Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Agnesta Lambert Kaiza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, siku chache zilizopita kupitia Bunge lako hili Tukufu tulikaa na kujadili na kupitisha Mpango wa Serikali wa Miaka Mitano. Yote ambayo tumeyapitisha, yote ambayo tumeyajadili na leo hii tupo kujadili na kupitisha bajeti za Wizara mbalimbali, tutambue kwamba ufanisi wa jambo hili hauwezi kabisa kupatikana ikiwa wananchi wetu hawana afya njema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Ripoti ya CAG inayohusiana na mashirika ya umma, ukurasa namba 128, utaona jinsi ambavyo CAG kwa uwazi kabisa ameweza kuonesha ukosefu wa mamlaka ya kudhibiti bei za dawa pamoja na vifaa tiba. Tunatambua na tunafahamu kwamba, Watanzania wote au niseme asilimia kubwa ni maskini, si wanyonge, lakini ni maskini. Watanzania hawa hawawezi kabisa kumudu bei ghali za dawa pamoja na vifaa tiba. Kutokuwepo kwa chombo hiki cha kudhibiti bei za dawa pamoja na vifaa tiba kumesababisha wafanyabiashara wanaouza dawa pamoja na vifaa tiba kujipangia bei kadiri wao wanavyoona inafaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo sababu kuu mbili zinazosababisha dawa na vifaa tiba kuwa na bei ya juu sana. Serikali yenyewe ambayo inapaswa kuwa namba moja kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma nzuri za afya kwa bei nafuu ndiyo ambayo imekuwa ikisababisha wafanyabiashara kupandisha bei za dawa pamoja na vifaa tiba kwa sababu katika hospitali zetu hakuna dawa kabisa. Serikali hii ambayo siku zote inajinasibu kwamba imekuwa ikitekeleza yale ambayo imepanga imekuwa ni namba moja kusababisha wananchi wetu kushindwa kumudu dawa hizi ambazo nimezielezea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa msingi huo basi, naomba niseme hivi, tunayo MSD ambayo kazi yake ni kununua na kusambaza dawa pamoja na vifaa tiba katika hospitali zetu, lakini kumekuwepo na upungufu mkubwa wa dawa hizi ambazo naelezea pamoja na vifaa tiba. Ni kwa nini basi kumekuwepo na huu upungufu? Ni kwa sababu Serikali imekuwa ikikopa fedha kutoka MSD na hairejeshi kwa wakati na wakati mwingine hairejeshi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukifuatilia Ripoti ya CAG ya mwaka 2017, 2018 na 2019, Serikali hii ilikuwa inadaiwa shilingi bilioni 53.63. Tungetegemea kwamba katika Ripoti ya CAG ya sasa tuone ni jinsi gani Serikali imeweza kupunguza, kama siyo kumaliza kabisa deni hilo ambalo ni kubwa sana. Hata hivyo, katika ripoti hii mpya ya CAG inasema, Serikali mpaka sasa inadaiwa kiasi cha shilingi bilioni 256. This is a shame kwa sababu huwezi kuwa inapoitwa leo wewe unazidi kuongeza madeni. Tulitegemea Serikali iwe ndiyo namba moja kuwa na huruma kwa Watanzania hawa. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Eric Shigongo.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka tu kumkumbusha mzungumzaji aliyekuwa anazungumza kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi imechukua hatua za kutosha kabisa za kuimarisha MSD. Kiongozi Mkuu wa MSD kwa sasa alitoka Jeshini. Chini ya uongozi wa Meja Jenerali huyu, MSD imefanya improvement kubwa sana ikiwemo kuanzisha kiwanda chake yenyewe cha kutengeneza paracetamol. MSD inatengeneza paracetamol zake yenyewe na imeweza kushusha cost za kufanya dialysis katika nchi yetu. Kwa hiyo, kusema kwamba, ni shame sio jambo sahihi, ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Agnesta Lambert, unaipokea Taarifa hiyo?

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa hiyo siipokei kwa sababu nilichokitaja hapa kwamba Serikali inadaiwa shilingi bilioni 256 ni kutokana na Ripoti ya CAG.

Sasa Mheshimiwa Mbunge pale kama anadhani kusema kwamba wamejenga kiwanda cha kutengeneza Panadol ndiyo iwe sababu sasa ya kusema kwamba mna haki ya kukaa na shilingi bilioni 256, yet Waziri husika anakuja hapa mbele anatuambia kwamba tunazo dawa katika hospitali, it can’t be. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge, kuna Taarifa nyingine kutoka kwa Mheshimiwa Khadija Shaaban Taya.

T A A R I F A

MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwambie mzungumzaji Mheshimiwa Agnesta kwamba sasa hivi tunajadili kuhusu Hotuba ya Waziri Mkuu, hatujaanza bado kujadili Hotuba ya CAG, nashukuru sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Agnesta Lambert.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kwa sababu nafahamu na kutambua kwamba Mheshimiwa Khadija anafahamu fika kabisa kwamba anachokisema sicho kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niendelee kujikita katika ushauri kuhusiana na jambo hili kwa upande wa Serikali. Kwa sababu ikiwa tutakuwa hatuna chombo hiki maalum au mamlaka maalum ambayo itadhibidi bei za dawa pamoja na vifaa tiba, mwisho wa siku tutakuwa na Watanzania ambao usiku na mchana wanaumwa na magonjwa madogo lakini wanakosa dawa ambazo kimsingi dawa hizo zilipaswa kuwepo. Kauli mbiu ya Serikali ya sasa ni ushindani wa viwanda na maendeleo ya watu iende sasa ikajielekeze katika kulipa hizi shilingi bilioni 256 ili mwisho wa siku MSD waweze kuleta dawa kwa wingi kuliko ilivyo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia hapa wengine wanachangia, Waziri alikuwa anajibu anasema dawa zipo, hakuna kitu kama hicho. Ni knowledge ya kawaida tu MSD wanategemea Serikali ilipe madeni na wenyewe waende kuagiza dawa, lakini mwisho wa siku MSD inaonekana imekuwa na yenyewe ikikopa kule inakoagiza dawa. Kwa hiyo, inafika sehemu ambayo haiwezi tena kuagiza mpaka Serikali iweze kulipa madeni. Kwa kipindi hiki ambacho tunapitia katika mlipuko wa wimbi la pili la Covid-19 ni vema basi Serikali hii ikafanya kwa vitendo kulipa hili deni ili mwisho wa siku tuweze kuhakikisha kwamba tunaona hili suala la Covid-19 hatupati shida ya dawa katika hospitali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukosefu wa hii mamlaka ambayo nimeisema mwisho wa siku Watanzania wanakwenda kununua dawa katika pharmacy wanakutana na bei ghali sana. Hii ni kwa sababu wafanyabiashara wa dawa hizi hawana kitu kinachowa-limit kwamba dawa hii inapaswa kuuzwa kwa bei kuanzia elfu moja mpaka elfu tano. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)