Mheshimiwa Waziri Mkuu na Wizara zinazohusika, wangetekeleza ahadi hii ambayo waliwaahidi wananchi wetu, kwa sababu wananchi wetu sasa wamevunjika moyo na tukiwaambia mambo mengine ya maendeleo wanakuwa wazito, kwa sababu wanasema mlituambia tujenge, tumejenga na sasa maboma yetu yana zaidi ya miaka saba, mengine miaka mitano, nguvu zao wanazitazama na Serikali imeshindwa kumalizia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbaya zaidi majengo mengine wizara inakuja na ramani mpya, wanasema ramani hii ni nyingine, sasa lile jengo lenu ramani imekuwa ya kizamani. Suala la chumba cha sindano kuchomwa au kupokea dawa wala sidhani kama lina uhusiano sana na ramani. Naomba sana Serikali imalizie majengo haya ili wananchi wetu waendelee na tabia yao nzuri ya kuchangia maendeleo ya Serikali pale wanapoambiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwa haraka suala la watumishi. Tunaweka hizi zahanati, tunaweka majengo mapya, hospitali na nini, lakini watumishi hatuajiri wakati nafasi zipo. Ningeiomba Wizara ya Utumishi zile nafasi ambazo ni replacement tunafahamu kwamba leo kuna watu wanastaafu, leo kuna watumishi wametangulia mbele ya haki, watumishi hao tayari wana bajeti tayari kwenye Wizara, wana mishahara ipo, kwa nini replacement haifanyiki mara moja mpaka kusubiri uje uombe wakati zile nafasi zipo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe wafanye recruitment kwa sababu watu ambao wana sifa tunao wengi, wako mtaani katika wizara mbalimbali, wawe wanasubiri tu ikitokea mtu amefariki, mtu amestaafu, anajazwa moja kwa moja ili inapokuja kuombwa ajira mpya, ziwe ajira mpya kweli siyo zile za replacement ambazo tayari zilikuwa kwenye bajeti. Kwa sababu inakuwa shida sana kuajiri watu kwa sababu ya bajeti, sasa zile nafasi ambazo watu wamefariki kwa nini watu wasiajiriwe moja kwa moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta zahanati ina Nurse mmoja halafu wananchi wanalalamika zahanati inafungwa, Nurse huyo pia ana watoto, ana mume anatakiwa akamhudumie au mke, sasa akitaka kwenda nyumbani akifunga anaanza kulaumiwa, wakati pia yeye ni binadamu ana mambo ya kijamii. Kwa hiyo ningeomba hizi replacement zifanyike haraka, kwa wakati, wala siyo za kusubiri kibali, kwa sababu ni nafasi ambayo ipo na Wizara ya Utumishi ipo, watu wafanyiwe recruitment, wajazwe kwa wakati, inapofika kwa Rais tunaomba ajira ziwe mpya kwa maana ya mpya siyo zile za kujaza nafasi kama ambazo hizi zilizopo sasa hivi ni za kujaza nafasi. Kwa hiyo tuombe zingine mpya ili watu waajiriwe na kazi zipo kwa sababu tumejenga hospitali nyingi hazina watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kwa sababu naenda haraka sana, muda mwenyewe ndiyo wa mwisho, suala la hii miradi yetu ya kimkakati. Tumetengeneza miradi mingi lakini mradi mmojawapo ni wa mwendo kasi Dar es Salaam. Ni mradi mzuri wa kimkakati na hapa kwetu ni mradi ambao tulijua utatusaidia kuondoa suala la foleni Dar es Salaam, lakini leo hii ule mradi umekuwa ni kero, yaani kuingia kwenye mwendo kasi kama una ubavu huwezi, watu wanaanguka wanaibiwa wanafanya nini, niliingia mle juzi nikaogopa wasije wakajua mimi ni Mbunge, wakaanza kuniambia sisi tunateseka na ninyi mpo. Naomba kampuni mbili zifanye kazi kwenye mradi ule, kama haiwezekani basi daladala zile zirudishwe za Posta - Kimara kwa sababu watu wanapata shida sana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)