Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon Lucy John Sabu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hoja iliyopo mezani. Nami nitajikita katika uwezeshaji wa wananchi kiuchumi hususan katika ujuzi kwa vijana na ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa juhudi mbalimbali ambazo imekuwa ikizifanya hususan kwa vijana kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi Kitaifa. Kupitia programu hii, nafahamu kwamba Serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kukuza ujuzi kwa vijana na ili waweze kujiajiri na kuajiriwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nikiri kuwa mnufaika wa vijana hawa ambao wamekuwa wakipatiwa ujuzi kupitia vyuo vya VETA hususan kwenye kurasimisha ujuzi lakini pia VETA wamekuwa ni watu ambao wanawasaidia vijana hawa kuwashikiza hususan kwa waajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la vijana hawa kupatiwa ujuzi na kujiajiri ni vitu viwili tofauti. Nikichukulia mfano, tulipokuwa na ziara ya Kamati tulitembelea TIRDO (Tanzania Industrial Research and Development Organization) ambapo tulikutana na vijana ambao wana ujuzi ama ubunifu wameweza kutengeneza taa ambapo zina uwezo hata kama ukiwa nje ya nyumba yako, wame-install program kwenye simu ukai-request kwamba zima ama washa taa hata kama ukiwa nje ya nchi. Changamoto inakuja kumekuwa na vijana wengi ambao wana ujuzi wa aina mbalimbali lakini wanashindwa kujiajiri kwa kukosa mtaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi napenda kuiomba Serikali yangu na kuishauri kwa kuwa tuna Programu ya Kukuza Ujuzi kwa Vijana ije na utaratibu wa kutengeneza fursa za kimkakati. Kwa mfano, tunao vijana ambao wana ujuzi wa ufundi seremala na kuna baadhi ya maeneo ambayo yana upungufu wa madawati, Serikali inaweza ikatengeneza fursa kwa vijana hawa wenye ufundi wa useremala kwa kutengeneza kambi rasmi na kuweza kuchukua vijana hawa kuwapa tender ya kutengeneza madawati kwa kuwapa materials na vitendea kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu Serikali imekuwa ikitoa mikopo kwa ajili ya vijana hususan kwenye Halmashauri zetu. Tunaishukuru Serikali yetu Sikivu, kipindi cha nyuma tulipiga kelele sana Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu makundi yalikuwa yakiundwa na watu kumi kumi lakini tarehe 26 Februari, kupitia Ofisi ya Wizara ya TAMISEMI ililegeza masharti ya mikopo na kuboresha zaidi kutoa nafasi kwamba hata wakiwa vijana watano wana uwezo wa kukopa mkopo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini matamanio ya vijana wenzetu ni kuwa mkopo huu uwe ni wa mtu mmoja mmoja. Kama Serikali imeweza kutoa mikopo kwa mtu mmoja mmoja hususan kwenye mikopo ya vyuo vikuu, naomba na hili Serikali ilifanyie kazi. Hii ni kwa sababu mikopo ya watu kwenye makundi inakuwa ina mambo mengi, kila mtu anakuwa ana interest zake kwenye ideas ambayo wanafanya kwenye biashara husika. Niiombe sana Serikali yetu sikivu iweze kutusaidia kwenye jambo hili ili liweze kuwa la manufaa zaidi kwa vijana wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo yote, niiombe Serikali yetu iendelee kutoa elimu kwa vijana wote ambao wanachukua mikopo kwenye Halmashauri. Nasema hivi kwa sababu vijana wanakuwa na interest tofauti tofauti, hivyo, mkopo unavyochukuliwa bila elimu ya kutosha matumizi yanakuwa tofauti na marejesho yanashindwa kufikiwa kwa wakati muafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja iliyopo mezani. Ahsante sana. (Makofi)