Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia kwenye hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nitajielekeza katika maeneo mawili ya lishe na sekta ya Asasi za Kiraia (NGOs).

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza Serikali kwa jitihada kubwa ambayo imekuwa inaendelea kufanya katika kuboresha hali ya lishe nchini pamoja na kutokomeza udumavu na aina zote za utapiamlo. Kipekee kabisa napenda kutambua jitihada kubwa alizofanya Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan, akiwa Makamu wa Rais ambayo ilisababisha yeye kumuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kusaini mikataba ya lishe kwa niaba yake na Wakuu wa Mikoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vivyo hivyo, nawashukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa namna ambavyo wanaendelea kuratibu masuala ya lishe ambayo yanaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu. Wanafanya hivi kwa kupitia maeneo matatu. La kwanza ni kusimamia utekelezaji wa mpango jumuishi wa lishe wa Kitaifa; la pili ni kusimamia vuguvugu la uongezaji kasi ya kuboresha hali ya lishe duniani; la tatu ni kujumuisha jumbe ya lishe katika jumbe za mbio za Mwenge wa Uhuru; na la nne latika kutekeleza viapumbele vya lishe vilivyoweka katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kipekee kabisa napenda kukishukuru Chama changu, Chama Cha Mapinduzi kwa kuwa chama pekee ambacho kimeweka kipaumbele kikubwa katika lishe. Mnaweza mkarejea kurasa za 7, 40, 139-141 ambapo Chama Cha Mapinduzi kimeweka malengo madhubuti ya namna gani itaelekeza Serikali kwenda kuboresha hali ya lishe nchini na kutokomeza udumavu na aina zote za utapiamlo. Waheshimiwa wanaweza kurejea Zaidi kwenye kurasa hizi nilizozitaja, kurasa za 7,40, 139-141. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa Tanzania tuna changamoto kubwa sana ya lishe duni inayosababisha kutuweka katika hatari ya kutokuwa na kizazi na nguvu kazi shindani. Wengi humu tunaongelea changamoto za ajira, lakini ikiwa watoto wetu wana lishe duni na wako dumavu hiyo nguvu kazi na kizazi cha kesho tutavipata vipi? Ndiyo maana ni lazima kutoa kipaumbele kwa ajenda hii ya lishe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie fursa hii kuikumbusha Ofisi ya Waziri Mkuu itamke rasmi ina maoni gani kuhusu janga hili la lishe bora. Ofisi ya Waziri Mkuu itakwenda kufanya nini kuhakikisha kwamba sekta na Wizara zote zinazohusika na suala hili wanakwenda kutekeleza yale yaliyoandikwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo langu la pili la Asasi za Kiraia; napenda kuipongeza sana Serikali kwa wito wa utashi wa kushirikiana na sekta binafsi ili kukuza ustawi wa maendeleo ya jamii na uchumi wa Taifa letu. Hata hivyo, naomba nitumie fursa hii kuikumbusha Serikali kuwa kuna sekta nyingine ambayo nayo inaweza kuchangia katika maendeleo ya Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba kuitambulisha Sekta ya Asasi za Kiraia kwa maana ya NGOs, CSOs na CDOs kwa sababu sekta hii ina sifa zote za kuwa chachu ya kuinua na kukweza dira ya mipango ya maendeleo ya Taifa. Nasema hivi kwa sababu hata kwenye Ilani hii ya Chama Cha Mapinduzi imetambua mchango mkubwa wa sekta ya Asasi za Kiraia, imetambua sekta ya Asasi za Kiraia ni muhimu katika kutekeleza mipango ya maendeleo. Mnaweza mkarejea kurasa za 124 na 128 na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, vivyo hivyo, Chama Cha Mapinduzi ndicho chama pekee ambacho katika nafasi zake za Viti Maalum, kimetenga nafasi ya kuwa na Mwakilishi wa kundi la Asasi za Kiraia. Humu Bungeni niko mimi nikiwakilisha kundi la Asasi za Kiraia kwa upande wa Tanzania Bara, lakini pia yupo Mheshimiwa Khadija Aboud anayewakilisha kundi hili kutoka Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, napenda kuipongeza Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa NGOs kwa kazi kubwa inayofanya kusimamia utekelezaji wa Sheria ya NGOs ya 2019 na kwa mara ya kwanza imeweza kuchakata na kubainisha ni kiasi gani cha fedha kinachoingia nchini kwa ajili ya sekta hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi cha miezi sita tu kati ya Julai, 2020 mpaka Machi, 2021, jumla ya mikataba 178 ilichakatwa na kufanyiwa upembuzi na Ofisi ya Msajili wa NGOs. Iliweza kubaini jumla ya shilingi bilioni 546, narudia; katika kipindi cha miezi sita, Ofisi ya Msajili wa NGOs iliweza kubaini jumla ya 546,758,508,000 ziliingia nchini kupitia NGOs. Kwa hiyo moja kwa moja sekta ya NGOs ina mchango mkubwa sana katika kuendeleza Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mantiki hiyo, nitumie fursa hii kuiomba Serikali itenge bajeti ya kutosha kwa Ofisi ya Msajili wa NGOs na Baraza la Taifa la NGOs ili waendeleze kusimamia utekelezaji na uratibu katika sekta hii muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vivyo hivyo, naomba nikiri kwamba awali nilikuwa na hofu juu ya maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto kumezwa na afya, lakini namshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kulitambua hilo na kuweka Naibu Waziri anayesimamia Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa ajira, Sekta ya Asasi za Kiraia inaajiri watu wengi. Kwa taarifa ya Wizara ya Afya, 2017, katika mashirika 300 tu yalichangia zaidi ya ajira 5,317. Vile vile sekta hii ya Asasi za Kiraia pia ni tanuru ya kuandaa viongozi wa Kitaifa. Viongozi hawa wa Kitaifa ni kuanzia Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan; Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa; Mheshimiwa Waziri, Profesa Kabudi; Mheshimiwa Waziri, Profesa Kitila Mkumbo; Mheshimiwa Waziri, Ummy Mwalimu; Mheshimiwa Waziri, Selemani Jafo; Mheshimiwa Naibu Waziri, Olenasha; Mheshimiwa Naibu Waziri, Ummy Nderiananga; Mwanasheria Mkuu, Mheshimiwa Profesa Kilangi. Kwa hiyo hii moja kwa moja inaonesha kwamba sekta hii inatoa mchango mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nitumie fursa hii kuiomba Serikali, vile ilivyowakaribisha sekta binafsi waandae mpango kazi na sisi pia sekta ya Asasi za Kiraia tupewe fursa kama hiyo tukaribishwe rasmi, maana tupo tayari kushirikiana na Serikali na tayari tunaandaa mpango kazi ambao tutapenda kuuwasilisha kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa, kabla ya kwenda kumwona Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan, kama ambavyo nilishaomba awali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia, ndani ya Bunge hili tuko Wabunge wengi sana ambao tumepitia sekta ya Asasi za Kiraia. Hivyo, naona tunayo fursa ya kuanzisha kikundi cha Wabunge Vinara wa AZAKI kwa maana ya NGOs, CBOs na CSOs ili kuimarisha utekelezaji wa mwongozo, uhusishwaji wa Asasi za Kiraia katika shughuli za Kamati ya Bunge na huu ni mwongozo ambao umeandaliwa na Bunge hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. Nashukuru sana kwa fursa hii. (Makofi)