Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Omar Issa Kombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wingwi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia fursa hii ya kuchangia hotuba ambayo iko mbele yetu kutoka Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile na mimi ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge hili Tukufu na kuweza kuchangia, naomba nichukue fursa hii nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kufika hapa. Vilevile nichukue fursa hii kukishukuru sana Chama changu Chama cha Mapinduzi kwa kuniamini kuweza kupeperusha bendera katika nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Wingwi katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, nichukue nafasi hii kuwashukuru sana Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi wa Jimbo la Wingwi kwa imani yao kwangu. Sambamba na hilo, niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Wingwi kwa imani yao kwangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Ofisi yake kwa hotuba nzuri iliyojaa maono ya viongozi wetu pamoja na Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi. Vilevile nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoanza kuchapa kazi katika kuwatumikia wananchi wa Tanzania. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Wingwi na kwa niaba ya wananchi wa Pemba hatuna shaka hata kidogo kama Wanzanzibar kwamba Muungano wetu upo kwenye mikono salama chini ya Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili amelidhihirisha siku anamuapisha Mheshimiwa Makamu wa Rais alipomwambia aanze kuzifanyia kazi changamoto za Muungano. Hii ni dhahiri kwamba Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ataendelea kuuboresha, kuuendeleza, kuuenzi na kuulinda Muungano wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kiukweli Serikali yetu inafanya jitihada kubwa sana katika kuuenzi na kuulinda Muungano wetu. Kuna mafanikio makubwa ambayo tunayapata sisi Wazanzibar lakini watu wanajitia kuwa hawaoni wala hawasikii wala hawataki kuona mafanikio makubwa ya Muungano wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha uongozi wa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli changamoto 11 zilipatiwa ufumbuzi lakini wanaposimama hawataki kuyasema haya. Changamoto nimeiona, ushauri wangu Mheshimiwa Waziri Mkuu Serikali iweke utaratibu wa kwenda kwenye vyombo vya habari kueleza mafanikio na yale mambo ambayo yanafanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa upande wa Zanzibar ili wananchi waweze kuona na kufahamu na kuelewa waepukane na kupotoshwa. Nasema hili kwa sababu kuna upotoshwaji mkubwa kwamba Serikali haifanyi kitu katika suala la Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niendelee kuipongeza Serikali kwenye mradi mkubwa wa umeme. Nafahamu mradi huu ukikamilika tutaweza kupata huduma hii kwa unafuu mkubwa zaidi. Sasa niiombe Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Serikali, kwa vile nchi yetu tuna pande mbili za Muungano; upande wa Zanzibar na upande wa Tanzania Bara, uandaliwe utaratibu maalum au watueleze ni jinsi gani sisi Wazanzibar tutaweza kufaidika pindi mradi huu utakapokamilika. Licha ya kwamba tunalo Shirika la Umeme kule Zanzibar lakini tunafanya kazi kwa ushirikiano. Niombe wakae meza moja na sisi watuangalie kama wenzao ili tuweze kupata huduma hii itakayokuja katika hali ya unafuu mkubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)