Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Ally Anyigulile Jumbe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Dunia na Afrika nzima inashangaa na kustaajabu ukuu wa Mungu ambao amebariki Taifa hili mpaka sasa hatujaingia kwenye lockdown na tunakaa kwenye Bunge hili. Naomba tuendelee kumshukuru Mungu na sifa na utukufu vimwendee yeye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba Watanzania na Wabunge wote tusijisahau, haya yanayotokea ni kwa sababu ya mtu mmoja tu, Mungu huwa anamwangalia mzawa wa kwanza wa familia, matendo yake ndiyo yanayoshuka chini. Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alimwamini Mungu, alisema Watanzania hatuna haja ya kuingia kwenye lockdown hata kama Mataifa mengine yanaingia twende tumuamini Mungu na yale maneno naomba tuendelee kuyaishi ndiyo yaliyotufikisha hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu haya yote pia Rais Dkt. John Pombe Magufuli hakufanya yeye peke yake, alikuwa na msaidizi wake ambaye alikuwa pia anamuonesha na kushauriana naye, naye si mwingine, ni mama yetu kipenzi, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan. Huyu mama ndiye yule ambaye aliahidiwa kwamba atampokea kijiti Mussa, sasa Mussa amebaki yeye anaendelea na ndiyo maana naomba leo niwasalimie kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

WABUNGE FULANI: Kazi iendelee.

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Waziri Mkuu anafanya kazi kubwa sana na anachapa kazi usiku na mchana. Ndiyo maana katika yote niseme naunga mkono hoja hii ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaendelea, nilipenda niongelee mambo mengi sana lakini nimejikuta nipo kwenye masikitiko makubwa sana. Kata kumi za Wilaya ya Kyela leo ni siku ya tatu wananchi wako kwenye maji, wako kwenye mafuriko. Naomba nichukue nafasi hii kuwapa pole, lakini naomba sasa hata kama taarifa hazijafika basi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Maafa kiiangalie Wilaya ya Kyela kwa jicho la huruma. Wilaya ya Kyela Kata kumi za Katumbasongwe, Bujonde, Kajunjumele, Matema, Isaki, Mwaya, Ikama, Ipinda na Makwale. Kata hizi zote wananchi wametoka kwenye nyumba zao, hawana chakula wala mahali pa kulala wako nje na mpaka barabara zote hata barabara yetu ya lami ipo kwenye maji sasa hivi na kuna sehemu imeanza kubomoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana naomba nichukue nafasi hii kusema kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu kuna haja ya kuipendelea Wilaya ya Kyela kwa namna moja au nyingine kwa sababu moja tu. Wilaya ya Kyela ndiyo iko chini kabisa kwenye uwanda, iko mita 450; mvua zote zinazonyesha Ileje, Songwe, Rungwe na Busokelo matokeo yote mabaya yanaelekea Kyela. Hata barabara zilizoko Kyela sasa hivi zimegeuka kuwa mito.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kyela bado haijapata pesa za development kwenye barabara zake. Miaka mitano iliyopita mpaka mwaka huu hakuna pesa hiyo. Naomba sasa Serikali iiangalie Kyela tofauti na sehemu zingine kwani yenyewe iko tofauti na sehemu zingine, iko chini mno. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie suala hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala dogo tu ambalo ni la Kimungu. Kuna watu wanashangaa kwa nini Tanzania hiko hivi? Viongozi wote wanafanya vizuri. Nataka niseme, ndugu zangu, kila Rais aliyetokea Tanzania alikuja kwa mkono wa Mungu na kwa kazi yake maalum. Hakuna Rais aliyekuja kivyake vyake kwa sababu nchi hii imebarikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wa Kwanza alikuja kwa ajili ya Uhuru na kutuunganisha Watanzania wote ili tuwe kitu kimoja. Akafuata Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi; baada ya kuungana Watanzania wote, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi aliona Watanzania mmoja mmoja, hawana uchumi wa kutosha, akatufungua wote, tukapata fedha, tukajifunza kutumia fedha. Nakumbuka kwetu ndiyo wakati ambao watu walianza kujifunza kuvaa viatu, tulikuwa tunaviita Ahsante Salim.

Mheshimiwa Naibu Spika, alipokuja Mheshimiwa Hayati Benjamin Mkapa, akaona kwamba nchi haina fedha, lazima nchi ijikamilishe, Serikali iwe tajiri. Akaifanya Serikali ya Tanzania ikaanza kuwa na uchumi wake na kulipa madeni. Akaja Rais Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete akaifanya Tanzania ijulikane nje. Hiyo ni kazi ya Mungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu walikuwa hawajui hata kwamba Mlima Kilimanjaro uko Tanzania. Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete alitufanya watu wa nje wajue Mlima Kilimanjaro uko Tanzania. Likaja Bulldozer ambalo kazi yake ilikuwa ni kuifanya Tanzania ijitegemee na hapa ndipo tulipofika. Haya hayajafika kwa kudra tu, ni Mungu aliyapanga kwamba yatakuwa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nataka kukishukuru sana Chama cha Mapinduzi. Chama hiki ni chama ambacho Mungu alikibariki, kwa sababu ni chama pekee ambacho kinafuata mifumo ya vitabu vya Mungu. Nimesoma kwenye Biblia; Kutoka 18:21-23 ndiko zilikoanzia nyumba kumi kumi. Maana alisema watu waongozwe na nyumba kumi kumi, elfu elfu na hamsini hamsini.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru sana. Ahsanteni sana kwa kunisikiliza. (Makofi)